Home Maoni ya Mhariri Dhamira ya Mugabe iheshimiwe

Dhamira ya Mugabe iheshimiwe

by Jamhuri

Moja ya matukio ya kukumbukwa katika urais wa Robert Mugabe wa Zimbabwe ni lile la Julai mwaka 2017.

Katika tukio hilo, Zimbabwe iliyokuwa ikiongozwa na mzee Mugabe iliuza ng’ombe wa thamani ya dola za Marekani milioni moja kwenye mnada na kukabidhi fedha hizo kwa Wakfu wa Muungano wa Afrika kusaidia kumaliza utamaduni wa kutegemea fedha kutoka kwa wafadhili wa nje ya Afrika.

Kwa mujibu wa maelezo yake kwa wakati huo, binafsi alitoa ng’ombe 300 kutoka katika zizi lake, raia wengine wa Zimbabwe wakaongeza ng’ombe wengine kiasi sawa na hicho.

Mugabe alikabidhi hundi ya dola milioni moja kwa uongozi wa Umoja wa Afrika (AU) wakati wa mkutano mkuu wa viongozi wa mataifa wanachama nchini Ethiopia mwaka huo wa 2017.

Akizungumza katika mkutano huo, Mugabe alisema mchango huo ni mdogo tu, lakini ni ishara muhimu katika kujaribu kukomesha utegemezi wa Afrika kwa pesa za wafadhili.

“Kama Mwafrika na mkulima, kutoa ng’ombe ni jambo la kawaida kwangu, ikizingatiwa kwamba bara letu limebarikiwa kuwa na ng’ombe wengi na ng’ombe hutazamwa kama hazina ya utajiri,” alisema Mugabe wakati huo.

Wakati wa kipindi chake kama mwenyekiti wa AU kati ya mwaka 2015 na 2016, Mugabe alitetea AU iwe ikifadhiliwa na Waafrika. Kwa wakati huo hadi Mugabe anatoa mchango huo, asilimia 60 ya bajeti ya AU ilikuwa ikitegemea wafadhili kutoka nje ya Afrika.

Kwa upande wetu, Gazeti la Jamhuri tumekumbusha tukio hilo kwa sababu kadhaa. Licha ya kwamba ni tukio la aina yake kufanywa na rais, kupiga ng’ombe mnada na kuchangia Umoja wa Afrika, bado kuna dhamira kuu ya kuhakikisha Afrika inajitegemea kama iliyoonyeshwa na Mugabe.

Inawezekana Mugabe alikuwa na dhamira safi, lakini baadhi ya wenzake walikuwa na mtazamo tofauti, ama vipaumbele tofauti kwa mujibu wa mataifa waliyokuwa wakiyaongoza kwa wakati huo.

Tunawakumbusha nchi wanachama wa AU na hata Wana – SADC waliohitimisha mkutano wao mkuu wa 39 majuzi, tuendeleze kwa dhati nia ya mzee Mugabe. Siku zote tuzingatie kuwa penye nia pana njia.

You may also like