RITA kuondolea adha uhakiki wa vyeti

DAR ES SALAAM

Na Aziza Nangwa

Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) umewataka wanafunzi wanaohakiki vyeti vya kuzaliwa kwa ajili ya mikopo kuzingatia maelekezo ili iwe rahisi kupata huduma.

Ofisa Habari wa RITA, Grace Kyasi, amelieleza JAMHURI kuwa kuna baadhi ya wanafunzi hukosea hatua za kutuma maombi ya uhakiki wa vyeti.

“Wengi wanatumia barua pepe ya Wakala ambayo ni [email protected] badala ya kutuma maombi kupitia ukurasa wa huduma mtandaoni unaojulikana kama E-huduma.

“Katika hatua hii mwanafunzi anatakiwa kuingia kwenye tovuti yetu; www.rita.go.tz, kisha aingie kwenye E-huduma na kutuma taarifa zake kwa urahisi,” anasema Grace. 

Anasema ili maombi yapokewe na kufanyiwa kazi kwa ufasaha, mwanafunzi anatakiwa kujisajili kwa kutengeneza akaunti katika ukurasa wa RITA huduma mtandaoni.

Grace anasema hadi sasa maombi 84,387 yameshahakikiwa na kurudishwa kwa wanafunzi kuendelea na utaratibu wa kuomba mikopo.

“Lakini pia tunapenda kuwakumbusha wanafunzi kutumia simu yetu ya huduma kwa wateja ambayo ni 800 117 482 iwapo watahisi kupata changamoto yoyote katika utumaji wa maombi yao,” anasema.

Grace ametoa wito kwa wananchi kutembelea banda la RITA katika Maonyesho ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia katika viwanja vya Mnazi Mmoja kufahamu huduma zinazotolewa na wakala huyo.

RITA wameshiriki maonyesho hayo yanayoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), ambapo katika banda lao wanatoa huduma ya usajili wa vyeti vya kuzaliwa pamoja na elimu kwa umma kuhusu huduma ya vizazi, vifo, ndoa, talaka, udhamini, ufilisi, wosia na mirathi.

Uzinduzi wa maonyesho hayo ulifanywa na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Zena Ahmed Said.