Kila mara niwazapo hatima ya umoja na mshikamano wetu huwa ninapekua na kusoma kijitabu kidogo, lakini kilichoshiba maneno ya busara sana kinachoitwa ‘Tujisahihishe’. Kiliandikwa na Mwalimu Julius Nyerere, mwaka 1962. Ni bahati tu kuwa sina mamlaka ya kuamuru, vinginevyo ningeamuru kila Mtanzania mwenye kujua kusoma, akisome kijitabu hiki. Kwa kuwa sina mamlaka hayo, basi niendelee kuwashawishi Watanzania, hasa viongozi wa kada zote na vyama vyote – wakisome.

Sehemu ya kitabu hiki inasema hivi: “Makosa yetu mengine hutokana na woga; woga unaotuzuia kumlaumu mkubwa japo tunajua kuwa kakosa, au kumtetea mdogo anayelaumiwa na wakubwa japo tunajua kuwa hana makosa. Na msingi wa woga ni unafsi. Pengine huwa tunaogopa sisi wenyewe kulaumiwa au kupata hasara fulani. Pengine twaweza kuwa hatuna cheo chochote ambacho tunaogopa kupoteza; pengine huwa hatuna wala tamaa yoyote ya kupata cheo fulani. Lakini woga unaweza kutokana na tamaaa ya kila binadamu kupendwa na binadamu wenzake. Sisi wote tunayo tamaa hii, au sivyo tusingekuwa binadamu. Woga huu huweza ukamfanya mtu kuvumilia maovu, hasa kama maovu yale yanatendwa na walio wengi kwa walio wachache au yanatendwa na wakubwa kwa wadogo. Kwa kuogopa kuwaudhi wengi tunawaacha watende makosa bila kuwasahihisha, wasije wakatuchukia. Huu ni unafsi mbaya sana. Ni kweli kwamba demokrasia haiwezi kudumu ikiwa wachache hawatakubali matakwa ya wengi. Lakini matakwa ya wengi hujulikana katika majadiliano au mazungumzo ya wazi wazi.”

Nimeyarejea maneno haya baada ya kuona mazuio ya polisi ya mara kwa mara kuhusu mikutano ya vyama vya siasa, hata kama mikutano yenyewe ni ya ndani.

Bahati mbaya sana, watu wanaogopa kuyasema haya kwa sababu ya kujaa hofu ya kuitwa ‘wapinzani’. Huhitaji kuwa mpinzani au katika chama tawala kuona kinachofanywa na Jeshi la Polisi si kitu chema. Si chema kwa mustakabali wa nchi, si chema kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), si chema kwa serikali na kwa hakika si chema kwa rais na jemedari wetu, Rais John Magufuli.

Kuwabana watu kupita kiasi si jambo la kujivunia. Haiwezekani katika nchi inayojenga usawa, upande mmoja ukawa na fursa ya kufanya mikutano kadiri unavyojisikia, lakini upande mwingine ukawa yatima kwa kuzibwa midomo hata kusikostahili.

Amri hii ya polisi ingekuwa yenye maana zaidi kama ingekuwa inagusa pande zote mbili, yaani upande wa upinzani na upande wa chama tawala. Kinachoonekana sasa ni upande mmoja kuminywa kupita kiasi.

Rais Magufuli alipoingia madarakani alitoa mwongozo wa namna siasa inavyopaswa kuendeshwa katika kipindi chake cha uongozi. Alipinga utitiri wa mikutano na maandamano. Akataka serikali anayoongoza iachiwe muda wa kushughulikia maendeleo badala ya kuhangaika na mikutano mwanzo hadi mwisho wa mwaka.

Akaenda mbali zaidi kwa kuagiza kuwa kama mwanasiasa anataka kufanya mikutano, basi kila mmoja afanye katika eneo lake – mbunge awe jimboni mwake, na diwani awe katika kata yake. Huu ulikuwa uamuzi wa busara.

Tofauti na msimamo huo wa rais, kinachoendelea sasa sicho kabisa. Wabunge wanazuiwa kufanya mikutano majimboni mwao. Madiwani wanazuiwa kufanya mikutano kwenye kata zao.

Kwa unafsi na kwa kujipendekeza, polisi na wanaochochea kuwapo kwa mazuio haya wanaweza kujidanganya kuwa wanamsaidia rais na serikali! Ukweli ni kuwa hawamsaidii. Watanzania wana uwezo wa kiakili wa kuona kuwa upande mmoja umechaguliwa mteremko, ilhali upande mwingine umeelekezwa kwenye mlima. Nchi yenye matabaka na ubaguzi wa aina hii haiwezi kuwa ya watu wamoja.

Hapo juu tumesoma haya kutoka kwa Mwalimu: “Lakini matakwa ya wengi hujulikana katika majadiliano au mazungumzo ya wazi wazi”. Naam! Matakwa ya wengi, si lazima yawe yale yanayotoka ndani ya chama cha siasa tu. Matakwa tunayojadili hapa ni yale yanayotoka kwenye kundi linaloipinga CCM hata kama ni dogo.

Kwa kuwa na majadiliano au mazungumzo ya wazi wazi [mikutano], CCM, serikali na vyombo vyake watawajua wananchi wengine wenye mawazo tofauti na CCM wanawaza au wanasema nini.   

Tunapoelekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa haina budi kuweka uwiano mzuri ili vyama vya siasa vishiriki kwa usawa ushindani wa kisiasa.

Kuendelea kuviminya na kuiacha CCM itambe, si jambo la haki. Kunajenga chuki. Hasira za binadamu zinazofichika ndani si nzuri. Leo polisi na Ofisi ya Msajili wanaweza kujidanganya kuwa wanamfurahisha Rais Magufuli kwa kuwabana ‘wapinzani’, lakini ukweli ukawa kwamba wanamuumiza.

Kama nilivyogusia, ninayasema haya kwa sababu ninaipenda CCM na ninaipenda Tanzania. Anayeshinda mtihani kwa haki mara zote huwa na furaha inayotoka moyoni, lakini anayeupata ushindi kwa hila, furaha yake huwa ya usoni tu.

Mwalimu anasema kwenye kijitabu chake: “Makosa ni makosa na dhuluma ni dhuluma, japo watendao makosa hayo au dhuluma ile ni wakubwa au ni wengi.”

Mwana CCM wa kweli hawezi kufurahia haya makatazo ya kutunga ya polisi yanayopambwa kwa kigezo cha ‘taarifa za intelijensia’. Maneno haya ni magumu kuyasema, lakini hayana budi yasemwe kwa sababu tunampenda Rais Magufuli, na tunaipenda Tanzania.

294 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!