Awali ya yote niwaombe radhi wapendwa wasomaji kwa kuwatupa mkono kwa kipindi kirefu sasa. Kwa siku za karibuni nimekuwa na dhima nyingi, kiasi cha kujikuta nikishindwa kutimiza yote niliyokusudia kwa wakati mmoja.

Itoshe tu kuwashukuru mno kwa kuendelea kwenu kuwa nasi kwa mwaka wa nane sasa bila kututupa. Desemba 6, 2011 inabaki kuwa siku muhimu kwetu kwa sababu tulichukua uamuzi mgumu na sahihi wa kuanzisha gazeti hili. Ushirikiano kutoka kwa wasomaji, watangazaji na wadau wengine wengi wenye mapenzi mema na JAMHURI tumeushuhudia kwa vitendo. Tunawashukuru sana.

Jana tulikuwa na kumbukizi ya miaka 58 ya Uhuru wa iliyokuwa Tanganyika. Ni siku muhimu. Waasisi wa taifa letu walipoamua kudai Uhuru kutoka kwa wakoloni, dhima kuu haikuwa kumwondoa mtu mweupe na kumweka mweusi tu, bali ilikuwa kuleta uhuru wa kweli kwa raia na wasio raia – alimradi ni binadamu – ili waweze kufaidi maana pana ya uhuru.

Uhuru ulitafutwa ili tuweze kujitawala wenyewe kwa misingi ya haki inayozingatia kanuni, sheria na katiba ya nchi yetu. Uhuru ulihangaikiwa ili kuwarejesha Watanzania na Waafrika katika misingi ya kuishi kwa furaha na kwa umoja. Haya tunayaona kwa uthibitisho kwenye falsafa ya Mwalimu Nyerere kama ile ya “Uhuru na Umoja”, na kadhalika.

Katika kipindi cha miaka 58 ya Uhuru, mengi yamefanikishwa. Viongozi wetu kwa nyakati zao wametumia nguvu na akili kuijenga nchi yetu. Wanaodhani hatujapiga hatua, warejee kusoma historia ya Tanzania kabla na baada ya Uhuru. Mambo mengi ya maana yamefanywa na yanaendelea kufanywa na Watanzania. Tunashuhudia sasa Rais John Magufuli anavyoipaishia nchi yetu kimaendeleo.

Mfumo wa siasa wa vyama vingi upo kikatiba. Mwaka 1992 tuliridhia kuwa na mfumo huu kwa sababu ambazo wengi tunazijua – kwamba ndiko ulikokuwa mwelekeo wa dunia.

Tumemsikia Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga akiagiza kung’olewa kwa bendera za chama cha siasa cha upinzani kuanzia vitongoji, mitaa hadi wilaya. Sababu za uamuzi huo hazikutangazwa, lakini ninaamini mwenye akili hawezi kukubaliana nazo hata kama angezipamba kwa mapambo gani.

Kuna wakati mtu unaweza kujiuliza, wakuu wa wilaya wenye ubongo wa aina hii wametoka sayari gani? Wanalenga kuvuna nini?

Vyama vya siasa vimeanzishwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vipo kikatiba. Si suala la utashi wa mtu au kiongozi. Hili ni takwa la kikatiba la watu kuwa na uhuru wa kujiunga katika chama au vyama vya siasa wanavyovipenda wenyewe bila shuruti.

Mkuu wa wilaya kabla ya kushika madaraka huapa kulinda sheria za nchi zilizotokana na haki za kiraia zilizoainishwa katika katiba. Anapotokea mkuu wa wilaya akawa kipofu wa sheria na katiba ya nchi, lazima tuwe na shaka na uzalendo au uadilifu wake. Kuamuru bendera za chama cha siasa zishushwe ni uvunjifu wa sheria, na kamwe mkuu wa wilaya hakupewa mamlaka ya kufanya uhalifu huo.

Mkuu wa wilaya ni kiongozi mkubwa kwa maana ya kuwa mwakilishi wa rais katika eneo husika. Inapotokea mwakilishi wa rais akawa ndiye chanzo cha uchochezi na uvunjifu wa amani, hapo tunapaswa kujiuliza, ni kitu gani anakitafuta? 

Tumeichoka amani kiasi cha kuanza kuchakua akili, mioyo na hisia za wananchi ili wakasirike na kuingia mitaani kufanya vurugu?

Kauli za aina hii za uonevu zinatolewa zikilenga nini? Je, mkuu wa wilaya anaona hii ndiyo njia ya kumfurahisha aliyemteua? Hivi kweli tumefikia kilele cha kuaminishwa kuwa kielelezo cha utendaji kazi cha mkuu wa wilaya, mkuu wa mkoa, DED au DAS ni kuua vyama vya upinzani? Hata kama ni kujipendekeza, ndiyo kufikie hatua ya kuanza kuleta hisia za vurugu katika nchi yetu tukufu?

Ndugu zangu, mataifa mengi ya Afrika yalikuwa na utulivu pengine kuliko hata Tanzania. Mathalani, Senegal ilikuwa na sifa zote za umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa watu wake kama ilivyo Tanzania. Lakini kilichotokea miaka kadhaa iliyopita nchini humo wengi tunajua.

Amani ni tunda la haki. Watu wanapotendewa haki watakuwa na amani. Huwezi kuvuruga kwa ubabe haki za watu wa kujiunga na vyama wanavyotaka halafu utarajie binadamu hao waendelee kuwa wapole.

Wala sidhani kwa amri za kiimla kama hizi zinamsaidia rais wetu katika kuongoza nchi. Sana sana wale wananchi wanaobanwa wataamini kinachofanywa na mkuu wa wilaya katumwa na rais, ilhali ukweli ni tofauti kabisa. Viongozi wasiumbe matatizo ambayo baadaye gharama zake zinabebwa na rais wetu.

Kuna mbinu nyingi za kuukabili upinzani na wapinzani, lakini si kwa kutoa amri za ajabu ajabu kama hizi za kushusha bendera. Haya mambo si lazima yalalamikiwe na wapinzani tu, bali Mwana CCM wa kweli anayelipenda taifa hili atasimama na kusema mkuu wa wilaya unachofanya ni cha hatari, hakifai, kiache.

Uhuru uliotafutwa na waasisi wetu ni uhuru wa kumfanya kila mmoja wetu katika nchi yetu awe huru kuishi kwa raha alimradi tu asivunje sheria. Kutundika bendera za upinzani kunavunja sheria gani? Kama ni uchochezi, ninaomba niwachochee Wana Sumbawanga wagome kushusha hizo bendera, maana ni haki yao. Mkuu wa wilaya atapita, lakini Sumbawanga na Tanzania zitabaki daima.

Mkuu wa wilaya anapoamua kwa ridhaa yake kujipendekeza, basi ajipendekeze kwa kiasi kwa kuamini kuna leo na kesho.

By Jamhuri