Bajeti Kuu ya Serikali tayari imesomwa bungeni Dodoma. Imesheheni mambo mengi. Wataalamu wa uchumi wamejitokeza kusema waliyoyaona. Wapo wanaopongeza, kadhalika wapo wanaoikosoa.

Wakosoaji wanahoji ukubwa wa tarakimu za bajeti hiyo. Wanasema kama iliyopita imeyekelezwa kwa kiwango kisichozidi asilimia 50; kwanini hii ya mwaka huu wa 2017/2018 nayo iwe na tarakimu nyingi zaidi. Jibu wanalo waandaaji.

Pamoja na yote yanayosemwa, walau yamo mambo mengi ya maana kabisa. Mathalani, kufutwa kwa Motor Vehicle License. Ushuru huu ulikuwa kero kubwa. Mtu alitozwa bila kujali kama gari lake lipo au halipo barabarani. Kuuweka kwenye mafuta, ni uamuzi mzuri. Hii itaongeza mapato ya Serikali. Wapo walioukwepa kwa kutembeza magari yao, lakini sasa hata wafanye namna gani, hawana namna ya kuukwepa. Pengine itumike nishati mbadala!

Shida inayoonekana kwenye uamuzi huu ni kiwango cha Sh 40 kwa kila lita. Si vibaya kiwango hicho kingekuwa chini kidogo, japo kwa Sh 20 au chini zaidi. Naamini hilo linazungumzika. Wakati wa majumuisho Waziri anaweza kulirekebisha.

Pili, kwa moyo wa dhati kabisa naipongeza Serikali kwa kurejesha ushuru wa asilimia 10 kwenye mafuta ya mawese yanayoingizwa nchini. Hiki kimekuwa kilio cha wakulima na wafanyabiashara wengi wa Tanzania.

Tanzania ya viwanda haiwezi kustawi kama tungeacha utaratibu huu wa kuingiza mafuta ya mawese nchini uendelee. Kufanya hivyo ni kuwanufaisha maelfu ya wakulima katika mataifa ya Malaysia na Indonesia.

Katika toleo namba 230 la JAMHURI niliandika kwa kirefu dhambi hii. Nilisema uingizaji mafuta ya kula ya mawese kutoka Malaysia na Indonesia, tena bila kuyalipia ushuru, ni kifo kwa wakulima wetu. Kibaya zaidi, wakulima wa huko wanapata ruzuku kutoka serikali zao kwa hiyo kuruhusu mafuta hayo bila kodi ni kutangaza kifo kwa wakulima wetu.

Kampuni zinazoingiza mafuta ya mawese zinahadaa kwa kusema zinaingiza mafuta ghafi! Hii si kweli hata kidogo. Mafuta hayo huwa yameshasafishwa kwa asilimia zaidi ya 90. Bahati nzuri wapo viongozi wetu kama Dk. Chrisant Mzindakaya, Dk. Zainabu Gama na Dk. Kilontsi Mpologomyi ambao walifuatilia vema hadaa hii na kubaini uongo mwingi.

Wakati fulani ushuru kwa mafuta hayo ulikuwa asilimia 10, lakini katika namna isiyoashiria uadilifu, Waziri wa Fedha wa wakati huo, Dk. Mustafa Mkulo, mwaka 2009 alifuta ushuru huo na kuwa sifuri!

Mawese, mbali ya kutoa mafuta, ni malighafi kwa utengezaji sabuni na vyombo mbalimbali kama viti, meza, sahani, ndoo, na kadhalika.

Hawa waagizaji wakishapata mafuta, malighafi inayobaki huitumia kutengeneza bidhaa hizo. Wale wenye viwanda vidogo wanapohitaji malighafi hiyo, njia pekee ya kuwanyima ni kuwauzia kwa bei ghali. Matokeo yake ni kufa kwa viwanda vingi vya vya wazalendo hapa nchini. Hatua hiyo iliwafanya ‘wababe’ wa uagizaji mafuta waendelee kutamba wao wenyewe kwenye mafuta, sabuni na utengenezaji bidhaa kama viti, meza, sahani na kadhalika.

Kufutwa kwa ushuru kwenye mafuta ya mawese ni mkakati madhubuti uliosukwa na wafanyabiashara wakubwa na kufanikiwa kuwarubuni ‘mabwana mipango’ wa serikali yetu.

Wastani wa mafuta ya mawese yanayoingizwa nchini ni tani 300,000 kwa mwaka. Kiwango hiki kingeweza kuipatia Serikali mabilioni ya shilingi kama kodi na ushuru. Nikashauri kwamba kwa kuwa Serikali ilikuwa kwenye maandalizi ya bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017, lingekuwa jambo la maana mno endapo ushuru kwenye mafuta ya mawese yanayongizwa nchini ungerejeshwa.

Mwaka 2009 ushuru ulipofutwa ulikuwa asililimia 10; nikapendekeza Serikali sasa ione busara ya kuongeza kiwango hicho walau hadi asilimia 20. Hiyo itasaidia kulinda viwanda vyetu vya ndani na ajira kwa Watanzania.

Hatuwezi kujenga viwanda vipya vya mafuta ya kula endapo hakutakuwapo malighafi ya kutosha. Malighafi inazalishwa na wakulima. Kilimo hakiwezi kustawi endapo soko la bidhaa halipo.

Hoja ya kwamba nchi yetu ina uhaba wa mafuta ya kula; na kwa sababu hiyo lazima tuagize kutoka nje, kwa maneno mengine ni kusema tusiwe na wakulima! Mahitaji ya soko ndiyo njia pekee ya kuwahamasisha vijana wengi kukipenda kilimo.

Aliyekuwa Mbunge wa Kwela, Dk. Chrisant Mzindakaya, alizungumza vizuri sana suala la haya yanayoitwa mafuta ghafi. Akasema hakuna kitu kinachoitwa “mafuta ghafi”. Wanachofanya wafanyabiashara ni kuleta mafuta yaliyokwishasafishwa. Akasema alisafiri hadi Indonesia, Malaysia na kwingineko, kufanya uchunguzi.

Akasema kwamba hicho kinachoitwa mafuta ghafi, ni uongo. Hakuna mafuta ghafi yanayoingizwa Tanzania, bali ni mafuta halisi ya kula yaliyokwishapitia usindikaji kwa asilimia 95! Huyu hawakumsikia.

Aliyekuwa Mbunge wa Kibaha Mjini, Dk. Gama, akiwa bungeni alitumia maneno ya kila aina kuonyesha kuwa uamuzi wa Serikali ulikuwa sawa na mauaji kwa wakulima masikini. Hawakumsikia.

Aliyekuwa Mbunge wa Tabora Mjini, Silaju Kaboyonga, akahoji kama kweli ni akili kufanya hicho kilichokuwa kimeandaliwa na Serikali. Hakuna kiongozi wa Serikali aliyefungua masikio kuwasikiliza, wala hakuna aliyefungua akili kufanya tafakuri ya maneno hayo.

Aliyekuwa Mbunge wa Kasulu Magharibi Kilontsi Mporogomyi, yeye alikwenda mbali zaidi. Akatoboa kwamba kuna dalili zote za rushwa kwenye suala hilo. Yeye pia alishakwenda huko nje kujiridhisha kama kweli kinacholetwa ni mafuta ghafi. Akakuta ni uongo. Hakuna mafuta ghafi, bali ni mafuta yaliyokwishasindikwa. Akafikia hatua ya kupendekeza Bunge liunde Kamati Teule kuchunguza hujuma hiyo. Haikuundwa.

Hawa ni sehemu ndogo tu ya wabunge wengi mno waliopinga uondoaji ushuru wa asilimia 10 kwenye mafuta hayo. Awali, nilidhani kuwa busara za wabunge wapinzani ndizo hubezwa, kumbe hata wa CCM nao huwakuta!

Mwenyekiti Mao Tse Tung wa China aliwahi kupiga marufuku uagizaji bidhaa kutoka nje ya nchi hiyo. Alipiga marufuku akilenga kuhakikisha Wachina wenyewe wanabangua bongo, wasomi wanakesha, wana sayansi wanakuna vichwa kupata njia sahihi ya kujitegemea. Alipiga marufuku hata uagizaji viatu.

Watu walipiga kelele. Wakasema Mao alikuwa mtesaji. Wakamtukana. Wakampa majina mabaya ya kila aina. Nchi za Magharibi, kwa kujua Mwenyekiti Mao alikuwa akipeleka ukombozi kwa wananchi wake, zikapandikiza uongo na chuki. Eti huo ulikuwa ukiukaji haki za binadamu na udikteta. Yote hayo yalikuwa ni kutaka kuhakikisha China inaendelea kuwa soko la Ulaya na Marekani. Na ili iendelee kuwa soko, lazima kuwapumbaza Wachina waendelee kununua vitu vya nje. Lakini wapi? Mwenyekiti Mao akawa imara.

Alipofariki dunia, viongozi waliomfuata waliboresha mawazo yake. Wakayachanganya na mawazo mapya. Wakapata sera nzuri za kujenga uchumi wao. Lakini kubwa walilokuwa wameweka mbele ni suala la kujitegemea. Mwenyekiti Mao na viongozi hao waliomfuata na waliamini kuwa katika kujitegemea lazima kuwe na mahali pa kuanzia! Ndivyo nchi inavyojengwa.

Juni 2009 niliandika makala yenye kichwa cha habari: “Kuna jambo tumemkosea Mungu!” Nilisema kama viongozi wetu hawaoni mafuta mazuri ya alizeti yanayouzwa pale Singida, mafuta yanayotokana na teknolojia ya mikono; tuna sababu gani ya kuwaamini?

“Nawapa pole wakulima. Wamenyongwa na watu waliowachagua. Wamepuuzwa na watoto wao waliowasomesha kwa fedha hizo hizo za alizeti na ufuta! Wametiwa kitanzi cha maisha na hao hao walioapa kuwatetea.

“Wakulima wasikate tamaa wala kuhuzunika. Huu ni mchakato wa mapambano ya kuelekea kwenye ukombozi wa haki. Wengine migongo yao imepinda kwa kutumia jembe la mkono. Wengine wamepoteza jicho au macho kutokana na kuumizwa wakati wa kulima au kuvuna. Wengine wana makovu yanayotokana na visiki mashambani. Wengine wameng’atwa nyoka au kuliwa na simba au mamba wakihangaika mashambani.

“Wakulima wetu wasikate tamaa. Kuna siku, kama si wao, basi watoto na wajukuu wao watafurahi. Hatutarajii kudumu milele na viongozi wasiokuwa na huruma kwa wakulima. Yana mwisho.

“Kama ushuru huo ni matokeo ya mlungula miongoni mwa viongozi wetu, Mungu wa haki ataamua.”

Waziri wa Fedha wa wakati huo (mwaka 2009) alikuwa Mustafa Mkulo. Nikahitimisha kwa maneno haya na mwisho nikaweka shairi. Nikasema; hadi hapo hayo yatakapotimia, kizazi cha wakulima kitakachokuwa kimejaa furaha kitaimba kwa kusema:

 

1: Mkulo ulitutesa, Wakulima tukalia

Ulitufanya matasa, Maisha tulililia

Njoo utuone sasa, pepo tumefungulia

Mwenyezi Mungu wa haki, Hawatupi waja wake.

 2: Wakulima ughaibu, Uliwaona nduguzo

Pesa ziliwaghiribu, Tukafanana uozo

Wote mkawa mabubu, Maisha yetu mzozo

Mungu yule wa Yakobo, Ndiye wa Abrahamu.

 

3: Mashangingi mlipanda, Mkapuza makabwela

Zamu ni yetu kudanda, Jehanamu mtalala

Taadhima imepanda, Mapochopocho twayala

Kumwonea mkulima, Laana mmeipata.

Naam, niliyoyasema mwaka 2009 yametekelezwa mwaka 2017. Mungu ni mwema. Kilio cha wakulima kimesikika.

By Jamhuri