Kushangilia wanaotuumiza ni kukosa uzalendo kwa nchi

Hadi tunakwenda mitamboni, ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ilikuwa ikishikiliwa nchini Afrika Kusini kutokana na amri ya mahakama.

Sababu za kukamatwa kwa ndege hiyo bado hazijawekwa bayana, japo kuna maelezo kuwa hatua hiyo imetokana na serikali yetu kudaiwa.

Hii si habari nzuri hasa kwa kipindi hiki ambacho Serikali ya Awamu ya Tano imenuia kwa vitendo kuifufua ATCL, hivyo kusaidia kukuza uchumi wa taifa letu.

Serikali ikiwa kwenye juhudi za kuhakikisha mgogoro huu unapatiwa ufumbuzi kwa njia za kiungwana, hali ni tofauti kabisa miongoni mwa Watanzania. Kwenye mitandao ya kijamii wapo wanaoshangilia kwa kitendo hiki kilichofanywa cha kuzuiwa ndege yetu.

Hata kama tuna tofauti miongoni mwetu zinazosababishwa, ama na mitazamo ya kisiasa, au vipaumbele, si jambo la busara hata kidogo kushangilia mapigo yanayoelekezwa kwetu kutoka kwa maadui wetu wa maendeleo.

Ndege za ATCL ni mali ya serikali. Mali ya serikali maana yake ni mali ya umma. Ndege hii na nyingine si za Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu au kiongoni awaye yeyote. Hii ni mali ya Watanzania wote bila kujali tofauti au misimamo yetu ya kisiasa.

Wanaoshangilia ndege au mali zetu kukamatwa, si tu kuwa wanakosa uzalendo, bali wanaushangaza ulimwengu kwa kuonyesha tabia isiyo ya kiungwana.

Tunaunga mkono Watanzania kuwa na mitazamo tofauti katika baadhi ya mambo, lakini kukinzana huko kunapaswa kuwa kwa masuala yetu ya ndani, na kwamba tunapokabiliana na tishio la kitaifa hatuna budi kuwa wamoja.

Pamoja na ukweli huo, tunaamini wakati umefika sasa kwa watendaji wa serikali kuwa tayari kufungua masikio na kuruhusu kupokea maoni kutoka kwa watu wenye mitazamo tofauti. Wapo waliojitokeza kuionya serikali juu ya hatari ya kukamatwa kwa mali, hasa ndege za ATCL, lakini pengine kwa ukaidi au kwa dharau tu, hadhari hizo zikapuuzwa. Haya tunayoyaona sasa ni matokeo ya kupuuzwa kwa mitazamo hiyo.

Kwa wakati huu hatuna budi kuyaweka kando hayo na kuungana pamoja kuhakikisha mikwamo ya aina hii tunaishinda. Kushangilia nchi inapoingia kwenye migogoro ya kiuchumi ni kukosa uzalendo. Tubadilike.