nmb-4Kesho ni Oktoba 14, Watanzania katika maeneo mbalimbali nchini, watakutana iwe katika ibada maalum, kumbukizi au katika mazungumzo ya kumkumbuka Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyefariki dunia tarehe kama hiyo mwaka 1999.

Tarehe hiyo, Watanzania walipata mfadhaiko mkubwa uliozingirwa na huzuni na masikitiko mara tu walipopokea taarifa rasmi ya tanzia kutoka kwa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, iliyoeleza kuwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, amefariki dunia. Taarifa hiyo iliyosambaa kote nchini ilisababisha wananchi wa mijini na vijijini kusimamisha shughuli zao mbalimbali za kutengeneza bidhaa viwandani, kilimo mashambani na huduma maofisni, shuleni, hospitalini na kadhalika kwa manufaa ya jamii. Ukweli shughuli zilisimama wiki mbili nzima.

Kifo cha Mwalimu Nyerere kimetokana na maradhi yaliyomvaa mwilini ya kansa ya damu. Jitihada zilichukuliwa kutibu maradhi hayo hapa nchini na huko ughaibuni kwa nia ya kuokoa maisha yake. Waganga na waganguzi wa tiba hiyo walitafutwa na kupatikana watibu maradhi.

Serikali ilichukua jukumu la kumpatia tiba maridhawa katika hospitali kubwa na maarufu ya St. Thomas iliyoko jijini Londoni, Uingereza. Mwalimu alilazwa hapo kwa takribani majuma mawili. Matabibu wataalamu walifanya tiba mchana na usiku kuokoa maisha yake. Lakini tiba hazikuweza kutibu barabara maradhi hayo mbele ya matabibu na baadhi ya familia yake, ndugu na viongozi wa Serikali. Mwalimu Nyerere alikata roho. Kilio. Nchini kote wananchi waliomboleza kifo hicho. Nyimbo za majonzi ziliimbwa. Ibada ziliendeshwa na maandalizi ya mazishi yalipangwa na kutimizwa.

Hekaheka ilionekana tangu mwili ulipoletwa na kupokewa Oktoba 18, hadi Oktoba 23, 1999 ulipozikwa kijijini Mwitongo, Butiama. Mwenyezi Mungu amuweke mahali pema peponi.

Mwalimu Nyerere alipoondoka duniani aliacha mambo ambayo Watanzania walipaswa kuyaendeleza katika kulinda na kuhifadhi mustakabali wa Taifa letu. Laiti tungeyazingatia wala tusingekuwa na itikadi hizi za kimaslahi (ideological interest) katika nchi yetu.

Leo tunapomkumbuka Mwalimu Nyerere imeshatimu miaka 16. Baadhi ya mambo yameharibika wala hayasemeki na hayachukuliki. Kisa tumepoteza umiliki wa itikadi yetu ya uadilifu. Wananchi wengi wanalia na wananchi wachache wanachekelea.

Kusudio la makala hii ni kuangalia Mwalimu aliacha nini kwa Watanzania, ambacho tungeweza kujivunia na kutamba mbele ya mataifa mengine duniani wakati baadhi yao hawana tulichonacho sisi.

Kabla ya kuangalia alichotuachia, nafikiri ni busara kukumbusha historia fupi ya maisha yake tangu kuzaliwa, masomo, harakati za kisiasa na kuungana na Watanzania katika kulikomboa Taifa letu kutoka katika mikono ya wakoloni.

Itoshe kueleza kuwa Mwalimu Nyerere alianza kuliona jua tarehe 13 Aprili, 1922 kijijini kwake Mwitongo, Butiama. Akiwa ni mtoto wa baba  Chifu Burito Wanzagi na mama Christina Mugaya Nyang’ombe.

Titi la mama yake lilimpa siha nzuri iliyompendezesha mbele ya jamii na kupevusha akili zake mapema hadi kumudu masomo shuleni na kazi zake za mikono kuwa mfano na vielelezo kwa wazazi, ndugu na jamaa zake. Uchungaji mbuzi ulikuwa upendeleo wake.

Alipotimu miaka 12 alianza elimu ya msingi katika shule ya Misenge. Elimu hiyo haikumpa shida. Mwaka 1937 alianza masomo ya sekondari pale St. Mary Tabora ambako hakwenda kapa. 1943 akaenda Chuo cha Makerere, Uganda na kuchukua Diploma ya Ualimu.

Julius Nyerere alitambua fika elimu ni ufunguo wa maisha yake na urithi wake wa kudumu. Kati ya Oktoba 1949 na Julai 1952 alisoma Chuo Kikuu cha Edinburgh, Scotland na akapata Shahada ya Uzamili (MA). Elimu yote hiyo ilikuwa ni mtaji wa baadaye kudai ukombozi wa Mtanzania.

Elimu na taaluma yake aliyopata ilimwezesha kufundisha katika shule za Tabora na Pugu. Hata hivyo, alitambua bado alikuwa na upungufu wa kuendesha maisha yake. Ndipo alipoamua kufunga ndoa na Mwalimu mwenzake, Maria Gabriel Magige, mnamo Januari 12, 1953.

Mnamo Februari, 1953 Mwalimu alihamishwa na kufundisha St. Francis College (sasa ni Pugu Sekondari) Mwakanga, Dar es Salaam. Akiwa Pugu alianza rasmi mambo ya siasa na kushirikiana na vijana na wazee wa Dar es Salaam  kuanzisha chama chs Tanganyika African Association (TAA) mwaka 1953  na baadaye kuanzisha chama cha Tanganyika African National Union (TANU) Julai 7, 1954. Hapo pumu zilipata mkohozi kwani harakati za kudai Uhuru wa Watanganyika zilianza rasmi chini ya uongozi wake. 

Baada ya kueleza historia fupi ya maisha yake Mwalimu Nyerere, sasa nirudi kwenye mada niliyokusudia kuiangalia Mwalimu aliacha nini kwa Watanzania. Historia bado inatukumbusha kuwa harakati hizo ziliwachukua Watanganyika miaka saba (1954-1961) kupata uhuru wa bendera bila mapigano wala kumwaga damu. 

Mkikimkiki wa siasa Tanganyika ulisambaa kuanzia Dar es Salaam; mashariki hadi Kigoma; magharibi. Kutoka Arusha; kaskazini hadi Mtwara; kusini pamoja na majimbo (sasa mikoa) yote nchini, wananchi walizungumza na kuimba nyimbo katika lugha moja tu ya Uhuru na Kazi na Uhuru Kazi ya TANU.

Lugha za makabila zaidi ya 120 hazikupata nafasi mbele ya lugha ya Kiswahili kwa sababu ya uelewano na mshikamano. Kiswahili ikawa ndiyo lugha ya mawasiliano. Udini haukuhesabika kama ni mtaji wa kuleta Uhuru wala ukabila haukuthaminiwa kama kete ya ushirikiano. Kazi ilikuwa zana madhubuti ya kuleta maendeleo ya watu. Uzembe na uzururaji ziliorodheshwa ni maadui wa kuleta Uhuru na chachu ya kudumaza unyonge wa Mtanganyika.

Ukweli mkoloni alisemwa na kutukanwa na hakika alistahili matusi aliyopewa. Alikuwa kupe ndani ya nchi yetu. Wanawake kwa wanaume waliungana kumng’oa mkoloni. Desemba 9, 1961 bendera ya kikoloni (Union Jack) iliteremshwa na bendera ya kibantu ilipanda. Ujenzi wa nchi ulianza, utamaduni ulienziwa na ulinzi na usalama ulidumishwa. Elimu ya siasa na itikadi ya nchi ilifundishwa kwa wananchi. Uchumi wa nchi uliboreshwa na kulindwa. Yote hayo yalifanywa chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere.

Dira ya nchi iliwekwa kwa kuanzishwa Azimio la Arusha na siasa yake ya Ujumaa na Kujitegemea ilipokewa. Juhudi na maarifa kuwa ni misingi ya maendeleo.Vitu vinne vya kuendeleza nchi watu ni ardhi, siasa safi na uongozi bora vilibainishwa kwa wananchi.

Maadui watatu wa Taifa letu walitambuliwa na kushambuliwa – ujinga, maradhi na umaskini. Shule zaidi zilijengwa na kuboreshwa. Vyuo vilianzishwa na kuendelezwa. Zahanati, vituo vya afya na hospitali zilijengwa na bila kusahau elimu ya lishe na chakula bora. Elimu ya ufundi na uhandisi mbalimbali ilitolewa na viwanda vidogo na vikubwa vilijengwa. Zana za kilimo mbolea na dawa za kuua wadudu waharibifu wa mazao mashambani zilitengenezwa.

Vijiji na miji iliongezeka na kupanuka. Ongezeko hilo lilitokana na elimu ya afya kutolewa na kueleweka ndani ya kila familia na kuweka afya njema kwa kila mtu. Kutoka watu milioni 9 mwaka 1961 hadi kufikia watu milioni 47 mwaka 2012.

Mafanikio yote niliyotaja na yale nisiyoyataja chanzo chake ni busara, hekima ukweli na adili ya Mwalimu Julius Nyerere. Leo baadhi ya mambo hayo hayapo kwa sababu hakuna mtu wa kusimamia! Ndani ya miongo miwili Watanzania tunayumba kwa sababu ya kuacha itikadi ya Taifa.

Katika miaka yake 77 ya kuishi duniani (1922-1999) Mwalimu ametuachia mambo manne kwa mtazamo wangu. Ameacha Uhuru wa kisiasa (political independence).

Watanzania walijitambua kifikira na uhuru wa mawazo yaliyowawezesha kutetea haki zao na za ndugu zao barani Afrika. Walipambana katika vita ya ukombozi na kuondoa unyonge wa Mwafrika. Mapambano dhidi ya unyonyaji wa uchumi wa Waafrika na kutawaliwa kimamboleo katika misingi ya soko huria na uwekezaji wa kimasharti. Kukataa kasumba za kitamaduni na kibiashara. Leo mambo hayo yamepewa kipaumbele na matokeo yake Mwafrika anadhalilika.

Pili, kujiamini (self-confidence) Watanzania tulikuwa na uthubutu kwa kusema na kutenda jambo. Tulitetea na kusimamia itikadi na tamaduni za mwananchi ndani ya nchi na nje ya nchi bila haya wala woga. Tulishiriki kazi pamoja na kutambua utu wetu.

Tatu, alituachia zingatio la itikadi (ideological commitment); viongozi na wananchi walithamini na kuzingatia msimamo na mwelekeo wao katika maslahi yao wakati wakitekeleza shughuli zao za maendeleo. Wananchi waliamini na kuthamini mali na rasilimali za Taifa ni mali yao wote.

Wananchi walikemea na vyombo vya haki vilihukumu bila upendeleo pale mtu alipofanya uhalifu wa kuhujumu mali na uchumi wa Taifa. Leo wananchi kwa njia fulani fulani wanakosa ari ya kutetea maslahi ya Taifa!

Nne, utambulisho wa Taifa (national identity) wananchi walijitambulisha mbele ya mataifa mengine kwa lugha yao, mavazi yao ya heshima, uthibiti wa kauli na matendo yao katika kulinda na kutumia kihalali mali ya Taifa.

Mambo hayo ndiyo yaliyojenga amani na umoja ambao leo tunajivunia. Lakini sasa umoja wetu upo mashakani kwa kutaka kuruhusu udini na ukabila kutamba katika nchi yetu. Amani yetu inatetereshwa na baadhi ya wenzetu kwa kuipa njia rushwa (ufisadi) na dhuluma kuibana haki.

Namalizia kwa kusema Mwalimu alikwisha kusema Watanzania wanataka mabadiliko, wamechoka na rushwa, umaskini, udini na ukabila.

Mabadiliko hayo lazima yaondoe mambo hayo. SIYO mabadiliko ya kufagilia rushwa kwa kutumia nyenzo ya kuchukia au kuondoa umasikini, kwani umaskini umejengwa na kupenda rushwa na ufisadi. Tuko tayari katika hilo. Imeandikwa.

2096 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!