Tunamshukuru Mungu kwa kuingia mwaka mpya wa 2016. Kwa kawaida mwaka mpya unapoanza watu wengi huwa na malengo ya mwaka maarufu kama new year’s resolution.

Wengine huwa na malengo ya kupunguza uzito, kupata kazi, kuanzisha familia, kufungua biashara, kuongeza elimu n.k.

Kwa watafutaji wa udhamini wa elimu ughaibuni, ninaamini kabisa lengo kuu la mwaka 2016 ni kupata udhamini kuweza kupata elimu waliyokuwa wanaitaka kutimiza ndoto zao. Swali la kujiuliza ni KWANINI UNAKOSA UDHAMINI UGHAIBUNI KILA UKIOMBA?

Tatizo la kwanza la watu wengi kushindwa kufanikiwa, iwe ni kwenye udhamini wa elimu au malengo mengine ni kutokuwa na tarehe ya kikomo ya utimizaji malengo; yaani deadline. Unapokuwa huna deadline maana yake ni kwamba utakuwa na malengo ya kuomba chuo, ukiomba ukakosa utaomba tena hujui ni lini utapata.

Kwakuwa unakuwa hauna deadline hutoweza kujua ni kiasi gani cha rasilimali uwekeze. Na kwa kutokuwa na deadline unajiongezea asilimia kubwa za kukosa. Je, mimi nilifanyaje wakati ninaomba udhamini kwenye suala la kuwa na deadline?

Wakati naomba udhamini wa kusoma shahada ya pili nilikuwa tayari nipo Marekani kwa udhamini wa Fulbright kufundisha Kiswahili chuo kikuu hapa. Hiyo ilikuwa ni kati ya Agosti 2008 hadi Mei 2009.

Nilijiwekea deadline kuwa ni lazima nipate udhamini wa shahada ya pili na kuanza shule yangu Agosti 2009. Kwa kuweka deadline maana yake ni kujiongezea nguvu na kujua ni rasilimali gani nahitaji kutimiza hili. Hivyo, sikuwa nafanya kazi ya kubahatisha. Nilichofanya ni kuomba vyuo 25 vinavyotoa udhamini. Namshukuru Mungu niliweza kupata vyuo vitatu kati ya hivyo vilivyonipa udhamini.

Endapo nisingekuwa na deadline ya lini nitimize lengo langu, ningeishia kuomba chuo kimoja au viwili na asilimia ya kukosa ingekuwa kubwa. Unapokuwa na deadline unapunguza asilimia za kukosa kwani kila hatua unakuwa makini kuhakikisha makosa hayafanyiki. Na hilo ndio nililofanya.

Waombaji kutokujua muda wa uombaji ni tatizo kubwa mno. Ifahamike si kila wakati ni muda wa uombaji vyuo na udhamini. Kuna kitu kinaitwa Application Timeline ni muhimu muombaji ufahamu kabla ya kuomba.

Vyuo vingi (siyo vyote) uombaji wa vyuo na udhamini huanza Agosti hadi Desemba kwa ajili ya kuanza shule Agosti mwaka unaofuata. Japo kuna vyuo vichache sana uombaji huendelea hadi Januari hadi Februari.

Hii maana yake ni nini? Kama unataka kupata udhamini uanze kusoma Agosti 2017 maana yake uombaji ni kati ya Agosti – Desemba 2016. Na ukiomba ukakosa maana yake unakuwa “umepoteza” miaka miwili, maana yake badala ya kuanza kusoma Agosti 2017 utaomba tena uanze kusoma Agosti 2018.

Hivyo, ni vyema kuandaa kila kitakiwacho mapema mno. Usisubirie zimamoto. Makala za zijazo nitaeleza baadhi ya maandalizi; ila hapa ni kujua tu makosa ni yapi kwa haraka haraka.

 

Kushindwa kutofautisha uombaji kati ya Marekani na Ulaya ni moja ya tatizo kwa waombaji. Taratibu za uombaji ni tofauti katika maeneo haya. Uombaji wa Norway au Ujerumani ni tofauti na uombaji wa Marekani au Canada. Hivyo usitumie njia uliyoomba nchi moja kuwa ni lazima iwe sawa sawa na nchi nyingine.

Hii inaonekana – mfano kwenye uombaji wa PhD. Wakati vyuo vingi vya Ulaya hufanya PhD kwa thesis yaani mwanafunzi huingii darasani, ni wewe na msimamizi wako kuanza kuandika na kufanya utafiti. Hii maana yake kwenye uombaji utaanza kuomba kwa kutafuta msimamizi, PhD supervisor. Wakati kwa upande wa Marekani PhD hufanywa kwa coursework and dissertation. Mwanafunzi huingia darasani kwa miaka miwili hivi kusoma kwanza kisha kuanza kufanya dissertation yake.

Hii kwenye uombaji ni tofauti na Ulaya. Huanzi kuomba msimamizi. Hii wewe unaomba chuo kama unavyoomba kwenye shahada ya kwanza au ya pili. Pia utofauti huu una maana kwenye vigezo vya uombaji, ulipaji fedha ya udahili (application fees) n.k.

Mfano wakati vyuo vya Marekani na Canada ni LAZIMA ulipe application fee kwa kila chuo uombacho, vyuo vingi zaidi ya asilimia 99 vya Ulaya hawana application fee. Sasa hili akilijua linasaidia kukufanya uweke nguvu zako wapi, ujipange vipi kibajeti n. k. Usipojipanga utaishia kusema una mikosi na huna bahati kumbe umeshindwa kujua sheria za mchezo.

Kosa jinguine ni waombaji kushindwa kutofautisha kipi kinaanza kati ya udahili na udhamini (admission and scholarship). Wengi wamekuwa wanajiombea vyuo, kisha wanapewa udahili baada ya hapo wanaanza kutembeza bakuli la kutaka mtu awape fedha kwenda kusoma ughaibuni. Nimekuwa napokea barua pepe nyingi kuhusu hili.

Wengi husema: “Makulilo mimi nimeomba vyuo vitatu Uingereza na nimepata vyote ila wanataka nilipe ada kiasi fulani na niwe na fedha ya kuanzia maisha kiasi fulani.”

Swali ninalowauliza kila wakati; je, wakati unaomba chuo hicho waliandika kuwa wanatoa udhamini kwenye kozi uliyoomba au ulijiombea tu? Hili ndio kosa kubwa, watu wanajiombea vyuo. Ukijiombea tu chuo kisa kina jina zuri au kozi nzuri bila kujua kama kozi au chuo hicho kinatoa udhamini kwa wanafunzi wa kimataifa, maana yake unakuwa unaomba chuo kama mwanafunzi anayeenda kujilipia -yaani Self-financing student.

Ukiwa mwanafunzi unayejipia utapewa udahili na kutakiwa ujilipie. Na kwa dunia ya sasa huwezi kupata udahili Uingereza utarajie Ujerumani ikulipie uende nchi nyingine eti Uingereza. Au upate udahili Ufaransa, utarajie Uingereza ikupe hela uende Ufaransa. Fahamu nchi za kibepari zinazidi kujipanua na kueneza ubabe wao, kila mmoja atavutia kwake.

Nini suluhisho sasa? Unapoomba chuo, lazima uombe vyuo ambavyo vinakuwa vimeandika kinagaubaga kuwa uombapo kozi fulani kwenye chuo chetu kuna ufadhili wa kiasi fulani. Kama hawajaandika kuwa wanatoa ufadhili katika kozi hiyo, usipoteze muda wako kuomba maana utapewa udahili kama self-financing student na utaishia kusaga meno.

Kwa kifupi lazima uombe vyuo ambavyo udahili na ufadhili vimeunganishwa pamoja, yaani admissions and scholarships are merged together, no separate applications. Hapo ni kwamba ukipewa udahili maana yake umepewa ufadhili, na ukikosa udahili maana yake umekosa ufadhili.

Kosa la mwisho na kubwa sana ni waombaji kutofahamu ushindani uliopo kwenye udhamini wa elimu ya juu. Wengi wanadhani waombaji ni peke yao! Ifahamike kuna maelfu ya watu wanaomba ufadhili wa elimu. Ni malengo ya watu wengi wa nchi zinazoendelea kupata elimu nzuri nchi zilizoendelea.

Waombaji wanatoka duniani kote- Afrika, Asia, Amerika ya Kusini n.k.

Hapa unakutana na kwanza waombaji wengi wenye sifa tofauti tofauti na wewe kutokana na mazingira yao (yaani si wote Watanzania wenye asili moja) n.k. Unakuta katika kozi moja waombaji mpo 250 na ufadhili kwenye kozi hiyo ni kwa watu 10 tu.

Ukijua ushindani unakutana nao unakusaidia kuboresha maombi yako, siyo kuzima moto unaamka usiku na kutuma mambo yako kwenye mtandao. Lazima uchukue miezi kuandaa maombi yako, kukusanya kila nyaraka itakiwayo kwenye maombi.

Pia kwa kujua ushindani unaokutana nao, ndiyo hapo lazima uombe vyuo vingi zaidi ya 15, la sivyo utakwenda kukosa na kupoteza miaka miwili kusubiri muda mwingine wa uombaji udhamini wa elimu.

Mwisho, napenda kuwaasa waombaji wote, uombaji wa udhamini wa elimu ya juu ughaibuni ni VITA. Na katika vita, lazima ujiandae vya kutosha. Si lele mama. Kwa msaada wangu na wengine, inatakiwa vita hii tuishinde.

2582 Total Views 3 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!