Jamii au familia makini ni ile inayoweza kwa akili za kibinadamu kutabiri na kuweka mipango kutokana na kinachotarajiwa.

Kwenye ngazi ya familia yapo yanayopaswa kufanywa na wazazi ili kukabiliana na makusudio au mipango yao ya kupanua familia.

Vivyo hivyo, serikali inao wajibu wa kuwatumia wataalamu wake kujua uamuzi fulani wa kisera au kisheria utatoa matokeo fulani. Kutambua athari – hasi au chanya za jambo lolote ni muhimu katika upangaji wa mipango ya maendeleo.

Idadi ya watoto wanaozaliwa nchini kila mwaka inajulikana. Idadi ya watoto wanaopaswa kuanza darasa la kwanza hujulikana hata kabla ya watoto wenyewe kufikisha umri wa kuanza masomo.

Lakini inapotokea wanafunzi wa darasa la kwanza, kwa mfano kwa mwaka huu wa 2020, wakajiandikisha kuanza masomo ya elimu ya msingi, ni wazi kuwa baada ya miaka saba watoto hao hata kwa idadi pungufu, watapaswa kuanza masomo ya kidato cha kwanza.

Vivyo hivyo, wale wanaoanza kidato cha kwanza tunatarajia kuwa baada ya miaka minne watapaswa kujiunga na masomo ya juu ya sekondari, vyuo na kadhalika.

Ni kwa mambo kama haya, ndiyo maana nchi inakuwa na wataalamu mbalimbali wenye uwezo kitaaluma wa kuliona jambo hata kabla ya lenyewe kujitokeza, kuliona likiwa tayari lipo na kushauri nini kifanywe ili kuendana na matokeo ya jambo hilo.

Wanafunzi wanaopaswa kuanza kidato cha kwanza mwaka huu hawakuibuka tu kutoka katika sayari au nchi nyingine. Kwa miaka saba iliyopita wataalamu wetu walitambua kila wilaya, mkoa hadi taifa kungekuwa na idadi gani ya watoto wanaopaswa kuanza masomo ya kidato cha kwanza mwaka 2020.

Ni jambo la kusikitisha kuona kuwa kwa miaka yote sote kama taifa tumekaa kimya bila maandalizi ya maana yenye kuwezesha kuwapokea watoto wetu wanaopaswa kuanza masomo ya kidato cha kwanza.

Tumeshituka na kuanza kuhaha huku na kule kuandaa mazingira ya kuwapokea watoto hawa kana kwamba hatukutarajia ufaulu wao.

Mara baada ya kutangazwa kwa matokeo ya darasa la saba ndipo sasa tunawasikia viongozi mbalimbali wakihaha na yakitolewa matamko ya ‘kuwatisha’ wale watakaozembea au watakaofeli kuwapeleka sekondari watoto waliochaguliwa.

Kote nchini kauli zinazosikika ni kama vile suala la kuwapokea watoto wa kuanza kidato cha kwanza ni jambo lililotokea kwa bahati mbaya. Tunataka kuonyesha kuwa jambo hili ni kama janga la asili ambalo huja bila kubisha hodi; na kwamba huwa hakuna namna nyepesi ya kuliepuka.

Wanafunzi wanaopaswa kuanza kidato cha kwanza si jambo la dharura kama ilivyo volcano; japo hata volcano nayo huanza kwa dalili fulani fulani.

Viongozi wa elimu, wanasiasa na wadau wote walitambua kwa miaka saba kuwa mwaka 2020 idadi ya watoto watakaopaswa kuanza kidato cha kwanza ni kubwa. Kimsingi maandalizi ya kidato cha kwanza hupaswa kuanza mwaka ule watoto wanaoanza darasa la kwanza kwa kuangalia idadi yao.

Ni jambo la aibu na fedheha kubwa kuona kwa miaka saba yote tunakaa kimya, badala yake tunashitushwa baada ya kusikia matokeo ya darasa la saba.

Licha ya kuwa jambo hili ni la fedheha, pia si haki kwa watoto ambao tayari walikwisha kuaminishwa kuwa elimu ya msingi kwa mtoto wa Tanzania ni kidato cha nne.

Ujenzi wa miundombinu ya madarasa, nyumba za walimu, maabara na vyoo uwe ni mpango wa kudumu kwa sababu hakuna dalili za kuwapo uwezekano wowote wa kupungua kwa idadi ya watoto wanaoanza darasa la kwanza, pia wale wanaojiunga kidato cha kwanza.

Kama idadi ya watu inaongezeka kila mwaka, na kama mpango wa serikali ni kuhakikisha watoto wote wa taifa hili wanapata elimu, basi hatuna budi kuwa na ujenzi wa miundombinu hiyo kwa kasi ile ile kila mwaka.

Si kila jambo lazima lisimamiwe na rais au viongozi wakuu wa nchi. Haya ni mambo yanayoweza kuanza katika ngazi za wilaya na mikoa kabla ya kuungwa mkono na ngazi ya taifa.

Kila wilaya na mkoa kuwe na mpango madhubuti wa kuhakikisha kila mwaka yanafanyika maandalizi kwa ajili ya mwaka ujao ili kuwawezesha watoto kuanza darasa la kwanza, pia kidato cha kwanza.

Utaratibu huu wa kufanya mambo kwa staili ya zimamoto, tena baada ya maagizo ya waziri mkuu haufai. Tuwe na mfumo wa kuyafanya mambo yetu yajiendeshe badala ya utaratibu wa sasa wa kusubiri kusukumwa na kauli za viongozi wakuu. 

Kila mmoja kwenye nafasi yake – kuanzia wilaya hadi taifa ajiulize anafanya nini kuhakikisha kuwa watoto wetu wanaanza darasa la kwanza, na wale wanaohitimu darasa la saba wanaanza masomo ya sekondari bila kucheleweshwa.

Hakika ni aibu kuona akili zetu zinazimuliwa na matokeo ya darasa la saba ndipo tutatumbue kuwa kuna mahitaji ya miuondombinu kwa wanafunzi wanaostahili kuanza kidato cha kwanza. Tuwe na utaratibu wa mambo ya mwakani kuanza kuyashughulikia walau mwaka mmoja kabla.

985 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!