Mwaka 2004 tukiwa katika ziara ya Waziri wa Maji na Mifugo, Edward Lowassa, tulizuru kwa mara ya kwanza Kijiji cha Lupaso kilichopo Masasi mkoani Mtwara.

Lupaso ndipo alipozaliwa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa. Umaarufu wa Lupaso hautofautiani sana na vijiji kama Butiama, Msoga na hivi karibuni kabisa – Chato.

Miaka 17 baadaye, yaani Septemba 24, mwaka huu, nilifika Masasi. Nikaingiwa shauku ya kufika Lupaso, hasa nikitambua kwamba mwaka jana sikushiriki mazishi ya Mzee Mkapa. Kutoka Masasi hadi Lupaso ni umbali wa kilometa 33 hivi. Bahati nzuri kipande hicho cha barabara kimewekwa lami.

Kwenye safari hii nilikuwa mimi, mkurugenzi mwenzangu na mmoja wa watoto wangu. Tulipowasili kijijini Lupaso tulipokewa na wanakijiji tuliowakuta wakibangua korosho. Miti yao ya kivuli ni mikorosho. Walituelekeza namna ya kuingia eneo husika ambalo ni umbali wa mita 50 hivi kutoka tulipokuwa.

Tulikwenda moja kwa moja hadi katika nyumba ya wazazi wa Mzee Mkapa iliyojengwa kwa udongo na kuezekwa kwa mabati ya zamani, ambayo ni imara kweli kweli. 

Kutoka hapo tukaonyeshwa kwenye nyumba wanamoishi wahudumu wa makazi ya Mzee Mkapa. Kwa mandhari ni nzuri mno.

Pembeni mwa nyumba hii kuna tangi refu lililojengwa kwa maelekezo ya Lowassa ili Mzee Mkapa apate maji. Lakini tulidokezwa na mwanakijiji mmoja kuwa maji kuingia na kutoka kwenye tangi hilo ni miaka zaidi ya 16 iliyopita.

Kutoka kwenye nyumba hii tukaelekezwa kwenye ‘ngome’ yenyewe ya Mzee Mkapa. Hapo kuna lango la kawaida tu. Kushoto kuna kibanda cha walinzi, na kulia ndipo kulipo na makaburi ya familia. 

Miongoni mwa waliohifadhiwa hapo ni wazazi wa Mzee Mkapa, dada na kaka zake, na baadhi ya ndugu. Kuna makaburi zaidi ya 10. Makaburi yote haya, pamoja na kaburi la Rais Mkapa, yamezungushiwa uzio mzuri wa matofali. Kaburi la Rais Mkapa ndilo pekee lililojengewa nyumba ndogo nzuri, na yenye viwango.

Wageni wanaruhusiwa kuzuru eneo lote la makaburi hadi kwenye viwanja. Hapa kuna nyumba kuu mbili – moja ni iliyojengwa na Rais Mkapa mwaka 2004, na pembeni kuna nyumba ya kawaida iliyokuwa mahususi kwa ajili ya walinzi wake. 

Ni nyumba za kawaida mno. Lakini pia kuna banda la mapumziko ambalo tuliambiwa Rais Mkapa alilitumia kusoma magazeti na vitabu mbalimbali. Ni banda la wazi, ambalo hata mtu aliye umbali wa mita 300 aliweza kumuona.

Banda jingine linatumika kutunza tausi ambao hayati Rais John Magufuli aliwapa zawadi familia zote za marais wastaafu. Kwa jicho la kawaida, wale tausi hali zao si nzuri, kwa sababu muda wote wanaishi ndani ya banda.

Mapema kabisa wakati tukijiandaa kuingia eneo la makaburi, wenyeji wetu walituhadharisha kuhusu upigaji picha. Picha ni kitu kinachozuiwa kabisa katika eneo hili. 

Nasi hatukuwa na sababu ya kuhoji uhalali wa zuio hilo japo binafsi ni uamuzi unaoweza kutafsiriwa kuwa unafifisha ari ya watu wengi zaidi kuzuru mahali alipolazwa mtu aliyeleta mageuzi makubwa mno ya kiuchumi, kisiasa na kijamii katika taifa letu.

Kwa upande wetu tulidhani ni jambo la heri watu wakaruhusiwa kupiga picha maeneo maalumu, hata kama ni kwenye sanamu la Rais Mkapa (endapo litajengwa), ili walau kupeleka salamu na hamasa kwa watu wengine kuingiwa shauku ya kuzuru Lupaso.

Nalizungumza jambo hili kwa unyenyekevu mkubwa kwa sababu inawezekana familia ndiyo iliyoamua iwe hivyo, na kwa maana hiyo uamuzi wowote kutoka kwao hauna budi uheshimiwe. Pamoja na ukweli huo, hata kama ni familia au ni mamlaka za serikali, kuna umuhimu wa kutambua kiu na mapenzi ya wananchi kwa Rais Mkapa, maana alikuwa kiongozi wao. 

Mara nyingi mtu aina ya Mkapa kwa ngazi aliyofikia, si mali binafsi ya familia au serikali. Huyu ni mtu wa Watanzania na walimwengu, na kwa maana hiyo kunapaswa kuwapo utaratibu wa kuwapa fursa watu kumuenzi kiongozi wao.

Nayaandika haya kwa staha kubwa nikitambua kuwa huenda bado serikali na familia wanajipanga kuifanya Lupaso kuwa eneo la kihistoria. 

Lakini wakati mpango huo (kama kweli upo) ukiandaliwa, ni vizuri wenye mamlaka wakayatazama makazi ya Rais Mkapa kwa jicho la pekee.

Makazi haya yanahitaji kujengewa uzio mzuri ili kuondoa hii dhana ya sasa ya kuwa ushoroba wa watu na mifugo. 

Makazi haya yanastahili kuwa na maji ya kudumu kwa ajili ya kustawisha miti, maua na kuwahudumia wananchi ambao kwa muktadha huu ni kama wako karibu na waridi lakini hawanukii.

Napendekeza kujengwe maktaba ya kisasa ili kuwawezesha watafiti, wasomi, wanafunzi na watu mbalimbali kufika Lupaso na kuchota maarifa kutoka kwenye maisha ya Rais Mkapa. 

Hilo liende sambamba na uanzishaji wa miradi ya kiuchumi itakayolifanya eneo hili liwe changamfu.

Mwisho, ninawapongeza kwa dhati vijana watumishi wa umma waliosimamia viapo vyao vya utumishi na kuhakikisha wanaendelea kuilinda na kuitunza Lupaso. Watu wa aina hii wanastahili pongezi.

Natoa mwito kwa mamlaka zilizozuia upigaji picha kupima faida na hasara za uamuzi huo. Kama faida ni chache, uamuzi huo utenguliwe. 

Tunapokuwa tukiendelea na maisha yetu mijini tusisahau kuwa Rais Mkapa aliyefungiwa pekee ndani ya nyumba yake Lupaso, anatuhitaji tufanye yanayowezekana ili jina lake lisifutike sasa na kwa vizazi vijavyo.

Bahati mbaya Watanzania hatuko vizuri kwenye utunzaji wa historia. Haya yanayoonekana Lupaso yameenea kwa Watanzania wengine waliolitumikia taifa letu kwa jasho na damu. Tusiwasahau. Pumzika kwa amani Mzee BWM.

By Jamhuri