Serikali sikivu inafitiniana, inafitinika

Utawala wa Serikali sikivu chini ya  chama tawala unaendelea kuwadhihirishia Watanzania kuwa umefitinika na sasa kila kiongozi  anadunda na lake na kauli zake na maagizo yake, bila kujali kuwa  uamuzi wao kwa upande mwingine unawaumiza Watanzania ambao kila siku wamekuwa wanasifiwa kuwa Serikali yao sikivu inawasikia.

Serikali sikivu haina haja ya kughani kwenye vyombo vya habari kuwa yenyewe ni sikivu. Usikivu ulio bora hautangazwi  na kubandikiwa mabango uchwara huku wananchi wakipewa lugha za kilaghai. Wananchi si wajinga washindwe kujua  kuwa Serikali yao inawasikia au imeziba masikio isiwasikie.

 

Watanzania wa leo hawana muda wa kufundishwa na kuhadaiwa kwa lugha za kilaghai, huku wakiona na kushuhudia namna viongozi wa inayojiita ‘Serikali sikivu’ jinsi wasivyo wasikivu kwao.

Serikali inayojiita kuwa ni sikivu leo hii iko kwenye mgogoro mkubwa na wananchi wafugaji wa maeneo mbalimbali ambao mifugo yao imelazimishwa kuzisikia rasasi za polisi na hatimaye kuuawa.

Mifugo mingi  ya wafugaji imepigwa risasi kwenye kazi ya kurejesha makwao wahamiaji haramu. Mamia ya ng’ombe yamepigwa risasi na polisi wa Serikali hii sikivu ambao kombati, mishahara na marupurupu yao yanatokana na kodi za wanaoaminishwa kuwa Serikali yao ni sikivu huku ng’ombe wao wakiuawa.

Leo hii ndani ya Serikali hii kutokana na utawala kufitinika kuna viongozi wa Serikali wanaoona kuwa ni sawa kupigwa risasi kwa ng’ombe wa wafugaji, halafu wafugaji hao hao waende kuichagua Serikali ile ile sikivu ambayo leo inaua mifugo yao kwa risasi. Kibaya zaidi viongozi hao hao wa Serikali hiyo hiyo hawaoneshi dhamira ya dhati yenye dalili za kuwasaidia wafugaji hao.

Ukweli wa kushindwa kwa Serikali hii sikivu isiyosikia na kuonesha dhahiri kuwa imefitinika, unaonekana kwenye mambo mbalimbali ya msingi. Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda, kwenye uamuzi wake alitengua tangazo la Waziri Kagasheki la kuligawa eneo la Pori Tengefu la Loliondo, wilayani Ngorongoro, Arusha.

Kagasheki alikuwa ametenga kilomita za mraba 1,500 za pori hilo lenye  ukubwa wa kilometa za mraba 4,000 kwa ajili ya kuendelea kuwa chini ya miliki ya Serikali na kuviachia vijiji kilomita za mraba 2,500.

Tangazo hilo lilitolewa na Waziri Kagasheki, Machi 19, mwaka huu ili Serikali ihifadhi eneo la kilomita za mraba 1,500 ambalo alieleza kuwa ni mapito na mazalia ya wanyamapori, pia kutunza ikolojia ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Tangazo hilo liliibua mgogoro mkubwa. Waziri Mkuu katengua uamuzi wa Kagasheki huku Kagasheki huyo huyo siku chache akiwa ametoka kwenye vyombo vya habari na kutuhumu baadhi ya wahudumu wenye nafasi nyeti wa Serikali sikivu kujishughulisha na ujangili.

Ni Serikali hii hii sikivu ambayo Waziri Magufuli anasema wenye malori wasimamishe (malori) barabarani kwa kuwa yanaharibu barabara, baadaye inagundulika kuwa waziri huyo ameleta hasara kwenye Taifa ya karibu Sh. bilioni 20. Waziri mkuu anatoka huko aliko anasimamisha amri ya Magufuli, anasema magari yaendelee.

Hawa wote wanatoka Serikali moja na wanashiriki pamoja vikao vya Baraza la Mawaziri chini ya Mwenyekiti wa Serikali sikivu.

Waziri Magufuli aliagiza kuondolewa kwa msamaha wa asilimia tano kwa uzito wa magari yanayopita kiwango kilichopo, msamaha ambao umekuwa ukitumika nchini kwa zaidi ya miaka saba sasa. Badala yake aliagiza kuanzia Oktoba mwaka huu kila gari litakalozidisha uzito litatozwa faini ya mzigo uliozidi bila kujali msamaha huo.

Kutokana na uamuzi wa Magufuli ambao ulianza kutekelezwa Oktoba mwaka huu, wenye malori na mabasi walianza mgomo ambao uliendelea kwa siku kadhaa hasa malori.

Hali hiyo ilitishia kuanguka kwa sekta ya usafirishaji nchini, hivyo kumfanya Pinda kuingilia kati baada ya siku tano kwa kutengua agizo la Waziri Magufuli na kuagiza kurudiwa kwa utaratibu wa zamani wa msamaha wa asilimia tano ya ziada ya uzito ambao hautatozwa faini.

Kwa haya machache kati ya mengi ambayo msomaji wangu unayakumbuka, utaachaje kusema kuwa Serikali sikivu isiyosikia iko dhidi ya utawala uliofitinika?

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa simu Na 0713246764 Au 0784246764, Skype: Mohamedi.Mtoi, Twitter: @mohamedimtoi