Hayati-Baba-wa-Taifa-Julias-K.-NyerereIlipoishia wiki iliyopita: Nchi za Dunia ya Kwanza (Ulaya) kama zinavyoitwa kimaendeleo, zimepitia machungu mengi tena kwa karne kadhaa ndipo zikafikiria aina ya demokrasia wanayojivunia siku hizi. Wamepitia ile hatua kihistoria tunayoiita “RENAISSANCE” kule Ulaya, wakaanza kuamka lakini waliuana kweli. Ukaja wakati tunaita wa mageuzi ya viwanda “INDUSTRIAL REVOLUTION” ndiyo wakati ubeberu na ukoloni ulipoanza kule Ulaya. Na wakati huo ndipo walipoanza kutafuta mahali pa kupata malighafi kwa uendeshaji wa viwanda. Endelea…

 

Lakini kama demokrasia ile iiiyobuniwa na Plato kule Ugiriki kabla hata Bwana wetu Yesu Kristo hajazaliwa ingalifuatwa duniani pangetawaliwa na mfumo wenye amani na haki. Demokrasia namna hiyo haipo. Mwalimu wangu mmoja pale St. Mary’s School Tabora (Mwingereza kutoka Liverpool) akituambia “boys there is no justice under the sun” “vijana hakuna haki duniani” akisema haki ya kweli inapatikana kwa Mungu tu huko mbinguni. Sasa mimi naelekea kuelewa na kukubaliana na yale aliyokuwa akituambia. Cha msingi alikuwa akifundisha watoto wa Kiafrika tujaribu sana kuridhika na tusifikiri kuwa hawa Wazungu ndiyo wenye raha, hamna!

Wakati tunamaliza elimu ya sekondari Novemba 1951 kabla ya kufanya mtihani wa Cambridge, alitufanyia kama hafla ya kuagana hivi. Ninakumbuka mpaka leo maneno yake haya, “Happyness, boys is the tranquility of mind” yaani nikitafsiri alimaanisha kuwa “Furaha ni ridhaa ya moyo” yaani kamwe haitokani na kuwa na vitu vingi wala madaraka makubwa, bali ni hali ile ya mtu kuridhika na ulicho nacho.

Hivyo, wanadamu wanaweza kuwakosoa wenzao pale wanapoona mafanikio ya wale wenye juhudi ya kujiendeleza. Ukosoaji unaanza kwa kubeza mafanikio yale ya wengine. Pengine wanatoa kebehi ili tu kukatisha tamaa wale wanaojitahidi kujiletea maendeleo chanya katika shughuli zao.

Siku za karibuni niliangalia kipindi katika luninga Channel Ten kama saa 3 hivi za usiku. Kulikuwa kipindi cha mahojiano kilichoitwa kama sikosei au pengine sikumbuki sawa sawa ‘Mada Moto’. Katika kipindi kile siku ile (Ijumaa ya tarehe 8 Januari) mtangazaji alimuuliza swali Mbunge wa Singida Mashariki (Mwanasheria Mkuu wa Chadema), “Unaonaje utawala wa Rais Magufuli na mambo ya Bandari na TRA?” Mimi nilishtuka niliposikia maoni ya muulizwa. Mheshimiwa alijibu tu kwa mkato, “mimi namuona Magufuli kama ni Highbrid product kati ya Sokoine na Mrema”. 

Akaendelea kusema Sokoine alikuwa kiongozi aliyetawala bila kufuata sheria, alikamata watu, kutia ndani na kuwashtaki bila kuwa hata na sheria ya wahujumu uchumi. Sheria imetungwa na Warioba hapo baadaye eti ikaja kuwa na “retrospective effect”. Hayo ni makosa ya enzi za Sokoine. Ni utawala gani huo usiofuata sheria katika nchi? Pili enzi za Mrema, watu walitishwa kweli na Wizara ya Mambo ya Ndani na wafanyabiashara wengine wakimfuata mpaka kule Kibosho Uchagani. Huo ni utawala wa vitisho na mabavu – hauna sheria. Mwisho akasema, huko Bandarini au TRA au huo ukusanyaji wa kodi wa utawala wa Magufuli kama una tija kwa wananchi mbona mpako leo mishahara ya wabunge hatujalipwa? Akamalizia, ni mfumo mbovu tu wa utawala wa CCM. Watu wale wale wa Serikali ya Kikwete wamerejeshwa. Sioni tofouti yoyote.” 

Huu mimi binafsi naona ni upotoshwaji kabisa wa maoni. Kwa mtazamo wangu, majibu yale yalitolewa, kihamaki, hayakujibu swali la msingi bali yalikuwa ni maendelezo ya chuki kati ya Chadema na CCM tu. Siyo busara kiongozi kujibu maswali katika hali ya chuki au hamaki (provocative mood).

Huu mtindo wa ukosoaji wa upinzani kweli unalenga kuleta maendeleo katika Taifa letu? Ninaona, baadhi ya wawakilishi wetu katika Bunge wanakuwa na mawazo yao mgando (fixed attitudes) na kwao hali na wakati au mazingira havibadiliki ni vile kama walivyofikiria tnagu wanagombea ubunge. Sasa hali namna hii inaleta makosa bomozi (destructive criticisms) na kumbe upinzani kwa namna unavyoendeshwa nchi za Dunia ya Kwanza ni kutoa tofauti au mawazo mbadala (yaani constructive criticisms). Jambo hili Tanzania bado halijulikani au haliwiki au halifahamiki au basi niseme upinzani wakati wowote ule huwa wanatafuta upungufu tu na kamwe hawatathubutu kukubali uzuri wowote ule.

Waingereza wana kausemi kuwa “every cloud has its silver lining” kwa maana ya kuwa kila wingu, walau lina utepe wa fedha ndiyo kumaanisha kuna kajinafasi ka kunufaisha ulimwenguni. Mimi katika umri wangu nimeona mabunge karibu yote katika nchi hii tangu Uhuru 1961 mpaka leo hii 2016. Ni mabunge zaidi ya kumi na mbili hivi nayo ni hayo Bunge la (1960, 1965, 1970, 1975, 1980, 1985, 1990, 1995, 2000, 2005, 2010, na leo hii 2015). Na katika kila Bunge lile la chama kimoja au la vyama vingi, wametokea wabunge wasemaji hodari au wakosoaji hodari humo. Hili halijakosekana hata mara moja.

Kwa kadiri ya kumbukumbu zangu za uzeeni, bado nayakumbuka majina ya baadhi ya wabunge waliochachafya Serikali kila wakati wa vikao vyao bungeni huko nyuma. Namkumbuka Mbunge wa Rombo akiitwa Leons Ngalai, huyu alikuwa ‘outspoken’ wakati wake miaka ile ya 1960-1970. Baada ya huyo akaja kujitokeza Mbunge wa Dodoma akiitwa Rev. Padri Supa naye alivuma enzi zake. Kukaja wakati wa Mbunge wa Lindi, Maalim Sinani Nabahani (mdai barabara ya Lami Dar-Lindi), kukaja Mbunge wa Sumbawanga, Mzee Mzindakaya (mlipua mabomu bungeni), kukaja Mbunge wa Chunya, Njellu Kissaka, Kiongozi wa G55, kukaja mkusanyaji nyaraka nyeti za Serikali na kuzianika, Rev. Fr. Slaa, kukaja vijana vingang’anizi wa mawazo yao tu akina Zitto Kabwe, John Mnyika na Tundu Lissu. Huo ni mtazamo wangu (my personal observations). Kwa nyakati au enzi zao bungeni walisikika sana. Ni wakosoaji wa Serikali wakati wao.

Baada ya kutoa litania hiyo ya mtazamo wangu wa wabunge machachari nabaki najiuliza hivi hakuna njia wasomi hawa wanaweza kuboresha mwelekeo wa maendeleo ya nchi hii, maelekezo chanya? Kukosoa ni njia halali ya kuonesha upungufu wa Serikali. Bosi hakuna namna kweli ya kutoa mawazo mbadala ili Taifa linufaike na mchango endelevu wa wawakilishi wetu wa bungeni? 

Wanasayansi husema “Surplus energy used properly is very productive. But if such energy is misused then calamity occurs” maana yake nguvu ya ziada zikitumika vema huzalisha, lakini nguvu hiyo hiyo ya ziada isipotumika ipasavyo inaleta majanga; lakini vijana wetu wenye nguvu wakifanya kazi ya uzalishaji basi hapo ni faida kwa Taifa. Kumbe wakitumia nguvu zao kuchapana makonde au kukaba watu au kupora hapo huwa ni balaa.

Kumezuka tabia ya kuzomea na kupiga kelele bungeni kupinga kile upinzani wasichokitaka. Kuna Bunge gani duniani upinzani wanapanga kutibua utulivu na amani? Wale wastaarabu wanachofanya ni kuweka mkakati wa kutulia bila kusema au kutikisika (passive resistance). Hawa wanatoa mipango mbadala ya ile ya Serikali na ndipo wanasema twendeni kwa wananchi tukawanadie sera zetu sote na wananchi watachagua zile wanazoona kwao ni nzuri, zinatekelezeka na zinakubalika.

 

>>INAENDELEA

1490 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!