Jose+Mourinho+Real+Sociedad+v+Real+Madrid+NbI6HcXwrYCx copy copyKwa mashabiki wa soka barani Afrika, Ligi Kuu ya England ndiyo kila kitu, ndiyo eneo lao la maabadi. Nembo hii ya kimataifa katika soka inafuatiliwa na zaidi ya watu bilioni moja kote duniani na watu milioni 260 kati ya hao wapo barani Afrika.

Wakati msimu mpya wa mwaka 2015-16 ukianza, majumba ya starehe na migahawa kutoka Cape Town hadi Cairo, itakuwa ikijiandaa kukidhi mahitaji ya mashabiki wengi watakaokuwa wakifika kushudia kipute hicho kwenye runinga kubwa kubwa zilizotundikwa ukutani.

Lakini ni timu gani ambayo ni maarufu zaidi katika bara hili? Huenda tusiweze kabisa kujibu swali hili kikamilifu, japo utafiti uliofanywa na ‘twitter’ unatupa sura ya wastani, kwa kukadiria idadi ya jumla ya watu katika kila taifa ambao wanafuata anwani rasmi ya timu za Ligi Kuu England kwenye ‘twitter’ na kisha kuziainisha tarakimu hizo katika asilimia kwa kila klabu.

 

Magharibi

Hapana shaka Chelsea ndiyo maarufu zaidi katika eneo hili. Hutoweza kuzungumzia Ligi Kuu nchini England katika eneo la magharibi mwa Afrika bila kuwazia Didier Drogba, Solomon Kalou, Samuel Eto’o, Victor Moses, Michael Essien na John Mikel Obi, wote ni wenyeji wa Afrika Magharibi ambao wameichezea The Blues.

Hata hivyo, Drogba ndiye mashuhuri zaidi kutokana na mafanikio yake nje na ndani ya uwanja. Hapana shaka kwamba alikuwa mshambuliaji mahiri katika klabu hiyo, akifunga bao la ushindi kwa mkwaju wa penalti na kuisaidia Chelsea kunyakua taji la Ligi ya Mabingwa mwaka 2012, na pia kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Afrika Magharibi kufunga jumla ya mabao 100 katika Ligi Kuu England mwaka huo.

Kadhalika, Drogba anaheshimika sana nyumbani Ivory Coast kwa juhudi zake za kueneza amani baada ya mzozo ulioibuka kati ya mwaka 2010-2011, na ameanzisha wakfu wake kuimarisha afya na elimu katika taifa hilo.

 

Mashariki

Chaguo la wengi katika eneo la Afrika Mashariki ni rangi nyekundu ya Arsenal. Umaarufu mkubwa zaidi wa The Gunners katika eneo hili unaweza kuwa ulitokana na dhana ya kuwa timu ‘isiyoweza kushindwa’, baada ya timu hiyo kuvunja rekodi katika msimu wa mwaka 2003-04 kwa kunyakuwa ligi bila kupoteza mechi yoyote, ilicheza mechi 49 bila kupoteza yoyote.

Mafanikio ya wachezaji wa Kiafrika kama vile Nwankwo Kanu, Emmanuel Adebayor, Kolo Toure na Lauren ilifanya Arsenal kuwa maarufu zaidi. Kanu bila shaka ndiye sababu ya Arsenal kupata umaarufu mkubwa nchini Nigeria.

Jambo la kushangaza ni kwamba Afrika Mashariki imepata kutuma mchezaji mmoja pekee katika Ligi Kuu nchini England – mchezaji wa timu ya taifa ya Kenya na klabu ya Southampton, Victor Wanyama.

 

Kusini

Siyo jambo la kushangaza kuwa Manchester United ndiyo timu mashuhuri zaidi katika eneo la kusini mwa Afrika.

Manchester United ndiyo timu yenye mafanikio makubwa zaidi katika historia ya Ligi Kuu England, baada ya kushinda jumla ya mataji 13 tangu Ligi hiyo ianze mwaka 1992.

Pia Man U iliwahi kumsajili mmoja wa wachezaji mashuhuri zaidi wa Afrika Kusini, Quinton Fortune, aliyewachezea Red Devils kwa kipindi cha miaka saba.

Fortune pia ni mmoja wa wachezaji wengi wa zamani wa Man UTD wanaozuru eneo hilo kila mwaka kutangaza timu hiyo. Afrika Kusini ilikuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuwa na chama cha wapambe wa Manchester United.

 

Kaskazini

Kwa watu wa Afrika Kaskazini, Arsenal ndiyo timu maarufu zaidi. The Gunners inawakilishwa vilivyo nchini Morocco, Algeria na Tunisia.

Vyama vya wapambe wa klabu hiyo katika mataifa haya vimesaidia kuipa klabu hiyo umaarufu kupitia mashindano kama vile mbio za kila mwaka za “Be a Gunner. Be a Runner”.

Lakini nchini Misri, ni Chelsea ndiyo inayotawala. Hii ni baada ya timu hiyo kumnunua Mohamed Salah kwa kima cha dola milioni 17 au pauni  milioni 11  Januari 2014.

 

Timu za Ligi Kuu England zenye ufuasi mkubwa zaidi kwenye ‘twitter’:

Arsenal – wafuasi milioni 6.14

Chelsea FC – wafuasi milioni 5.92

Man Utd – wafuasi milioni 5.73

Liverpool FC – wafuasi milioni 4.64

Man City FC -wafuasi milioni 2.59

By Jamhuri