Home Kitaifa Ripoti yafichua ufisadi wa kutisha jumuiya ya watumia maji

Ripoti yafichua ufisadi wa kutisha jumuiya ya watumia maji

by Jamhuri

MOSHI

NA CHARLES NDAGULLA


 
Ripoti ya ukaguzi maalumu uliofanywa na wakaguzi wanane kutoka Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro kwenye Jumuiya ya Watumiaji Maji ya Kirua Kahe (KKGWST), imefichua mambo ya ajabu, ukiwamo ufisadi na mkandarasi kulipwa pesa taslimu.
Mbali na wazabuni kulipwa pesa taslimu, ripoti hiyo imeibua madudu ya kutisha ikiwamo kampuni ya kusambaza mabomba pia kupewa kandarasi ya kutengeneza magari ya jumuiya hiyo licha ya kutokuwa na karakana ya kutegeneza magari.
Mzabuni huyo ni Kampuni ya RIL Solution ambayo ililipwa Sh 18,711,480 na kati ya hizo Sh 6,851,600 zilitumika kutengeneza magari ya jumuiya hiyo huku Sh 11,859,820 zikiwa hazina maelezo ya kazi iliyofanyika.
“Upungufu uliopo ni pamoja na kampuni ya vifaa vya mabomba kuhusika kutengeneza magari lakini hakuna taarifa za ushindani wa manunuzi haya pamoja na kazi zilizofanyika,” inasema sehemu ya ripoti hiyo ambayo JAMHURI ina nakala yake.
Jumuiya hiyo inadaiwa kulipa pesa taslimu Sh 108,441,695 kwa ajili ya kazi ya PRT, mradi wa solar eneo la Njiapanda, ununuzi wa pampu, kufanya matengenezo pamoja na usimamizi wa kazi mbali mbali.
Ripoti hiyo inafichukua kuwepo kwa upungufu mwingi kwenye malipo hayo na kwa mujibu wa taarifa ya mapato na matumizi ya jumuiya hiyo, malipo ya Sh 86,162,695 yanaonekana kulipwa kwa RIL Solution, mzabuni ambaye alifanya kazi ya kuweka solar kwenye kisima cha Njiapanda.
Hata hivyo, taarifa ya benki kwa mujibu wa ripoti hiyo inaonyesha kuwa malipo hayo yalilipwa kwa Kirua Kahe badala ya mzabuni (Ril Solution) na kwamba fedha hizo zilichukuliwa taslimu na menejimenti ya jumuiya hiyo na mzabuni kulipwa fedha taslimu.
“Kwa hali hii ni vigumu kuthibitisha kama Sh 86,162,695 zililipwa kwa Ril Solution na kama thamani ya mradi huo inafanana na kiasi hicho cha fedha, jumuiya ya KKGWST imekuwa ikinunua pampu kwa ajili ya ukarabati wa visima vya maji Kilototoni pamoja na kisima cha Njiapanda lakini wakati wa ukaguzi hatukuweza kuona pampu zilizoharibika zikiwa zimehifadhiwa stoo,” inaeleza ripoti hiyo.
Timu hiyo ya wakaguzi ikatoa mapendekezo kwa jumuiya hiyo ikiwamo kufuata taratibu za manunuzi kama zilivyoelekezwa na Sheria ya Manunuzi ya Umma na kanuni zake (PPA 2011 na PPR 2013) na kuwasilisha kwa mkaguzi nyaraka za mradi wa ukarabati wa miundombinu ya maji Kilema kwa ajili ya uhakiki.
Mapendekezo mengine ni menejimenti ya jumuiya hiyo kuwasilisha kwa maandishi sababu za kutoa benki Sh 86,162,695 na kumlipa mkandarasi kwa fedha taslimu na kuagiza ukaguzi wa kiufundi ufanyike katika miradi ya Kilema na mradi wa solar Njiapanda ili kubaini thamani ya fedha iliyotumika.
Mambo mengine yaliyoibuliwa katika ukaguzi huo ni pamoja na jumuiya hiyo kukusanya mamilioni ya fedha na kushindwa kuzipeleka benki kinyume cha sehemu ya nane ya mwongozo wa fedha za jumuiya wa mwaka 2019.
Inaelezwa kuwa kati ya Januari 2017 na Juni 2019 jumuiya hiyo ilishindwa kupeleka benki kiasi cha Sh 382,446,299.
Ripoti hiyo imeonya kuwa kitendo hicho kinaleta hatari ya fedha hizo kutumika bila kufuata taratibu, kuibwa, wateja wapya kutopata huduma ya maji kwa wakati na kupotea na kusababisha hasara kwa jumuiya.
Ukaguzi huo maalumu ulifanywa katika kipindi cha Januari 2017 hadi Juni mwaka huu na ripoti imesainiwa na Dyoya J. Dyoya ambaye ni Mkaguzi Mkuu wa ndani kutoka Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro.
Timu hiyo ya wakaguzi wa ndani iliteuliwa na Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro kwa barua yenye Kumb. Na. AD. 208/283/01 ya Agosti 23, mwaka huu iliyoagiza wakaguzi hao kufanya ukaguzi maalumu katika jumuiya mbili za watumia maji za Kilema Kusini na Kirua Kahe.
JAMHURI  limemtafuta Mwenyekiti wa Bodi ya watumiaji maji ya Kirua Kahe, John Macha kwa ajili ya kupata kauli yake juu ya tuhuma zilizoibuliwa katika ukaguzi huo, lakini kwa zaidi ya wiki mbili sasa amekuwa akipiga danadana kutoa kauli yake.
Badala yake mwenyekiti huyo akahoji kama mwandishi anayo ripiti hiyo na alipoelezwa kuwa anayo alikiri kuitambua na kudai si yote yaliyoainishwa kwenye ripoti hiyo ni ya kweli, japo hakuchanganua ni yapi yenye ukweli na yapi yasiyo ya kweli.
Naye Ofisa Uhusiano wa jumuiya hiyo, Charles Lyimo, amekataa kuzungumzia ripoti hiyo na kutaka atafutwe Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro kwa kile alichodai yeye ndiye ana majibu sahihi juu ya ripoti hiyo.
“Mwenye majibu ya hayo maswali ni katibu tawala na mwaka 2017 sikuwa Kirua Kahe nilikuwa Mwananchi Communications nikiandikia Gazeti la Mwananchi. Mcheki tu Katibu Tawala kaka, kila kitu anacho yeye atakupa utakamilisha tu stori yako,” anasema katika ujumbe wake mfupi wa maandishi alioutuma kwa mwandishi wetu.
Hata hivyo, Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Habibu Kazungu, amesema taarifa hiyo haijamfikia ofisini kwake, hivyo kukataa kuizungumzia, ingawa JAMHURI lina taarifa kuwa ripoti hiyo ipo ofisini kwa katibu tawala huyo.
 
MWISHO.

You may also like