Msimamo wa kutaka kila kitu kifanyike bila ubabaishaji katika kamati na wizara zinazomhusu, umetajwa kuwa ndio unaomgharimu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.

Miongoni mwa nyadhifa kubwa alizo nazo katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni pamoja na ujumbe wa Kamati ya Maadili, Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho.

Lakini pia, kwa sasa Lukuvi ni Mbunge wa Jimbo la Isimani mkoani Iringa. Alipata kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Vijana, nafasi ambazo inaelezwa amezitumikia kwa mafanikio makubwa.

Vyanzo vya kuaminika kutoka ndani ya CCM vimeidokeza Falsafa mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba uadilifu wa Lukuvi katika nyadhifa mbalimbali alizo nazo ndani ya chama hicho tawala na serikalini ndio sababu kuu ya kuelekezewa mashambulizi ya kumchafua mbele ya umma.

Katika siku za karibuni, Waziri Lukuvi ameandamwa na mashambulizi kutoka kwa baadhi ya watu wakiwamo wanasiasa wa upinzani, wakimtuhumu kwamba ametumia nyumba ya ibada kupigia debe muundo wa serikali mbili na kutoa vitisho dhidi ya muundo wa serikali tatu.

Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ukiongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, ulimtuhumu Lukuvi kuwa ametumia sherehe za kumsimika Askofu wa Kanisa la Methodist mkoani Dodoma, Josephat Bundala, kuwatisha wananchi kwamba endapo muundo wa serikali tatu utapita, Jeshi litafanya mapinduzi na nchi kuongozwa kijeshi.

Kwa upande mwingine, Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (JUMIKI), imemtumia barua Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta, kueleza tuhuma zilizotolewa na Lukuvi kwamba inahusika na vitendo vya uvunjifu wa amani.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya JUMIKI, Yusuph Khamis, alisema kauli za Lukuvi zinaligawa Taifa kwa misingi ya kidini jambo ambalo lilipigwa vita na waasisi wa Taifa.

Aliongeza kuwa tuhuma kwamba Uamsho inaeneza itikadi za CUF si za kweli kwa sababu jumuiya yao haina ushirika na chama chochote cha siasa, bali inafanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria.

Watu mbalimbali akiwamo Lukuvi mwenyewe, wamenukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari wakisema Lukuvi hakuwa na kosa na badala yake, kama raia na kiongozi alikuwa na haki ya kutoa maoni yake na kuwapa wananchi elimu ya uraia ili wanapoamua, waamue kile wanachokijua vema.

Hata hivyo, vyanzo vimesema kwamba tuhuma zote zinazoelekezwa kwa Waziri Lukuvi zina msukumo wa wanasiasa wa ndani na nje ya CCM wanaotetemeshwa na nguvu ya utendaji thabiti wa kiongozi huyo.

“Unajua huyu kada [Lukuvi] ana maadui wake ndani na nje ya chama chake kutokana na masimamo wake mkali. Hababaiki, hanunuliki wala kukubali kujiunga na makundi ya mtandao, ni mtu anayetaka kila kitu kifanyike waziwazi bila ubabaishaji,” kimesema chanzo cha habari.

Chanzo kingine kutoka ndani ya CCM kimesema, “Huyu Lukuvi kinachomponza ni msimamo wake wa kutokubali kutumika na kundi lolote kwa sababu pia ana nafasi nyingi za uongozi ndani ya CCM na Serikali. Lakini pia makada wenzake wanamtilia shaka kwamba atagombea urais ingawa yeye mwenyewe hajawahi kuomba, hana nia na wala hatarajii kugombea urais mbali ya majukumu anayopangiwa na kukabidhiwa.”

Alipohojiwa na Falsafa iwapo naye anaamini utendaji wake kupitia nyadhifa alizo nazo ndio sababu ya kuelekezewa mashambulizi, Waziri Lukuvi amesema kwa kifupi, “Siwezi kuzungumzia mambo hayo.”

Hata hivyo, hivi karibuni Lukuvi alikaririwa na vyombo vya habari alipoulizwa kuhusu tuhuma zinazoelekezwa kwake akisema, “Kauli ya Lukuvi ni kisingizio tu, wametafuta pa kutokea wameshindwa sasa wanang’ng’ania hoja zisizo na mashiko kutafuta huruma kwa watu na watu wengi wamekwishawashitukia.”

Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Methodist mkoani Dodoma, Josephat Bundala, amenukuliwa akisema anaamini kuwa kauli iliyotolewa na Lukuvi katika kanisa hilo siyo iliyowafanya wana UKAWA kususia vikao vya Bunge Maalum la Katiba, huku akisisitiza kuwa tangu mwanzo vikao vya bunge hilo vilikuwa vinatawaliwa na mabishano, itikadi za kisiasa na misimamo iliyosababisha misuguano mikubwa.

“Hawapo pamoja [wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba] ndiyo maana lilipotokea lile la Lukuvi, wakaona ndio mlango wa kutokea, ninaamini UKAWA watarejea bungeni baada ya kuzungumza na wenzao, hapa ni lazima wafanye maridhiano kulinda nchi,” amesema askofu huyo.

1219 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!