DC: Wastaafu msioe watoto, mtakufa 

ARUSHA

Na Bryceson Mathias

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Sophia Mjema, amewaasa wastaafu kutotumia mafao watakayopata kuoa watoto wadogo au kuolewa na vijana, akisema watawasababishia kufa kwa kihoro.

Sophia ameyasema hayo wakati akifungua semina ya elimu kwa wastaafu watarajiwa zaidi ya 400 wa Mkoa wa Arusha.

Semina hiyo ni maalumu kwa uwekezaji kwa maisha endelevu baada ya kustafu na imeandaliwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).

Akifungua semina hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, DC Sophia anasema:

“Akina baba wastaafu, mkipata mafao msiende kuoa wasichana wadogo wadogo, na akina mama msiende kuwaweka ndani vijana wadogo wadogo, mkilizwa mtakufa haraka.

“Akina baba wastaafu andaeni maisha yenu vizuri na kujikinga na maradhi, msikimbilie kununua (kuoa) magari madogo.”

Kwa upande wa akina mama wastaafu, Sophia amewaasa akisema fedha watakazopata ni zao si za wajukuu.

“Hao wajukuu ni wa watoto wenu, na kama mkienda kuwatembelea msiende kuwavuruga, ukienda kwao kapange hotelini,” anasema.

DC huyo amewataja anaowaita ‘matapeli’ ambao hujiweka karibu na mtu anayekaribia kustaafu kuwa ni matumizi yasiyo ya lazima, familia, ujenzi wa nyumba kubwa (ghorofa) wakati familia ni ndogo pamoja na ulevi wa kupindukia.

Taasisi tisa za benki ambazo ni wadau wa PSSSF wameshiriki kutoa elimu kwa wastaafu.