Bei ya gesi asilia ambayo imegeuzwa kuwa kimiminika (LNG) inayotumika kwa wingi mijini kwa ajili ya kupikia, imepanda katika siku za karibuni.

Kupanda kwa bei ya gesi hii kunakuja wakati Watanzania wakisubiri mustakabali wa malalamiko yao kuhusu kupanda kwa gharama za kutuma na kupokea fedha mitandaoni, maarufu kama ‘kodi ya kizalendo’.

Lakini pia kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia kunatishia kupanda kwa nauli nchini, sambamba na kupanda kwa gharama za maisha ya siku hadi siku.

Inafahamika kwamba ni muhimu kuhakikisha misitu inahifadhiwa kwa kuwa hii ni moja ya rasilimali bora tuliyozawadiwa na Mwenyezi Mungu, inayoshikilia mustakabali wa uhai wa binadamu.

Kupanda kwa bei ya gesi ya kupikia wakati huu Watanzania wakihamasishwa kutafuta nishati mbadala kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, ni hali inayotishia sekta ya uhifadhi, hasa uhifadhi wa misitu.

Wakati mitungi ya sasa ya gesi ilipoanza kuuzwa kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nne, wananchi waliahidiwa kuwa bei ya gesi hiyo itakuwa rafiki ambayo kila Mtanzania ataimudu ili matumizi ya mkaa na kuni yadhibitiwe.

Watanzania walihamasika na watu wa mijini wakawanunulia ndugu zao, hasa wazazi wanaoishi vijijini, wapunguze matumizi ya mkaa na kuni; na mara kwa mara wamekuwa wakiwatumia fedha za kujaza gesi inapokwisha.

Ni bahati mbaya kwamba tangu wakati huo bei ya mitungi ya gesi imeendelea kupanda na kwa kasi iliyopo sasa, kuna hatari watu wakarejea kwenye matumizi ya kuni na mkaa; huko ambako tulipaswa kuwa tumekwisha kuondoka muda mrefu.

Pamoja na ukweli kwamba Tanzania kama taifa hatuna uwezo wa kudhibiti kupanda au kushuka kwa bei ya bidhaa muhimu kama gesi na mafuta katika soko la dunia, tunapaswa kufanya mambo kadhaa muhimu kwa Watanzania wa sasa na vizazi vyetu.

Ni vema sasa serikali ikatazama namna ya kuruzuku nishati hii muhimu inayopaswa kutumiwa na watu wa aina zote, badala ya wenye kipato cha juu na cha kati pekee wanaoishi mijini.

Bei ya gesi isiruhusiwe kupanda kiholela, kwa kuwa kupanda kwake kuna athari kubwa katika mazingira zitakazoonekana zaidi baadaye. 

Ni vema mamlaka husika zikatazama si tu namna ya kudhibiti kupanda kwa bei ya gesi ya kupikia, bali pia kuishusha bei hiyo ili nishati hii isambae katika kila kona ya nchi na kuwa mbadala halisi wa kuni na mkaa, tofauti na ilivyo kwa sasa.

By Jamhuri