Tarehe ya leo miaka minne iliyopita, Dk. John Magufuli, aliapishwa kuwa Rais wa tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kuapishwa kwake kulimpa muda wa kuandaa dira yenye kuonyesha mwelekeo wa aina ya serikali anayokusudia kuiunda kwa ajili ya kutekeleza yale aliyowaahidi Watanzania kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020.

Hatimaye siku iliwadia, na akiwa sehemu ya Bunge, akahutubia taifa kupitia mhimili huo. Kilichofuata baadaye ni kuona akitekeleza mengi aliyoahidi kwenye hotuba yake ya uzinduzi. Wale waliozoea kupokea hotuba na kuziweka kando, wakasikika baadaye wakishangaa kuona mambo mengi yanayohitaji ujasiri na moyo wa ushupavu yakitekelezwa. Wale wanaomjua Dk. Magufuli wala hawashangai kuona aliyoahidi ndiyo hayo hayo anayotekeleza.

Rais Magufuli ni binadamu, na katika ubinadamu huo amejitahidi kufanya kile anachoamini kina manufaa kwa nchi na wananchi. Sote tu mashuhuda. Mara zote amewahakikishia wananchi kuwa hali ya uchumi ni nzuri, na amewataka wananchi wasiwe na shaka hasa pale kunapoibuka kauli za kuashiria kuwa hali ya uchumi si nzuri.

Kwa hali tuliyokuwa nayo kabla na baada ya mwaka 2015 tunaweza kusema yapo mazuri mengi yaliyofanywa na serikali inayoongozwa na Rais Magufuli. Kuna dhana kuwa kusifu si miongoni mwa dhima za mwanahabari, lakini itoshe kusema kuwa maendeleo ya nchi ni vita inayopaswa kupiganwa na wananchi wote; kwa hiyo mwanahabari hawezi kuukana ukweli kwamba naye ni sehemu ya vita hiyo.

Mengi mazuri yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano yanasemwa na kuimbwa kila leo kwa hiyo yanajulikana.

Kwa mujibu wa Katiba, Rais Magufuli amebakiza mwaka mmoja ili atimize ngwe ya kwanza ya uongozi wake wa miaka mitano. Baada ya hapo, na kwa kuzingatia kazi alizozianza, anaweza kuomba na kuongezwa ngwe nyingine ya miaka mitano.

Kwa kipindi cha miaka minne, kama nilivyosema, yapo mengi, mazuri na makubwa mno yaliyotendwa na serikali kwa msukumo wa rais mwenyewe na baadhi ya wasaidizi wake makini.

Sambamba na hayo mazuri, kumeibuka ‘mashimo’ mengi yenye kina kirefu yanayohitaji nguvu na msukumo wa ziada kuyafukia.

Miongoni mwa maeneo ambayo bado yanaonekana kuwa ‘kichwa ngumu’ ni utendaji kazi usioridhisha wa baadhi ya watendaji, hasa katika ngazi za chini. Maendeleo ya nchi haiwezekani yakaonekana au yakawa na tija kama eneo kubwa la wananchi ambao ni wale wa hali ya chini, wakaendelea kutaabika kwa kero zinazoweza kuepushwa au kutatuliwa mara moja.

Tumeshuhudia kwenye ziara za rais na hata waziri mkuu, namna mamia ya wananchi wanavyojitokeza kueleza kero zao mbalimbali. Kero hizi zinawapata wananchi katika maeneo ambayo kuna wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, ma-DED, watendaji kwenye tarafa, watendaji wa kata na vijiji.

Haya yanatokea katika maeneo ambayo kuna wakuu wa polisi wa mikoa, wakuu wa polisi wa wilaya, maofisa usalama wa taifa, wakuu wa Magereza, Uhamiaji na kadhalika. Mtu unaweza kujiuliza, iweje mwananchi mnyonge ahangaikie haki yake kwa miaka mitano au 15 bila kuwapo kiongozi wa kumsaidia?

Je, malalamiko haya ya wananchi yatamalizwa kwa mwaka mmoja uliobaki? Je, yatamalizwa kwa miaka mingine mitano baada ya mwaka 2020? Sina taaluma ya utabiri, lakini ninadiriki kusema hakuna namna yoyote – kwa aina hii ya mfumo – tunaweza kuona muujiza wa kumalizika kwa kero hizi.

Huko nyuma nimepata kueleza kuwa shida kubwa kabisa kuliko zote inayokwamisha maendeleo yetu ni kukosekana kwa mifumo inayojiendesha.

Hili linathibitishwa na mengi. Kwa mfano, mara kadhaa Rais Magufuli anapozungumzia mambo makubwa yanayofanywa kwa kodi za wananchi, amekuwa akihoji: “Kwanini haya yafanyike sasa? Kwani huko nyuma kodi zilikuwa hazikusanywi?” Swali zuri sana.

Jibu la swali hili ni kuwa kinachofanya kazi nchini mwetu ni ‘mtu’ na si ‘mifumo’. Hii ina maana kuwa aina ya kiongozi ndiyo inayoamua aina au kiwango cha maendeleo ya jamii na nchi. Pamoja na uwezo binafsi, inapendeza zaidi nchi iwe na mifumo iliyo imara ambayo inamfanya mkuu wa wilaya au mkuu wa mkoa awajibike bila kusubiri kusukumwa na makamu wa rais au waziri mkuu.

Kero zinazowakabili wananchi hazitakoma hadi tutakapofumua mfumo wa sasa wa uongozi na kuwa na mfumo ambao mkuu wa mkoa anaweza kuwa na mamlaka, si tu ya kumweka mtu rumande, bali ya kumwajibisha mhusika kisheria. Kwa kukosa mfumo,  ndiyo maana sasa tunaona ma-RC na ma-DC nguvu kubwa waliyonayo ni kuamuru mtu awekwe rumande!

Rais Magufuli amefanya na anaendelea kufanya mambo makubwa na mazuri kwa nchi yetu. Mambo haya yatadumu endapo atafanya mabadiliko makubwa kwenye mifumo yetu ya uongozi na uendeshaji wa mambo mbalimbali. 

Tufike mahali mifumo ya kitaasisi iwe na nguvu kuliko mtu au watu fulani fulani. Tuwe na mifumo ambayo kiongozi akiondoka asiwepo mtu wa kuhofu, kwa maana wote tutakuwa tumeamini katika kutenda mambo yetu kwa taratibu za mifumo.

Jambo jingine ninaloshauri ni kuwa Rais Magufuli awe makini na sifa anazomwagiwa. Kuna sifa za kweli, lakini nyingine ni za kutaka kuonekana tu. Kazi iliyo mbele ni kubwa pengine kuliko hata ile aliyokwisha kuifanya katika miaka minne. Sifa zisituondoe kwenye mstari kwa kuamini tulichofanya kinatosha.

Kwa wakati huu, wale wanaomshauri nini cha kufanya katika maeneo yanayoonekana kuwa bado yako kwenye matatizo, ni wa muhimu na wa maana zaidi kuliko wale ambao kazi yao ni kusifu tu. Wasifu lakini wasisahau kushauri na kupendekeza nini kifanywe ili kuinogesha safari ya kuwa na Tanzania mpya.

Hongera Rais Magufuli. Kazi uliyoahidi kuifanya umeifanya, imeonekana lakini safari bado ni ndefu. Tuungane kuhakikisha tunakuwa na Tanzania yenye ustawi kimaendeleo.

By Jamhuri