Novemba 11, mwaka huu, nilikuwa miongoni mwa watu waliohudhuria semina ya biashara na ujasiriamali katika ukumbi wa Matumaini Centre, uliopo Sabasaba Iringa mjini. Semina hii iliendeshwa na mtaalamu na mshauri wa kimataifa wa masuala ya biashara na ujasiriamali, Perecy Ugula, kupitia kampuni yake ya Great Opportunity Consulting Limited (GOC Ltd). Semina hii ilidhaminiwa na Benki ya Barclays Tawi la Iringa, kuadhimisha siku ya wafanyakazi wa benki hiyo. Waandaaji na wadhamini wa semina hii waliamua kuwafundisha wanawake na vijana wa kikundi cha Matumaini; mafunzo yaliyokuwa na dhima ya ‘ujasiriamali katika mtazamo mpana’. Mimi nilikuwa mmoja wa wageni walioalikwa na GOC Ltd.

Pamoja na kwamba nimekuwa nikichambua biashara na ujasiriamali katika magazeti, mitandao ya kijamii pamoja na blogs mbalimbali; kiukweli mafunzo niliyoyapata siku ile yamenifungua sana. Namna Mtaalamu huyu anavyofundisha, mbinu anazotumia, mvuto wa uwasilishaji mada zake pamoja na uzoefu wake uliotukuka katika ujasiriamali vyote, vilifanya ubongo wangu upate makali mapya.

 

Kutokana na hayo, nimepata bahati ya kumfahamu mkurugenzi huyu wa GOC Ltd, (Ugula) na timu yake. Kwa kweli wamejipanga kuleta msaada na mageuzi makubwa katika sekta ya ushauri wa kibiashara na ujasiriamali. Mkurugenzi Ugula ni muhitimu wa masuala ya kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), lakini ana mafunzo ya ngazi ya uzamili katika mambo ya uongozi wa ushirika.

 

Mbali ya hayo, amehudhuria mafunzo ya ujasiriamali ya Umoja wa Mataifa (UN) chini ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) na kutunukiwa cheti cha Mkufunzi wa Wakufunzi wa Ujasiriamali. Katika nyanja ya kimataifa, Ugula ni mmoja ya walimu (mentors) wanaowalea wajasiriamali vijana kutoka mataifa zaidi ya 120 duniani.

 

Malezi hayo yanafanyika kupitia mtandao wa YenMarketPlace. Mtandao huu una udhamini na mwongozo kutoka UN. Jambo la kufurahisha ni kuwa mtaalamu huyu na timu yake ya wataalamu wanafanya biashara na ujasiriamali wakiwa na kampuni na miradi mbalimbali ya huduma na bidhaa.

 

Hivyo, wanafundisha uhalisia na mambo wanayoyafanya. GOC Ltd tayari imeshafanya semina na mafunzo katika maeneo mengi Tanzania, hususan kwa vikundi, mashirika yasiyokuwa ya serikali na taasisi za kimataifa, ikiwamo Winrock International. Nilipoyajua haya nikatambua nimekutana na ‘dhahabu’!

 

Kutokana na ‘dhahabu’ niliyoibaini katika semina hii, nikaona si vema nikatawanyika pasipo kumdodosa mtaalamu huyu pamoja na huduma yake hii ambayo ni adhimu sana nchini kwetu (Tanzania). Kama ambavyo nimekuwa na shauku ya kuwashirikisha wasomaji wetu fursa na mambo mema katika biashara na ujasiriamali; leo nimeona niwashirikishe fursa hii ya mafunzo na namna yanavyoweza kuboresha biashara zenu.

 

Pengine nitangulie kusema mambo takribani mawili kuhusu ukienyeji wetu katika biashara na uzoefu kutoka kwa wenzetu. Wafanyabiashara wengi wa Tanzania tumekuwa tukifanya biashara kwa mazoea, kwa kienyeji na kubahatisha kwingi. Hatuna mbinu wala mafunzo ya kitaalamu kwa ajili ya kuendesha biashara zetu kwa tija.

 

Mambo ni tofauti sana kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wenzetu waliopo katika nchi zilizoendelea. Hata majirani zetu Wakenya wametuzidi katika utamaduni huu wa kuhudhuria semina, warsha, makongamano ama matamasha mara kwa mara kujipatia mbinu mpya za kibiashara. Unapohudhuria semina, makongamano ama warsha hizi unapata wasaa wa kupata mbinu mpya.

 

Semina hii ilipomalizika, nikamfuata mtaalamu huyu nikamueleza kwamba kuna wasomaji wetu ambao wametapakaa nchi nzima, ambao kila wiki wanafuatilia Anga za Uchumi na Biashara. Kiu ya wengi imekuwa ni kupata semina na maarifa ya ujasiriamali na biashara ambavyo vitawawezesha kusonga mbele.

 

Baada ya kumueleza haya, Ugula alinieleza kuwa kampuni yake ina majibu ya hitaji langu na lile la wasomaji wetu. Akatanabaisha kuwa madhumuni ya GOC Ltd ni kutoa huduma za ushauri wa kijasiriamali na programu za aina zote ziendanazo na biashara na miradi ya maendeleo.

 

Akanieleza wamekusudia kuziba ombwe la ukosefu wa maarifa, ujuzi, kanuni na mikakati endelevu miongoni mwa wafanyabiashara, taasisi za kimaendeleo, serikali pamoja na vikundi vingine vya kiuchumi zikiwamo SACCOS, FBOs na NGOs.

 

Pia akasisitiza kuwa kampuni yake imelenga kuwasaidia mtu mmoja mmoja, wale wote wenye kiu ya kufanikiwa kupitia ujasiriamali, wahitimu kutoka ngazi zote za elimu vikiwemo vyuo vikuu na makundi yanayojishughulisha na kuzisaidia jamii.

 

Katika kufuatilia machapisho yao, nikagundua GOC Ltd ni kampuni iliyokuja Tanzania wakati mwafaka. Nafahamu ombwe la maarifa lililopo miongoni mwa wajasiriamali nchi hii kutokana na namna wanavyonipigia simu, kuniandikia ujumbe kupitia simu na kompyuta pamoja na kukutana nami.

 

Wapo baadhi ya wasomaji ambao hufanikiwa kukutana nami, lakini ninapowasikiliza shida zao wengine huwa nashindwa hata nianzie wapi kuwasaidia kutokana na ukosefu mkubwa wa kujitambua, kujiamini na imani kwa biashara zao. Mbinu za useminishaji nilizokutana nazo kwa Perecy Ugula na kampuni yake ya GOC Ltd vinatoa majibu mengi kama sio yote kati ya yale yanayohitajika kwa wajasiriamali wengi.

 

Kwa kuwa maono ya kampuni hii ni kuwafikia na kufanya kazi na maelfu ya wadau wa maendeleo kwa njia ya ushauri wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii; huduma zao zimejielekeza katika maeneo matatu makubwa. Mafunzo maalumu ya elimu ya ujasiriamali yanayolenga kujenga uwezo uthubutu na ushindani katika biashara huku mbinu zenye viwango na ithibati ya UN vikitumika.

 

Huduma nyingine ni mafunzo na karakana (workshops) za kibiashara zinazolenga kutumbukiza maarifa ya kibiashara katikati ya watu wazoefu na wale walioanza biashara. Ni katika huduma hii ya pili ndipo ambapo wanaendesha usajili wa biashara na michanganuo ya miradi.

 

Pia wanasaidia uandishi wa michanganuo ya kibiashara kwa ajili ya kuombea mikopo katika benki pamoja na mbinu za kubaini, kuibua na kutumia fursa za kibiashara. Suala la ongezeko la thamani, kutafuta masoko na usimamiaji wa biashara ni mambo yaliyojumuishwa humu.

 

Huduma ya tatu wanayoifanya ni kutoa huduma za ushauri kwa kadiri ya mahitaji maalumu ya wahitaji. Hapa ndipo walinivutia sana; yaani ninyi kama ni kundi la wafanyabiashara, kikundi, VICOBA, ROSCAs ama SACCOs mnaweza kuwaita wataalamu hawa na kisha mkasema matatizo yenu halafu wao wakaandaa semina ama kifurushi cha mchanganuo unaojibu matatizo yenu kwa upana na usahihi.

 

Katika semina ile, tulifundishwa mambo mengi mazuri lakini mkufunzi huyu alitupatia zoezi ambalo liliniacha hoi na nikajiona kumbe ningali na ujinga mwingi katika biashara. Mkufunzi alitutaka washiriki tukae katika makundi matatu na tushikane mikono. Kisha akatuagiza kila mtu atulie kwa dakika kumi atafakari jambo lolote ambalo atalifanya ndani ya dakika tano.

 

Dakika kumi zikaisha na kila mmoja akatakiwa kufanya alichokifikiria. Wengine wakaanza kuhamisha viti, wengine wakakusanya chupa za maji, wengine wakaenda uani, wengine wakaanza kupigana picha; ilimradi tu ilikuwa vurugu ukumbini. Baadaye akachagua watu watatu waeleze nini waliwaza kukifanya na ikiwa wamefanikiwa au la!

 

Wa kwanza akasema alipanga kwenda uani (na amefanikiwa). Wa pili alipanga kupiga picha (na amefanikiwa). Wa tatu alipanga kukusanya chupa za maji (na amefanikiwa). Wa nne alipanga kupata namba ya mmoja wa washiriki (na hajafanikiwa). Katika mjadala uliofuatia kuhusu majibu hayo ndipo mkufunzi alitufumbua akili namna Watanzania tunavyoishi nusunusu tukiwa hatuna malengo yenye tija na yanayoelezeka.

 

Mathalani, akaeleza kuwa mtu unaposema unataka kupiga picha; je, nani kakutuma? Unapiga kwa malengo gani na nani atakulipa ama kuinunua? Unasema unataka kukusanya chupa za maji, ili iweje? Unazipeleka wapi na ni nini kimekusukuma kufanya unachofanya?

 

Awali, jambo hili lilionekana kuwa la kitoto lakini udadavuzi wa mkufunzi huyu ulifanya kila mshiriki kukiri kuwa atakwenda kufikiria upya kuhusu biashara yake na maisha yake kwa jumla. Ilidhihirika kuwa Watanzania wengi tunafanya mambo bila kuwa na picha kamili ya tunakoenda na mafanikio tunayotafuta.

 

Kwa mfano, kama una biashara ya duka; hivi umeshawahi kujiuliza utafanyaje siku ukiamka asubuhi na kukuta duka lote limeungua? Je, kwa miaka mingapi ijayo utaendelea kuifanya biashara hiyo ya duka? Je, kama ukifariki leo umemuandaa nani kuhakikisha duka lako si tu linaendelea bali pia linakua?

 

Nimeendelea kuwasiliana na mkurugenzi huyu, Ugula na timu yake ya GOC Ltd, kuangalia uwezekano wa kuzipeleka huduma zao kwa Watanzania wengi zaidi. Bahati nzuri wameniruhusu kumuunganisha mtu yeyote, kikundi, taasisi ama asasi yeyote itakayokuwa na uhitaji wa huduma zao.

 

Kwa maana hii ninafurahi kuwajulisha wasomaji wa Anga za Uchumi na Biashara, kwamba sasa popote ulipo unaweza kuwasiliana nami kwa ajili ya msaada na ushauri wa kibiashara na kiujasiriamali kupitia kampuni hii ya GOC Ltd. Wafanyabiashara, wajasiriamali na Watanzania wote ni wakati wa kuamka na kuchangamkia fursa za kunolewa bongo zetu ili kusogea mbali kimaendeleo.

 

Sote tunahitaji ushindi wa kiuchumi!

[email protected], 0719 127 901

 

 

 

By Jamhuri