Nimesukumwa kuandika makala hii kwa ukweli kwamba hatuwezi kujenga taifa lenye maadili mema pasipo familia zenye maadili mema. Siku moja nilipita katika mtaa fulani nikakuta majibizano ya ajabu kati ya mtoto na mzazi, nilishangaa sana.

Ustawi wa taifa unaanzia nyumbani. Kinyume chake ni kweli. “Kuporomoka kwa taifa kunaanzia nyumbani.’’ Ni methali ya Kiafrika. Uhai wa taifa unategemea uhai wa familia. Tunapaswa kutambua kuwa mafanikio ni tunda la bidii.

Methali ya Kichina inasema: “Ukinieleza nitashauri.’’; “Ukinionyesha nitasahau.’’;  “Tukishirikiana nitaweza.” Ni hakika wazazi na walezi wana ulazima wa kushirikiana katika malezi na makuzi ya watoto. Metahali hiyo inaupambanua ukweli mwingine kwa kusema: “Hali ya nchi inaonekana nyumbani.”

Papa Yohana Paul wa II alipata kuandika: “Namna familia inavyokwenda ndivyo taifa linavyokwenda na ndivyo dunia yote inavyokwenda.”  Maadili mema ni uhai, maadili mema ni uhai kwa taifa, maadili mema ni uhai kwa familia.

Hakika jamii ya ulimwengu haiwezi kukataa ukweli wa Hans Kung kwamba: “Pasipo maadili hakuna uhai.” Hatuwezi kuendelea kiroho, kimwili, kiuchumi, kisiasa na kijamii pasipo kuwa na maadili yanayompendeza Mungu na binadamu wenzetu wanaotuzunguka.

Matatizo mengi yanayoikabili jamii yetu yana chanzo chake katika tabia. Tabia ndiyo chanzo cha matendo tunayoyaona kama kukosekana kwa uaminifu, ubadhirifu wa mali za umma, ufisadi, migogoro ya ndoa, misuguano ya kijamii, ugaidi, unyanyapaa na kadhalika.

Yote haya yana chimbuko lake. Mtoto anapozaliwa ni kama malaika, hana kosa anapokuwa amezaliwa. Anakuwa mgeni aliyeleta habari njema kwenye familia. Wazazi, ndugu na jamaa hufurahi kumpokea mtoto aliyezaliwa. Jambo gani linatokea baadhi ya watoto wanapokuwa wanabadilika?

Tunapokuwa tunazungumzia maadili ya ulimwengu wa sasa kwamba yameyumba, lazima kwanza tutupie jicho letu kwenye familia zetu. Tuelewe kwamba jukumu la kujenga taifa letu ama kulibomoa taifa letu tunalo sisi wazazi, walezi na wanajamii.

Mwandishi wa Kitabu cha Mithali ameandika kwa ufasaha kabisa kwamba: “Mlee mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha hata atakapokuwa mzee.’’ (Mithali 22:6). Na wahenga wetu walipata kunena: “Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.”

Mtoto ni malezi, malezi bora ni ufunguo wa maisha kwa mtoto. Malezi bora ni urithi wa milele kwa mtoto. Taifa bora la kesho linategemea malezi bora yanayotolewa na taifa bora la leo, malezi bora ndio mwelekeo sahihi wa maisha ya mtoto.

Watoto wa leo ni raia na viongozi wa kesho, ndio watakaokuwa sifa au aibu kwa wazazi, familia na taifa lao.

Papa Francis ameandika kwa ufasaha usiopingika: “Mtoto ambaye amejifunza katika familia kuwasikiliza wengine, kuzungumza kwa heshima na kueleza maoni yake pasipo kupuuza ya wengine, atakuja kuwa na nguvu ya mazungumzo na mapatano katika jamii.”

Familia ni kitalu cha haki, amani na upatanishoFamilia bora hujenga jamii bora! Ndiyo maana tunathubutu kusema kwamba umaarufu wa jamii unatokana na familia zilizo safi.

“Familia ni jumuiya ya msingi, ndicho chanzo cha uhai mpya wa binadamu, ndicho kituo cha kwanza ambamo mtu anaweza kupata maendeleo ya kiroho,  kimaadili na kimwili kwa ukamilifu.”

Ni tafakuri iliyotolewa na Baraza la Maaskofu Wakatoliki wa Tanzania kupitia ujumbe wao wa Kwaresima wa mwaka 2010. Familia imara ni msingi wa taifa bora la nchi. Pasipo familia taifa halitakuwepo. Familia ni shule ya malezi na makuzi bora.

Familia ni shule ya kusamehe na kusamehewa, kupenda na kupendwa, ni mbingu ndogo ya wanafamilia ambapo watoto na wazazi wanaishi maisha ya upendo, undugu na urafiki.

Padri Festo Mkenda SJ anasema: “Upendo wa baba na mama ni mfano bora kwa watoto.” Uhusiano ulio imara wa taifa na wenye kujaa baraka hujengwa kwenye ngazi ya kifamilia. Ni ukweli kwamba ikiwa familia hazielewani, hata taifa halitaelewana.

Methali ya Kijerumani yatujuza: “Upendo huanzia nyumbani.” Mchungaji A. W. Tower alipata kusema: “Malezi bora kwa mtoto ni lulu kwa ulimwengu.” Kesho bora ya mtoto inajengwa na leo bora ya mzazi bora. Methali ya Kiswahili inatukumbusha maneno haya: “Samaki mkunje angali mbichi.”

By Jamhuri