Mashindano ya soka ya Ligi ya Mkoa wa Mwanza msimu huu, yametajwa kuwa na msisimko mkubwa ikilinganishwa na msimu uliopita. Msisimko huo unadhihirishwa na ongezeko kubwa la mashabiki na wapenzi wa soka, wanaojitokeza kushuhudia na kushangilia mechi husika katika viwanja mbalimbali.

Katibu wa Chama cha Soka mkoani Mwanza (MZFA), Nasib Mabruki, ameeleza kuridhishwa kwake na hamasa ya mashindano hayo yanayozishirikisha timu 18 kutoka wilaya mbalimbali.

“Kitendo cha wapenzi na mashabiki wa soka kujitokeza kwa wingi kushuhudia mechi za ligi hii, kinaashiria kuwa watu wengi wana mwamko na hamasa kubwa katika soka,” amesema Mabruki katika mazungumzo na JAMHURI kwa njia ya simu, juzi.

 

Timu zinazoshiriki ligi hiyo na wilaya zinakotoka zikiwa katika mabano ni UDC FC, Nansio Utd na Lake Warriors (Ukerewe), Nyamagana Utd, Bocca Junior na River Side (Nyamagana), Masabuda FC, Mwanza Utd na Kisesa Utd (Magu).

Nyingine ni TSC Academy, Jonas FC, Channel AFR na Mbao FC (Ilemela), Misungwi Stars, Nange FC na Biashara FC (Misungwi), Sengerema Stars (Sengerema) na Black Mamba (Kwimba). Mabruki amesema ofisi yake inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuboresha soka mkoani Mwanza, ili kuuwezesha mkoa huo kuendelea kutoa wachezaji bora wa kitaifa na hata kimataifa.

 

Baadhi ya wachezaji bora wa kitaifa ambao chimbuko lao ni mkoani Mwanza, ni Mrisho Ngassa na Mwinyi Kazimoto wanaoichezea Simba; Kelvin Yondani na Oscar Joshua wanaoichezea Yanga.

 

Toto African ya Mwanza, Simba na Yanga za Dar es Salaam ni miongoni mwa timu 14 zinazoshiriki michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom ya Tanzania Bara msimu huu.

 

“Matarajio yetu ni kwamba ushirikiano wa wadau mbalimbali wa soka utauwezesha mkoa huu kuendelea kutoa wachezaji mahiri zaidi watakaong’ara katika mashindano ya kitaifa na kimataifa,” amesema Mabruki.

 

Shule ya Alliance Sports Academy ya jijini Mwanza ni miongoni mwa vituo vinavyoibua na kupika watoto na vijana wenye vipaji vya soka, ambao hatimaye watakuwa tegemeo katika mashindano ya soka ndani na nje ya nchi. Katibu huyo wa MZFA ametoa wito kwa wananchi kuendelea kujitokeza zaidi kusaidia soka kwa hali na mali, kwani mchezo huo ni ajira nzuri kwa vijana.

 

“Lakini pia nitumie nafasi hii kuishukuru Serikali ya Mkoa wa Mwanza kwa jinsi inavyoendelea kutuunga mkono katika jitihada za kuboresha soka mkoani,” amesema.

By Jamhuri