Nini kimeikumba Stamico?

Wakati ikielezwa kuwa madini ni moja ya sekta ambazo zimewezesha kupatikana kwa mapinduzi ya uchumi nchini, taasisi muhimu inayoshughulikia sekta hiyo, Shirika la Madini la Taifa (Stamico) inaelezwa kuwa liko hoi kifedha.

Wakati Benki Kuu (BoT) ikieleza kupitia ripoti yake ya hali ya uchumi kwa mwezi Novemba mwaka jana kuwa madini (dhahabu) inaongoza katika kulipatia taifa fedha nyingi za kigeni kupitia mauzo ya bidhaa nje ya nchi, wiki iliyopita Bunge lilielezwa jijini Dodoma kuwa hali ya Stamico kifedha si nzuri.

Ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma iliyowasilishwa bungeni inaeleza kuwa hali ya shirika hilo kifedha ni mbaya kutokana na kuwa na matumizi makubwa yanayozidi kiasi cha fedha ambacho kinaingizwa.

Kwa mujibu wa kamati hiyo, matumizi ya Stamico yanazidi mapato yake ghafi kwa wastani wa asilimia 134 kwa ajili ya gharana za uendeshaji.

Ni jambo la kushangaza kuwa viongozi wa Stamico wamekubali kuiacha hali hiyo iendelee hadi inakuja kuibuliwa na Kamati ya Bunge ambayo imebainisha mathalani kuwa kwa mwaka 2016/17 matumizi ya Stamico yaliongezeka kwa asilimia 12 kutoka Sh bilioni 9.05 na kufikia Sh bilioni 10.61 mwaka uliofuata, huku mapato yakiporomoka kutoka Sh bilioni 6.33 hadi Sh bilioni 2.01.

Tunaungana na watu na taasisi nyingine kuhoji mantiki ya taasisi hii ya umma kuwa na gharama za juu za uendeshaji kuliko mapato yake. Hilo linaweza kutokana na sababu kuu mbili. Mosi, kuna uwezekano kuwa shirika limeshindwa kupanua wigo wa makusanyo ya mapato yake, hivyo kukusanya kiasi kidogo cha fedha ambacho hakikidhi mahitaji yake. 

Pili na dhahiri ni kuwa matumizi ndani ya shirika hilo ni makubwa sana kuliko makusanyo yake. Hapo ndipo watendaji wa Stamico wanapoacha maswali mengi ambayo yanahitaji majibu kutoka kwao.

Inakuwaje watendaji hao wanashindwa kupanga vema mipango yao ili kuhakikisha kuwa matumizi hayawi makubwa kuliko uwezo wa shirika kukusanya mapato? Hilo linaweza kufanyika kwa aidha kuongeza wigo wa makusanyo ya mapato au kupunguza matumizi. 

Kama viongozi wa Stamico wanashindwa kufanya hivyo, ni dhahiri kuwa watakuwa wameshindwa kazi. Haiwezekani wakatumia fedha nyingi kukusanya fedha chache. Hiyo ni biashara ya hasara moja kwa moja, kwa sababu biashara yoyote ili ilete faida, makusanyo yanapaswa kuwa makubwa kuliko matumizi.

Viongozi wa Stamico wajipime kwa hili na kufanya mabadiliko yatakayoleta mageuzi katika uendeshaji wa taasisi hiyo, la sivyo wataiyumbisha sekta nzima ya madini.