*Asema wanatumbua fedha, watengewa fungu la Ukimwi

Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wa Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu, wiki iliyopita aliwasilisha bungeni maoni ya Kambi hiyo, na kueleza namna Tume ya Mabadiliko ya Katiba inavyofuja fedha.

Ifuatayo ni sehemu ya hotuba hiyo.  Katika mwaka wa fedha wa 2012/2013, Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliidhinishiwa Sh bilioni 33.944 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 ya Sheria za Tanzania.

Kwa mujibu wa Maelezo ya Makadirio ya Matumizi Mengineyo kwa Mwaka wa Fedha 2013/2014 yaliyoletwa mbele ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala mwezi uliopita, hadi kufikia Februari 25, 2013 Tume ilishapokea Sh bilioni 18.473 kutoka Hazina na ilikwishatumia Sh bilioni 14.968, sawa na asilimia 81 ya fedha zilizopokewa.

 

Kwa mujibu wa maelezo hayo, Sh bilioni 3.504 ambazo hazijatumika zimetengwa kwa ajili ya kulipia madeni kutokana na huduma za uchapishaji wa Mwongozo wa Mabaraza ya Katiba, uratibu wa mchakato wa kupatikana wajumbe wa Mabaraza ya Katiba na gharama nyingine za uendeshaji wa ofisi.

 

Maelezo ya Tume yanaonesha kwamba Sh bilioni 15.471 ambazo hazijatolewa na Hazina, zitatumika kwa ajili ya kusambaza nakala milioni moja za Rasimu ya Katiba Mpya (Sh bilioni 3.848); elimu kwa umma juu ya Rasimu ya Katiba Mpya (Sh milioni 400); kuratibu na kuendesha Mabaraza ya Katiba kwa nchi nzima (Sh bilioni 4.734); na Sh bilioni 6.488 kwa ajili ya matumizi mengine pamoja na ‘stahili za Wajumbe na Sekretarieti.’

 

Katika maoni yetu ya mwaka jana, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ililalamikia kile ilichokiita “…matumizi yasiyoelezeka na yasiyokubalika ya fedha za umma hasa hasa katika mazingira ambayo wananchi wanahubiriwa na watawala kwamba miradi ya maendeleo yao ya kiuchumi na kijamii haitekelezeki kwa sababu ya ufinyu wa bajeti ya Serikali.”

 

Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilidai kwamba Sh bilioni 14.633 zilizotengwa kwa ajili ya kuwalipa wajumbe na watendaji wa Tume posho mbalimbali zilikuwa zinatishia kuigeuza.

 

“Heshima ya kutumikia waliyopewa wajumbe wa Tume kuwa hongo ya Serikali.” Madai ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuitaka Serikali ieleze Bunge hili tukufu gharama zote za kila mjumbe wa Tume, sekretarieti na watumishi wengine wote wa Tume “ili wabunge na wananchi wa Tanzania wafahamu kodi wanazolipa zinavyotumika katika mchakato wa Katiba Mpya” yalikataliwa na Serikali kwa hoja kwamba taarifa hizo ‘ni siri kati ya mwajiri na mwajiriwa.’

 

Mheshimiwa Spika, Bunge lako tukufu linaombwa kuidhinisha Sh bilioni 33.944, kiasi kile kile kilichoidhinishwa mwaka jana, kwa ajili ya matumizi ya Tume kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014. Kiasi hiki ni pamoja na Sh bilioni 12.193 kwa ajili ya “… kulipia posho za vikao kwa Wajumbe wa Tume 34 na Sekretarieti 160 …”;

 

Sh bilioni 1.728 ambazo “… zitalipia posho ya kujikimu kwa ajili ya Wajumbe na Sekretarieti wanaposafiri ndani ya nchi kikazi”; na Sh bilioni 1.65 kwa ajili ya “… kulipa gharama za nyumba za Wajumbe na Sekretarieti wanaotoka nje ya Dar es Salaam.”

 

Aidha, kuna Sh milioni 18 zinazoombwa kwa ajili ya kugharimia chakula kwa wajumbe wa Tume na Sekretarieti watakaokuwa wamepata maambukizi ya Ukimwi; Sh milioni 60 kwa ajili ya usafiri wa ndani; Sh milioni 50 kwa ajili ya gharama za malazi kwa Wajumbe wa Tume na Sekretarieti ‘wanaposafiri kikazi’; Sh milioni 423 kwa ajili ya ‘chai na vitafunwa’; na Sh milioni 50 kwa ajili ya wahudumu wanaosaidia kazi za Tume wakiwa mikoani wakati wa kushiriki kwenye Mabaraza ya Katiba na zoezi la upigaji kura ya maoni.

 

Vilevile, Mheshimiwa Spika, Bunge lako tukufu linaombwa kuidhinisha Sh milioni 60 ya kulipia maji kwa matumizi ya ofisi za Tume; Sh milioni 30 kwa ajili ya kulipia gharama za usafiri wa basi na taksi kwa wajumbe na Sekretarieti watakaposafiri ndani ya nchi kikazi; na Sh milioni 103 kwa ajili ya kulipia gharama za simu za mikononi.

 

Mheshimiwa Spika, Bunge lako tukufu linaombwa kuidhinisha posho na ulaji zaidi ya huu kwa ajili ya wajumbe na Sekretarieti ya Tume. Ulaji huu mwingine unajumuisha Sh milioni 604 kwa ajili ya posho kwa Wajumbe wa Tume na Sekretarieti wakati wa Bunge Maalumu la Katiba.

 

Maelezo ya Tume yamejaribu kuhalalisha matumizi ya fedha hizi za ziada kwa kuzibatiza jina la ‘hardship allowances’, yaani ‘posho ya mazingira magumu’, wakati vikao vya Bunge Maalumu la Katiba vitafanyika Dar es Salaam au hapa Dodoma!

 

Vile vile, katika ulaji huu mpya, zipo Sh milioni 266 zinazoombwa kwa ajili ya chakula na viburudisho wakati wa vikao vya Bunge Maalumu la Katiba; Sh milioni 12 nyingine kwa ajili ya huduma za chakula na viburudisho kwa shughuli zinazohusiana na Tume; na Sh milioni 185 kwa ajili ya kulipia usafiri wa basi na taksi.

 

Aidha, kuna Sh milioni 30 za utengenezaji wa fulana na kofia kwa Wajumbe wa Tume na Sekretarieti wakati wa kushiriki kwenye zoezi za uhamasishaji kuelekea upigaji wa kura ya maoni; Sh milioni 40 nyingine kwa ajili ya utengenezaji wa sare wakati wa maadhimisho mbalimbali ya kitaifa; na Sh milioni 12 kwa ajili ya posho za kujikimu kwa watumishi wa Tume watakaohudhuria kwenye maadhimisho mbalimbali ya kitaifa.

 

Zaidi ya hayo, kuna Sh bilioni 1.307 zinazoombwa kwa ajili ya posho za kujikimu kwa ajili ya Wajumbe na Sekretarieti ya Tume wanaposafiri ndani ya nchi wakati wa kushiriki kwenye shughuli ya upigaji wa kura ya maoni; na Sh milioni 218 kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya magari ya Tume wakati wa kushiriki shughuli ya uhamasishaji kuelekea upigaji wa kura ya maoni.”

 

Kwa ujumla, Mheshimiwa Spika, Bunge lako tukufu linaombwa kuidhinisha Sh bilioni 19.039 kwa ajili ya posho za aina mbali mbali na malipo mengine yanayowahusu Wajumbe na Sekretarieti ya Tume kwa mwaka wa fedha 2013/2014. Hii ni zaidi ya asilimia 56 ya bajeti yote inayoombwa kwa ajili ya Tume.

 

Kwa ulinganisho, posho na malipo mengine yanayowahusu Wajumbe na Sekretarieti ya Tume yalikuwa Sh bilioni 14.633 au asilimia 43 ya bajeti yote ya mwaka wa fedha uliopita. Hii ina maana kwamba gharama za moja kwa moja za Wajumbe na Sekretarieti ya Tume zitaongezeka kwa zaidi ya Sh bilioni 4.406 au zaidi ya asilimia 30 ya gharama za mwaka jana kama Bunge lako tukufu litaidhinisha maombi haya!

 

Maombi haya ya mabilioni ya fedha za wananchi yanatoa uvundo na harufu mbaya ya ufisadi, na hayaelezeki na wala kukubalika kwa misingi ya kisheria, na kwa rekodi ya utendaji kazi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

 

Kwanza kabisa, kwa mujibu wa kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Tume ina Wajumbe wasiozidi 30 pamoja na Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wake. Kwa maana hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua uhalali wa maombi ya Sh bilioni 12.193 kwa ajili ya posho za vikao kwa Wajumbe 34 wa Tume wanaotajwa katika kijifungu 210321 cha kasma 210300 kwenye randama ya Fungu 08 linalohusu Tume.

 

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua Wajumbe hawa wanne wa ziada ni akina nani na wameteuliwa lini kuwa Wajumbe wa Tume? Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kuelezwa, inakuwaje Tume iwe na Wajumbe 34 wakati Sheria iliyoiunda inataka Tume yenye Wajumbe wasiozidi 30?

 

Pili, kwa mujibu wa kazi za Tume kama zilivyoainishwa katika kifungu cha 9 cha Sheria; na kwa mujibu wa utaratibu wa utendaji kazi wa Tume kama ulivyofafanuliwa katika Sehemu ya Nne ya Sheria; na kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 22(1) cha Sheria hiyo, Wajumbe na Sekretarieti ya Tume siyo wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.

 

Badala yake, uhusiano pekee wa kisheria uliopo kati ya Tume na Bunge Maalumu ni ule uliotajwa katika vifungu vya 20(3), 20(4) na 25(2) vya Sheria vinavyomruhusu Mwenyekiti wa Tume kuwasilisha Rasimu ya Katiba Mpya kwenye Bunge Maalumu, na kuwaruhusu Mwenyekiti na wajumbe “… kutoa ufafanuzi utakaohitajika wakati wa majadiliano katika Bunge Maalumu.”

 

Hii ina maana kwamba mara baada ya kuwasilisha Rasimu ya Katiba Mpya, Mwenyekiti wa Tume anakuwa functus officio, yaani hana kazi nyingine yoyote ya kufanya kwenye Bunge Maalumu. Aidha, Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume hawana kazi nyingine yoyote ya kufanya katika Bunge Maalumu hadi hapo watakapohitajika na Bunge Maalumu kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa jambo lolote linalohusu Rasimu ya Katiba Mpya.

 

Wakishatoa ‘ufafanuzi utakaohitajika’ walioitiwa, nao pia wanakuwa functus officio. Kwa sababu hizo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua uhalali wa Sh bilioni 1.055 ambazo Bunge lako tukufu linaombwa kuziidhinisha kwa ajili ya posho, chakula na viburudisho na usafiri wa basi na taksi kwa Wajumbe wa Tume na Sekretarieti wakati wa vikao vya Bunge Maalumu la Katiba.

 

Tatu, kwa mujibu wa kifungu cha 33(2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, jukumu pekee la Tume katika hatua ya uhalalishaji wa Katiba Mpya ni kutoa elimu ya uraia na uhamasishaji juu ya Katiba inayopendekezwa kwa muda usiozidi siku 30 kuanzia siku ya kuchapishwa katika Gazeti la Serikali.

 

Kwa kazi ya mwezi mmoja tu Wajumbe na Sekretarieti ya Tume wanaombewa Sh bilioni 1.307 kwa ajili ya posho za kujikimu. Kwa mahesabu hayo, kila Mjumbe wa Tume, Katibu na Naibu Katibu pamoja na wakuu wa vitengo saba vya Tume na madereva wa kila mmoja wao watalipwa wastani wa Sh milioni 16.756 kwa mwezi huo mmoja, au Sh 558,547 kama posho ya kujikimu kwa kila siku moja!

 

Katika nchi ambayo wauguzi katika hospitali za umma wanalipwa mshahara wa kuanzia wa takriban Sh 360,000 kwa mwezi; na walimu wa shule za msingi wanaanzia Sh 250,000 na wale wa sekondari Sh 325,000 kwa mwezi, malipo haya kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba yana uvundo na harufu mbaya ya rushwa kwa Wajumbe wa Tume!

 

Hivyo basi, kwa vile kifungu cha 14(2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kinatamka kwamba Wajumbe wa Tume na Sekretarieti watalipwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za nchi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM iliambie Bunge lako tukufu ni sheria na kanuni zipi za nchi yetu ambazo zimetumika kuhalalisha malipo haya makubwa kwa Wajumbe na Sekretarieti ya Tume.

 

Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM itoe kauli rasmi mbele ya Bunge lako tukufu kama kuna uhalali wowote wa kutumia fedha za wananchi wa Tanzania ili kununua ‘chakula maalumu’ (special foods) kwa ajili ya Wajumbe na Sekretarieti ya Tume watakaopata Ukimwi kwa sababu ya kuendekeza ngono zembe na starehe zao binafsi wakati wanatakiwa wafanye kazi ya Tume!

 

Vinginevyo, Bunge lako tukufu lielezwe kwa ufasaha ni kwa namna gani mchakato huu wa Katiba Mpya unatazamiwa kusababisha maambukizo ya Ukimwi kwa Wajumbe na Sekretarieti ya Tume!

 

Kwa Serikali kujificha nyuma ya pazia la ‘siri ya mwajiri na mwajiriwa’ hakutoshi tena, kwani ni kulizuia Bunge lako tukufu kutekeleza wajibu wake kikatiba wa kuisimamia Serikali chini ya ibara ya 63(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sura ya 2 ya Sheria za Tanzania.

 

Aidha, ni haki kwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kujua uhalali wa malipo haya kwani, kwa mujibu wa ibara ya 63(3)(a) ya Katiba, Bunge lako tukufu “laweza kumuuliza Waziri yeyote swali lolote kuhusu mambo ya umma katika Jamhuri ya Muungano ambayo yako katika wajibu wake….”

 

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua Sh milioni 218 kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya magari ya Tume zitatumikaje ndani ya kipindi cha siku 30 za uhamasishaji na kuelimisha wananchi kupiga kura ya maoni kwa Katiba Mpya.

 

Hii ina maana kwamba hata kama kila Mjumbe wa Tume, Katibu, Naibu Katibu na wakuu wa vitengo saba vya Tume watapewa gari moja kwa kila mmoja wao kwa kipindi hicho, kila gari itatumia wastani wa Sh 186,325 kwa siku kwa ajili ya mafuta tu!

 

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua ni safari zipi hizo za Tume ambazo zitalazimu matumizi ya full tank ya mafuta kila siku kwa mwezi mzima? Huu, kama Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alivyowahi kusema, ni ‘wizi mtupu’!

 

Amlipaye mpiga zumari ndiye achaguaye wimbo. Baada ya Tume kulipwa mabilioni yote tuliyoyapigia kelele kwenye maoni yetu ya mwaka jana, kuna ushahidi kwamba Tume imekuwa inacheza wimbo uliochaguliwa na CCM na Serikali yake.

 

Februari ya mwaka huu, Tume ilichapisha Mwongozo kuhusu Muundo, Utaratibu wa Kuwapata Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya (Mamlaka za Serikali za Mitaa) na Uendeshaji Wake. Mwongozo huo ulisainiwa na Mwenyekiti wa Tume, Jaji Joseph Sinde Warioba, na ulianza kutumika Machi Mosi, 2013.

 

Ingawa Tume imedai kwamba Mwongozo huo ulitolewa kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba Mwongozo ulitolewa kinyume na matakwa ya Sheria hiyo na kwa lengo la kuinufaisha CCM na washirika wake.

 

Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba, Mathias Chikawe alijibu hoja hizi kwa kifupi akidai Jaji Joseph Warioba na Dk. Salim Ahmed Salim wanaoongoza Tume hiyo, ni watu makini wasioweza kujiingiza katika ufisadi kama alivyodai Lissu.

 

1396 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!