Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania (5)

Huu ni mtiririko wa maandishi yaliyomo kwenye kitabu cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania kilichoandikwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mwaka 1994. Sehemu iliyopita, Mwalimu alisema, “Ni vigumu kuelewa kwa nini watu walio tayari kuwabebesha wananchi mzigo wa SeIikali tatu za kudumu, wanahofu gharama za kura ya maoni ya mara moja! Na kama viongozi wetu ni wapumbavu kiasi cha kwamba hawawezi kutunga swali “Je, unataka Serikali tatu?” Au “Je, unataka Serikali ya Tanganyika?” Kazi hiyo wangeweza kuwaachia wataalamu wenye uwezo zaidi.” Endelea…..

Kwa kutambua kwamba Bunge linafanya uamuzi yake kwa njia ya kura baada ya mijadala ya wazi, Serikali iliona kwamba hoja yoyote kati ya hizi ingewasilishwa bungeni, ingeweza kuligawa Bunge, kukigawa chama chetu na kuwagawa wananchi katika suala zito kama hili la Muundo wa Muungano.

Kuhusu suala la kura ya maoni, Serikali iliona kwamba utekelezaji wake ni sawa na kufanya uchaguzi mkuu, jambo ambalo ni la gharama kubwa.

 

Aidha, kwa kuzingatia kwamba kura ya maoni kupigiwa suala linalohitaji jibu la ‘NDIYO’ au ‘HAPANA’ , ni vigumu kupata swali lililo wazi kwa wananchi ambao hawana uzoefu wa utaratibu huo wa kura ya maoni.

Pamoja na hayo, kwa kuzingatia kwamba uamuzi wa kura ya maoni ni lazima ukubalike katika sehemu zote mbili za Muungano, itakuwa vigumu kupata uwiano wa kura utakaokubalika pande zote mbili kuwa ndiyo kiwango cha uamuzi.

 

10. Pamoja na juhudi za Serikali zote mbili kupitia Kamati ya Pamoja, Serikali zetu pia zilifikia makubaliano na kufanya maamuzi kuhusu baadhi ya matatizo mazito yaliyokuwapo katika Muungano wetu.

 

Maamuzi hayo ni:

(a) Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kukubali Zanzibar kujitoa katika uanacharna wa OIC;

 

(b) Utaratibu wa kumpata Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano uwe ni kwa njia ya kupigiwa kura kwa pamoja na mgombea urais (running mate).


11. Kwa msingi huu na kwa kuzingatia maamuzi ya awali ya Serikali ya kutaka kupata maelekezo ya chama na maoni ya wananchi kuhusu muundo utakaotatua matatizo ya Muungano, Serikali iliona kuna umuhimu wa kushauriana na wabunge waliohusika ili kupata mwafaka wa maudhui ya hoja yenyewe.

 

Mwafaka huo ulifikiwa katika kikao cha Kamati ya Wabunge wakikaa kama Kamati ya Chama tarehe 22/8/1993. Kutokana na mwafaka huo, hoja ya wabunge ilirekebishwa na azimio la Bunge kupitisha kwa kauli moja kwamba:

 

“Serikali iandae na kusimamia utaratibu utakaoshirikisha wananchi na taasisi mbalimbali ili kufikisha bungeni kabla ya Aprili 1995, mapendekezo ya muundo mwafaka wa Muungano ambao utazingatia haja ya kuwapo Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano pamoja na mambo mengine.

 

12. Azimio hili linaagiza mambo mawili yaliyo wazi:

(a) kupatikana kwa muundo mwafaka wa Muungano ambao unazingatia haja ya kuwapo Serikali ya Tanganyika.

 

(b) Kuwapo na utaratibu wa kushirikisha wananchi na taasisi mbalimbali utakaosimamiwa na Serikali kabla ya mapendekezo ya mwisho kufikishwa bungeni.

 

13. Kwa kuwa suala la muundo wa nchi ni zito na ni la kikatiba, ushirikishwaji wa wananchi ni jambo lisiloweza kuepukwa. Aidha kwa uzoefu wetu na hali halisi ya nchi yetu, ni lazima utaratibu wowote utakaokubalika, uwezeshe Serikali ya Jamhuri ya Muungano kushauriana na chama na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.


14. Kutokana na Azimio la Bunge, Serikali ya Jamhuri ya Muungano imeona kwamba suala la muundo wa Muungano, sasa linahitaji kufanyiwa kazi na kupatiwa uamuzi haraka zaidi na hivyo ni muhimu kuwasilishwa kwenye chama mapema kwa maelekezo, bila kusubiri mapendekezo ya Kamati ya Pamoja ili kuondoa hisia kwamba Serikali inajaribu kulikwepa suala hili.


15. Katika hali hii, Serikali inapendekeza kwamba Halmashauri Kuu ya Chama iafiki pendekezo la Serikali la kuandaa Waraka wa Serikali wa kutafuta maoni ya wananchi (white paper), kuhusu muundo mwafaka wa Muungano kwa kuzingatia mambo yafuatayo:


(a) Dhana ya kuwa na Serikali tatu ndani ya Muungano, yaani Serikali ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Tanganyika ikubalike. Muungano wa aina hii kwa sheria za Katiba na za kimataifa ni wa Shirikisho (Federation).


(b) Kwamba muundo uwe ni Muungano wenye Serikali tatu, yaani Serikali ya Muungano, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. lkumbukwe kwamba neno Muungano linavyofahamika kwenye sheria za Katiba na za kimataifa linamaanisha kwamba majukumu yale ya msingi ya dola yanahamishiwa kwenye Serikali ya Muungano.”


Haya ni maelezo ya ajabu sana kutoka kwa watu wazima kwenda kwa watu wazima wengine. “Kwanza kabisa, Serikali yetu inaiambia Halmashauri Kuu ya Taifa, “inaonekana kuwa hoja ya awali ingekuwa vigumu kuitekeleza kutokana na muda uliowekwa kufikia Februari 1994, na pia haikutoa fursa ya kupata maelekezo ya chama wala Serikali zetu mbili kushauriana.

“Aidha, kwa kutambua kwamba Bunge linafanya maamuzi yake kwa njia ya kura baada ya mijadala ya waziwazi, Serikali iliona kwamba hoja yoyote kati ya hizi ingewasilishwa bungeni ingeweza kuligawa Bunge, kukigawa chama chetu na kuwagawa wananchi katika suala zito kama hili la Muundo wa Muungano.”

Kwanza, hii “hoja ya awali” ambayo waheshimiwa hawa wanasema hawakuwa na muda wa kutosha kuitekeleza ni ile ya kutaka Serikali Tatu, ambayo kwanza, ni kinyume na sera ya Chama, pili, walikuwa wameagizwa na Kamati Kuu ya CCM siku chache zilizopita wakaipinge bungeni; tatu, tarehe 12 Agosti, 1993, Selikali yenyewe ilikuwa imeliambia Bunge kwamba ilikuwa inaandaa waraka wa kutafuta maoni ya wananchi kuhusu suala hili; na nne, (na pengine kutokana na kauli hii ya Serikali), tarehe 20 Agosti, 1993, wabunge wahusika walikuwa wamekwisha kuondoa hoja yao ya awali, nao wakaleta hoja mpya ya kuitaka Serikali ifanye referendamu ya kutafuta maoni ya wananchi.

Labda waheshimiwa wabunge nao waliona kuwa hoja hii ya kudai Serikali tatu “ikiwasilishwa bungeni, ingeweza kuligawa Bunge, kukigawa Chama chetu na kuwagawa wananchi katika suala zito kama hili la Muundo wa Muungano.”

Mimi siamini hivyo; naamini kuwa kama ingewasilishwa bungeni ili ijadiliwe, ingejadiliwa ikakataliwa na mambo yakesha.

Maamuzi yoyote ya kidemokrasia hayana budi yatokane na mjadala. Bila ya mjadala, maamuzi, hata yaliyo muhimu kabisa, yatafanywa kwa nguvu au kwa hila. Lakini kwa vyovyote vile, hoja hii, wabunge wahusika walikwisha kuiondoa.

Kama viongozi wetu waliamini kuwa kujadiliwa kwake kutaleta mgawanyiko huo waliouhofu, kwa nini, basi, walitaka kuitekeleza ila muda wa kufanya hivyo ndiyo uliokuwa hauwatoshi? Na kwa nini waliifufua tena? Hivi wao waliamini kuwa mjadala wa hoja ndiyo utaweza kugawa Bunge, na Chama, na wananchi, lakini kutekelezwa kwake hakutakuwa na matokeo hayo? Na ni nani alikuwa amewatuma wakaitekeleze?

Pili, Chama ambacho walikuwa hawakupata fursa ya kupata maelekezo yake kuhusu hoja ya Serikali tatu mpaka sasa sikijui! Chama Cha Mapinduzi kilikwisha kutoa maelezo yake zamani sana, kilipolikataa pendekezo la Tume ya Jaji Nyalali; Waziri Mkuu alikuwa amelieleza hivyo Bunge kwa maelezo mazuri sana; na Kamati Kuu ilikuwa imeyarudia siku chache tu kabla ya Serikali haijaamua kuipitisha hoja hiyo bungeni. Serikali ilitaka maelekezo ya Chama gani? Na Serikali zetu mbili zilitakiwa zishauriane kuhusu nini?

Serikali zote mbili ni za Chama Cha Mapinduzi. Na viongozi wake wote ni wajumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa, ambayo tarehe 10 Agosti 1993 iliwaagiza wakaipinge hoja ya Serikali tatu. Walitaka zishauriane juu ya jambo gani?

Hoja ya pili wanayoisema ni ile ya kura ya maoni. Wanasema: “Kuhusu suala la kura ya maoni, Serikali iliona kwamba utekelezaji wake ni sawa na kufanya uchaguzi mkuu, jambo ambalo ni gharama kubwa. Aidha, kwa kuzingatia kuwa kura ya maoni hupigiwa suala linalohitaji jibu NDIYO au HAPANA, ni vigumu kupata swali lililo wazi kwa wananchi ambao hawana uzoefu wa utaratibu huu wa kura ya maoni.”

Ni vigumu kuelewa kwa nini watu walio tayari kuwabebesha wananchi mzigo wa SeIikali tatu za kudumu, wanahofu gharama za kura ya maoni ya mara moja! Na kama viongozi wetu ni wapumbavu kiasi cha kwamba hawawezi kutunga swali “Je, unataka Serikali tatu?” Au “Je, unataka Serikali ya Tanganyika?” Kazi hiyo wangeweza kuwaachia wataalamu wenye uwezo zaidi.

 

Ila wasiwatukane Watanzania, ambao miaka yote hii wamekuwa wakipiga kura za NDIYO au HAPANA, kwamba ati wakiulizwa swali kama hili watashindwa kulijibu.

Ati kuuliza watu,

“SerikaLi ziwe tatu?”

Ni swali gumu ajabu,

Watashindwa kulijibu.

Tena ati wanasema,

Walihofia gharama,

Ila Serikali tatu,

Gharama zake si kitu.

“Pamoja na hayo,” Taarifa ya Serikali inaendelea, “Kwa kuzingatia kwamba uamuzi wa kura ya maoni ni lazima ukubalike katika sehemu zote mbili za Muungano, itakuwa vigumu kupata uwiano wa kura utakaokubalika, pande zote mbili kuwa ndiyo kiwango cha uamuzi.”

Hii ni abrakadabra ambayo sielewi kabisa maana yake. Lakini kwa vyovyote vile hoja ya kura ya maoni ingeweza kukataliwa, na mambo yakesha. Kwa nini Serikali haikufanya hivyo, ila badala yake ikafufua hoja ya Serikali tatu?

 

By Jamhuri