Hivi karibuni timu ya soka inayomilikiwa na Mamlaka ya Mapato ya Uganda (URA), ilitua hapa Tanzania kucheza mechi kadhaa za majaribio.

Timu hiyo ambayo ni moja ya timu bora katika ukanda wa Afrika Mashariki, ilicheza na Wekundu wa Msimbazi Simba Sports Club, Dar es Salaam Young Africans (Yanga) yenye makao yake makuu kona ya mitaa ya Jangwani na Twiga, zote za jijini, na Wagosi wa Kaya Coastal Union ya Tanga.

 

Wekundu wa Msimbazi walipigwa kumbe la mabao 2-1 kabla ya watani wao wa jadi Yanga kulazimishwa sare ya mabao 2-2. Mechi zote zilichezwa Uwanja Mkuu wa Taifa Dar es Salaam.

 

Akizungumza katika mahojiano na JAMHURI jijini hivi karibuni, Kocha wa URA, Paul Nkata, amesema amegundua kuwa Yanga ina kikosi kizuri ikilinganishwa na kile cha Simba.

 

Amefafanua kuwa Yanga wanacheza mpira wa kuelewana zaidi, na hasa pale wanapoamua kutafuta bao la kusawazisha. Katika mechi yao na Yanga, URA walikuwa wa kwanza kupata mabao mawili kabla ya kiungo wa kimataifa wa Yanga, Haruna Niyonzima, kusawazisha magoli yote mawili.

 

Aidha, kocha huyo amesema Simba bado wanahitaji muda zaidi wa kufanya mazoezi waweze kuelewana, na kuongeza kuwa ni wazuri sehemu ya winga tu, huku akipendekeza kuwa sehemu nyingine wanatakiwa kuzifanyia marekebisho kabla hawajaanza Ligi Kuu ya Soka ya Vodacom Tanzania.

 

Baada ya mechi hizo dhidi ya URA, Simba na Yanga wameingia katika mchakato wa kutaka kumsajili mfungaji bora wa mechi hizo, Lutimba Yoyo, ambaye ndiye mfungaji wa magoli yote katika mechi mbili. Timu hizo zinamhitaji mshambuliaji huyo aliyeonesha umahiri mkubwa katika soka. Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara inatarajiwa kuanza Agosti 24, mwaka huu.

 

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeshatangaza ratiba inayoonesha kuwa Yanga na Simba zitafungua dimba kwa kupepetana na timu zilizopanda daraja Ligi Kuu msimu huu. Yanga watakwaana na Ashanti United katika Uwanja wa Taifa jijini wakati Simba watasafiri kwenda Tabora kumenyana na faru mkubwa (Rhino Rangers) katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.

 

Mechi nyingine za ufunguzi ni kati ya Mtibwa Sugar ya Manungu Morogoro na Azam FC ya Dar es Salaam katika uwanja wa Manungu, JKT Oljoro itaoneshana umahiri na Coastal Union ya Tanga katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha.

 

Mgambo JKT watakutana na maafande wenzao wa  Ruvu JKT katika Uwanja wa nyumbani wa Mgambo (Mkwakwani) Tanga, wakati Ruvu Shooting itakuwa na kibarua cha kuchuana na Tanzania Prisons ya Mbeya katika Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani.

By Jamhuri