Tumeuanza mwaka kwa bahati mbaya. Watanzania zaidi ya 40 wamefariki dunia katika matukio mawili makubwa.

Tukio la kwanza ni la vifo vya Watanzania 20 mkoani Lindi vilivyosababishwa na mafuriko. Tukio la pili ni la vifo vya Watanzania wengine kwa idadi kama hiyo vilivyosababishwa na kile kinachodaiwa kuwa ni ‘upako’ mjini Moshi. 

Tunawapa pole wote waliofiwa na wapendwa wao, pia tunawaombea wote waliojeruhiwa wapone haraka ili warejee kwenye harakati za maisha ya kila siku.

Tukio la Lindi lina maelezo yake, maana ni tukio la asili ambalo aghalabu kulikabili ni jambo gumu, japo siku hizi wananchi tunashauriwa kufuatilia na kuheshimu utabiri wa hali ya hewa.

Lakini tukio la Moshi ni la kusikitisha, kwa sababu ni la kuandaliwa! Katika hali ya kawaida haitarajiwi watu zaidi ya 10,000 waelekezwe kwenye mlango mmoja kwa ajili ya kukanyaga mafuta ya ‘upako’.

Tangu tumepata Uhuru mwaka 1961, serikali yetu ilijipambanua kwa kuweka wazi kuwa haina dini, lakini watu wake wana dini. Ndiyo maana tangu wakati huo Watanzania wamekuwa huru kuabudu dini kadiri ya imani zao.

Hata hivyo, uhuru huo wa kuabudu umeachwa kiasi kwamba kumeingia watu wenye nia njema ya kuleta wongofu, na wakati huo huo wameingia wenye misimamo ya kusaka faida zaidi.

Hatuna budi kuiga mambo mazuri yanayotendwa katika mataifa ya wenzetu. Majirani zetu, Rwanda, wameanzisha mpango mzuri, si wa kuyadhibiti makanisa, bali kudhibiti na hata kukomesha nyendo zisizo za kawaida ndani ya makanisa na nyumba nyingine za ibada.

Serikali isijiweke kando kwa kigezo kuwa haipaswi kuingilia uhuru wa kuabudu. Serikali ina wajibu wa msingi wa kuwalinda raia wake dhidi ya aina zote za madhila na hata utapeli.

Haiwezekani mambo yasiyo na maana yanayoonekana yaendelee kufanywa halafu serikali ijiweke kando kwa kigezo kwamba watu wana uhuru wa kuabudu. Ndiyo, watu wana uhuru wa kuabudu, lakini hawana haki ya kuibiwa, kulaghaiwa au kuuawa kwenye msongamano.

Tunatoa mwito kwa serikali kuitazama mifumo yote ya makanisa haya yanayochipuka kama uyoga na hatimaye uwepo ‘utaratibu elekezi’ utakaosaidia kuwatambua manabii na mitume wa ukweli na wengine ambao ni matapeli. Mabadiliko haya yanatakiwa yafanywe haraka kabla ya maafa makubwa kutokea.

By Jamhuri