Na Angalieni Mpendu  

Rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa. Msemo wa ilani hii umesemwa miaka mingi katika nchi yetu, tangu awamu ya kwanza hadi hii ya nne ya utawala wetu huru wa Watanzania.
  Nasema kabla nchi yetu kuwa huru, enzi ya ukoloni rushwa ilikuwapo, lakini ilikataliwa na kuogopwa mithili ya mnyama simba msituni anavyoogopwa na wanyama wenzake na sisi binadamu.


  Viongozi wa watawala wa awamu ya kwanza ya utawala wetu, walisema tuiogope rushwa kama ugonjwa wa ukoma kwa sababu ukoma ni ugonjwa wa kuambukiza wa mabatomabato ambao unaharibu mishipa ya fahamu na kukata viungo vya mwili. Ni ugonjwa hatari sana.
  Viongozi wa Serikali na chama cha siasa, TANU/CCM walitoa elimu kuhusu madhara ya rushwa na adhabu kali zilitolewa kwa watu waliobanishwa kuwa wametoa au kupokea rushwa. Sababu rushwa ni adui wa haki.


  La kushangaza na kusikitisha, rushwa imejichomoza kutoka mafichoni na kuzagaa nchi nzima hata kuonekana ni kanuni na moja ya tabia na desturi ya mwenendo wa maisha ya Watanzania. Inasikitisha.
  Zipo sababu kadha wa kadha zilizofanya rushwa kuzagaa hata kufikia hatua hiyo. Baadhi ya sababu ni kukosa uzalendo, uadilifu wa pupa ya kupenda na kutaka kujilimbikizia mali mapema zaidi.


  Kukosa uwezo wa kushughulikia mambo, ukosefu wa taaluma, uzoefu, tamaa na chuki ni baadhi ya sababu zinazofanya watu kupenda kutoa na kupokea rushwa. Hayo ni maradhi mabaya na makubwa mno.
  Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alichukia rushwa. Alikemea na aliwaadhibu watoa na wapokea rushwa. Alisema kuwa nchi yetu inanuka rushwa, na lawama alizielekeza kwenye chama chake cha siasa – CCM na Serikali.
  Nazungumzia rushwa kwa sababu mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi. Watanzania tunajiandaa kuchagua viongozi wetu katika ngazi ya kata, jimbo na nchi kwa maana ya kumchagua diwani, mbunge na Rais.


  Tayari watu wameanza minong'ono na kutamka kuwa zipo dalili za baadhi ya wagombea uongozi kuweka vikundi vya watu kusimamia mchakato wa kutoa na kupokea rushwa ili wawe viongozi wa kuongoza nchi.
  Binafsi, nimeanza kusikia siasa za kuchafuana wanaofanya siasa hizo wanatumia fedha kutoa kama misaada, huruma na ibada za dini ilhali ni kupenyeza rushwa eti kuwapumbaza wananchi, wao ni watu wema.


  Makundi hayo yanaendesha mchakato ndani ya vyama vya siasa, jumuiya za dini, vyombo vya utetezi wa haki, kwenye maskani na vijiweni, na Serikali ikiaminishwa wafanyao hivyo ni watu wema na wenye huruma kwa jamii.
  Mchakato huu si mzuri kwani unadhalilisha utu wa mtu, unajenga chuki kati ya mgombea na mpiga kura, kati ya mgombea na mgombea na kati ya mpiga kura na mpiga kura, kila mtu anamuona mwenzake si bora, bora ni yeye.


  Mambo hayo yamekwishatokea katika chaguzi zilizopita na sasa kwajengeka imani kama huna fedha ya kuhonga hupati uongozi. Ndiyo maana leo karibu sehemu kubwa ya viongozi wameingia madarakani kwa njia ya rushwa!
  Kutoa rushwa ndiyo sifa ya kupata uongozi, lakini si kutoa rushwa tu; hapana. Rushwa hiyo ni kubwa kiasi gani na inawezesha jambo gani katika harakati au maendeleo ya mtu. Enzi za kuamini, kufuata na kutambua uwezo, elimu ujuzi na kipaji cha kuelewa mambo, wa kutenda kwa maana ya kutimiza majukumu, wajibu na ahadi haipo! Liliopo ni fedha, Rushwa. Rushwa ndani ya mioyo!
  Kelele, vilio na masikitiko dhidi ya rushwa hayatakwisha kama hatutaweka dhamira ya kwenda ndani ya vyama vya siasa kuondoa rushwa. Tuweke nia kujikomboa, ukombozi wetu una maeneo mengi.
 
Itaendelea

0717/0787 113542

1176 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!