Kwa hili RC Chalamila amepatia

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, huwa hakosi vituko! Wengi wetu tulitarajia wiki iliyopita afungue mwaka mpya wa 2020 kwa kituko! Hakufanya hivyo!

Badala yake ameukaribisha mwaka kwa kutoa maelekezo mazuri yanayopaswa kuungwa mkono, si Mbeya pekee, bali nchini kote.

Amemwagiza Kamanda wa Polisi mkoani humo kuhakikisha mabango yote ya waganga wa kienyeji yanayopotosha umma yanang’olewa. Mabango yanayohamasisha wanafunzi kushinda mitihani bila kusoma (kuwaongeza akili), matangazo yanayohadaa umma kuwa mtu anaweza kuwa tajiri kwa kujiunga Freemasons, matangazo ya kwamba unaweza kusafisha nyota na kupendwa na kila mtu, matangazo ya kwamba unaweza kupata nguvu za kiume hata kama umezaliwa na kilema hicho; ni baadhi ya mambo ya kipuuzi kabisa yaliyofumbiwa macho na mamlaka za nchi.

Tunapokuwa tukitafakari au kusaka mchawi wa maendeleo yetu hatupaswi kuishia kuwalaumu wakoloni, mafisadi, viongozi au wahalifu wengine. Kuna vikwazo vingi vinavyochangia mkwamo wetu wa maendeleo hata kama tunavidharau kwa udogo wake machoni.

Unapoaminisha wanafunzi kuwa kuna dawa za kuwasaidia kufaulu mitihani, maana yake unakuwa unazalisha kizazi cha wajinga. Na haya yanakuwa hayaishii darasani au kwenye elimu tu, bali yanakwenda hadi kwenye michezo. 

Leo tuna genge la watu walioaminishwa na matapeli kwamba timu ya mpira inaweza kufaulu mashindano kwa dawa za ‘mtaalamu’ kutoka Sumbawanga, Tanga, Bagamoyo, Kigoma na kadhalika. 

Kwamba dunia ya leo bado tuna watu wanaoamini kuwa tunaweza kushinda Kombe la Dunia bila maandalizi ya kimwili na kiakili, ni jambo la bahati mbaya sana.

Miaka takriban 60 tangu tupate Uhuru bado tunalo kundi la watu wanaoaminishwa na wao wanaamini kwamba utajiri wa mtu unaweza kutokana na kiungo cha albino au sehemu ya siri ya mwanadamu! Dunia ya leo kuwa na mawazo ya kijima namna hii ni jambo la aibu na fedheha.

Tunaposikitika kwa kuambiwa au kushuhudia matukio ya watoto wadogo kunajisiwa, ajuza na vikongwe kuuawa; kina mama kunyofolewa sehemu za siri; hatuna budi kusaka na kukomesha vyanzo vya mambo haya. Naamini miongoni mwa vyanzo ni mabango haya ya waganga matapeli.

Mamlaka za nchi zina haki na wajibu wa kukomesha mabango haya yaliyoenea kila kona ya nchi yetu. Matapeli wanafanya vitendo vya utapeli ilhali mamlaka husika zikiwa zinawatazama bila kuchukua hatua. 

Haiingii akilini kuona kuwa viongozi kuanzia mitaa na vitongoji wanashindwa kukabiliana na genge hili hadi wasubiri kauli ya msukumo kutoka kwa mkuu wa mkoa au viongozi wakuu wa nchi.

Kama nilivyosema hapo awali, mkwamo wa maendeleo au ustaarabu katika jamii unasababishwa na mambo mtambuka, lakini mengine mengi yakiwa ndani ya jamii zetu wenyewe. Mwanafunzi anapoaminishwa kuwa kuna dawa ya kumsaidia kuongeza akili darasani, naye akaamini hivyo, hapo tutatajie majanga tu katika jamii na nchi. Akili inajengwa na aina ya mlo wenye virutubisho.

Mabango haya yameenea yakiwa na namba za simu za matapeli hao. Pengine mamlaka zinazopaswa kuyaondoa nazo zimeingiwa hofu kwa kuamini kuwa kwa kufanya hivyo nao ‘watashughulikiwa’. Jamii inayoamini kwenye ushirikina na mambo mepesi mepesi ya kipuuzi, haiwezi kujikwamua kwenye lindi la ujinga na umaskini.

Kama alivyoamua RC Chalamila, ni vema msimamo huu uwe wa viongozi wote katika ngazi zote. Hii iwe kazi ya wananchi wote wanaoitakia mema nchi yetu. Sioni ni kwanini wananchi wawe wepesi kushiriki uhujumu uchumi kwa kung’oa alama za barabarani, lakini wawe wagumu kuondoa mabango haya ya kitapeli huko mitaani wanakoishi.

Tujenge jamii inayoamini kuwa mafanikio katika maisha ni matokeo ya kazi halali. Tuaminishe watoto wetu kuwa matokeo mazuri darasani ni matunda ya kusoma kwa bidii. Tuwaaminishe wananchi kuwa hakuna utajiri unaodumu unaotokana na fedha za majini. 

Tufanye kila tunaloweza ili kuwafanya watu wa taifa letu wasiwe waumini wa viinimacho na njia za mkato za maisha kama vile uchezaji kamari.

Vijana wanaotamani mafanikio kwenye michezo tuwaaminishe kwa vitendo kuwa hao kina Messi, Ronaldo na wengine wa kiwango chao ni matokeo ya juhudi, nidhamu na vipaji. Waambiwe bayana kuwa hata wakiwa na makontena ya hirizi, kamwe hawatafanikiwa kwenye michezo.

Kwa dhati kabisa ninampongeza RC Chalamila kwa hatua yake ya kung’oa mabango yote yanayopotosha umma. Kwa kuwa matapeli hawa huweka namba zao za simu kwenye mabango yao, kazi ya kuwanasa ni nyepesi.