Ndugu Rais, hivi karibuni wengi wamekuwa na shamrashamra, vifijo na nderemo huku wakiuaga mwaka 2018 na huku wakiushangilia mwaka 2019.

Wanasema ni upendeleo wamepewa kuufikia mwaka 2019 kwa sababu wengi walitamani kuufikia, lakini hawakuweza.

Tunajiuliza ni wakati gani waliwauliza hao wengine ambao hawakuweza nao wakawajibu kuwa walitamani kuufikia? Mwanadamu ana maneno mengi ya kujifariji na hasa anapoona maisha yake yanaleta shaka.

Mwaka 2018 umepita. Sasa tunaweza kuusoma kama tunavyosoma kitabu. Kitabu huwa kina kurasa nyingi. Ukurasa huu utakufundisha, lakini ukurasa mwingine utakuchekesha tu wakati ukurasa mwingine ukiusoma unakuhuzunisha na wakati mwingine kukufanya ujutie kwa uliyoyafanya kiasi kwamba ukatamani mwaka ungeanza upya ili uyaepuke usiyafanye.

Kuna mambo makubwa mengi tumeyafanya mwaka 2018 yatupasa tuyafurahie kwa sababu kwayo tutatuzwa. Kama yapo machahe maovu tuliyafanya basi hayo tuyajutie. Mwanadamu kaumbwa na nyongo na kwa sababu hiyo maovu machache yanauchoma moyo wake zaidi kuliko mema mengi yanavyomfurahisha.

Kuyachambua yote tuliyoyafanya huko nyuma kunahitaji muda, lakini yako machache ya hivi karibuni ambayo labda yanahitaji mtazamo mpya zaidi.

Nayakumbuka vema maneno ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi. Alisema kama watu wawili wanataka kumposa binti mmoja, lakini kati yao mmoja wao tayari ana mke inaweza ikawa faida kwa yule asiye na mke. Maisha anayoishi na mkewe yule mwenye mke yanakuwa yanajulikana. Kama ana tabia ya kumpiga mkewe hiyo itawekwa hadharani na hivyo kumpatia nafasi zaidi yule asiye na mke.

Nchi yetu mwaka huu inaelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Na mwakani – 2020 tutakuwa na uchaguzi mkuu. Siku zinapita haraka sana na hasa kama unafaidi. Ni juzi tu tulikuwa na uchaguzi mkuu. Ni vema basi tunapokuwa madarakani tukakumbuka kuwa iko siku tutatoka. Kumbukumbu hiyo itatusaidia kutenda haki. Walioko madarakani kwa maneno ya Mzee Mwinyi watakuwa wanaenda kuposa huku tayari wakiwa wameoa. Mema yao na maovu yao kama yapo yatawekwa hadharani. Hivyo ni busara sasa kuanza kujitathmini.

Yapo mambo ambayo labda yanahitaji kuwekwa sawa kabla ya kuingia ulingoni kwa sababu wananchi watakuwa na haki ya kutuhoji.

Mwanamwema Bashiru Ally alisema, “Kama tumejenga shule za kutosha zinazoonekana na kama tumejenga zahanati za kutosha zenye dawa zinazoonekana tuna wasiwasi gani!’’ Tunazindua daraja la Salenda au Tanzanite huku tukiwa na malaki ya wanafunzi ambao wameshindwa kuendelea na masomo sababu hakuna vyumba vya madarasa wala madawati. Mwanamwema Bashiru ni maskini gani hajui kuwa hakuna dawa katika hospitali za serikali?

Baba ukionyesha mapenzi uliyonayo kwa wakulima wa korosho walioko Mtwara na Lindi uliamua serikali inunue korosho zote. Nchi ikatangaziwa kuwa fedha kwa mabilioni ya shilingi tayari zimepelekwa huko. Hata wasiolima korosho walikushangilia. Wanajeshi wakaonekana wakipakia na kupakua marobota ya korosho, lakini hawalipi. Baba imezalishwa chuki kubwa Kusini dhidi ya serikali. Serikali ni Rais.

Kudhani kuwa ni kazi ya wapinzani ni upungufu wa fikra kwa sababu wao siyo walipaji.

Waliokutwa na korosho walitakiwa wakaonyeshe kama wana mashamba.

Walioshindwa kuonyesha mashamba korosho zao zilichukuliwa. Baba waambie watu hao korosho hizo zilipelekwa wapi? Lakini baba kwani wote wanaouza samaki ni lazima wawe wavuvi? Au je, waliwakuta wakulima wa korosho wakilalamika kuwa wameibiwa korosho zao hivyo wakaamua kuwasaidia kuwasaka wezi wao? Wenye fedha kugharimia zao la korosho tangu kupalilia, kupuliziwa dawa na huduma nyingine kwa makubaliano na wenye mashamba kuwa watawalipa korosho hapo zitakapokuwa tayari si utaratibu mpya. Ni utaratibu walionao tangu zamani. Hata pale mkulima alipokosa fedha za matibabu alimwendea mwenye fedha na kukopa fedha kwa makubaliano kuwa atamlipa korosho zitakapokuwa tayari. Sasa wenye fedha wamelizwa na kufanywa maskini huku mkulima akiwa hajapata chochote. Tusione aibu kulitazama hili upya kwa sababu lengo lilikuwa jema na nia ilikuwa nzuri kuwasaidia wakulima, lakini tumezusha balaa kubwa.

Kuyapita mapito haya yatupasa tubadilike kifikra kwa sababu huko tunakokwenda fikra mufilisi hazitapewa nafasi. Tulipoanzisha vita ya makanikia kwa nguvu kubwa Watanzania wema wengi tuliwajaza matumaini makubwa. Katokea mtetezi wa raslimali za Taifa. Ni nani leo anajua tulipofikia? Yametumika mabilioni ya fedha za walipa kodi kujenga bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam kwa maelezo kwamba utatengenezwa umeme mwingi wa kuijaza nchi na wa kuuzwa nje ya nchi. Tulitarajia vituo vyote vya mafuta leo vingekuwa vinauza gesi kwa matumizi ya magari na mitambo na matrilioni yanayotumika kuagiza mafuta yangetumika kwa maendeleo ya jamii. Tunaongea juu ya ujenzi wa zahanati nyingi, lakini upatikanaji

wa dawa hauzungumzwi zaidi. Tunapowaambia tumetenga fedha nyingi kwa afya tuwaangalie usoni tujue wanatufananisha na mnyama gani. Atatushangilia nani bila kukodi washangiliaji feki?

Wakanijia maskini wale wakaniambia, “Mwalimu Mkuu, tunarudi kwetu Mwanza mgonjwa wetu amefariki. Kuchukua maiti Muhimbili wanatutaka tulipe milioni 12 tutazipata wapi. Tumeamua tuwaachie maiti wamzike wao.’’

Tumeisusa gesi haitupi sifa na sasa wanakamuliwa mpaka maiti ili tufanye mambo makubwa kwa fedha zetu za ndani. Nakumbuka wakati wa kampeni Edward alisema, “Tunao utajiri mkubwa sana wa rasilimali gesi. Tutakwenda nao huko nje kwenye vyombo vya fedha tukaiweke rehani ili tupate fedha nyingi zitakazotuwezesha kununua ndege zetu na kupanua viwanja vya ndege. Zitakazotuwezesha kununua meli zetu na kupanua bandari zetu pamoja na kujenga barabara zetu na reli imara. Fedha zitakazotuwezesha kujaza dawa na vifaa tiba katika hospitali zetu na kuboresha elimu ya watoto wetu.’’ Maneno ya matumaini.

Baba ,ulitumia busara kubwa kuzifuta kanuni-sumu zilizoifedhehesha nchi zilizoandikwa na waziri mwenye dhamana ya mifuko ya jamii. Kumtumbua wa chini na kumuacha waziri aliyezitunga kanuni-sumu hizo kumeiondoa busara yote. Naye sasa anafanana na mtu aliyevaa magunia. Busara itakapochukua nafasi yake atawajibika au atawajibishwa. Uwezo wake bungeni hauwezi kumfanya timamu aelewe, iweje jua la alfajiri lionekane kuwa na rangi ya dhahabu wakati mchana ni jeupe na linapofikia machweo lionekane ni jekundu?

Please follow and like us:
Pin Share