Kazi ya uchambuzi wa taarifa za utafiti wa awali kuhusu rasilimali za mafuta na gesi asilia katika visiwa vya Zanzibar na bahari yake, imeanza huko Edinburg, nchini Uingereza, na inatarajiwa kukamilika baada ya mwezi mmoja.

Uchambuzi wa taarifa za utafiti wa awali unafanywa na wataalamu waliobobea katika kazi utafutaji na uchimbaji wa mafuta kutoka kampuni ya Bell Geospace ya nchini Uingereza, wanaofanya kazi hiyo kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Kampuni ya Uchimbaji Mafuta ya RAKGAS ya Ras Khaimah kutoka Falme za Kiarabu.

Uchambuzi huo wa kitaalamu unaanza baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya utafiti wa utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia kwa kutumia ndege maalumu, kukamilika.

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Maji Nishati na Mazingira Zanzibar, Ali Khalil Mirza, amesema wamejulishwa na wataalamu wa kampuni ya Bell Geospace kwamba ripoti ya utafiti huo wa awali itawasilishwa serikalini baada ya mwezi mmoja kuanzia sasa.

“Kwa sasa ni vigumu kusema chochote kuhusiana na rasilimali ya mafuta na gesi asilia hapa Zanzibar, tunasubiri ripoti yao wataalamu watasema nini, wameona kitu gani kwa sasa taarifa zitabaki kama zilivyo,” amesema Katibu Mkuu Mirza.

Katibu Mkuu huyo ameliambia JAMHURI kwamba utafiti uliofanyika kwa kutumia ndege ni moja ya tafiti zinazotumia teknolojia ya hali ya juu ambazo hazina athari zozote kimazingira wala kuathiri miundombinu.

Wataalamu wa Kampuni ya Bell Geospace walijikita zaidi katika kutafiti rasilimali ya mafuta na gesi asilia katika kitalu cha Pemba-Zanzibar ambapo inaaminika kuwa huenda kukawa na uwezekano wa kuwapo kwa rasilimali ya mafuta.

Pamoja na kutafiti eneo hilo, pia wataalamu hao walifanya utafiti katika maeneo mengine ya bahari ya Zanzibar, ambapo kwa mujibu wa maelezo ya Katibu Mkuu Mirza, kazi hiyo imekwenda vizuri na watafiti hao walijiegemeza zaidi katika kitalu cha Pemba-Unguja ambapo waliruka kila siku kwa muda wa saa sita.

“Huu ni utafiti wa awali, nachukua fursa hii kuwajulisha kwamba wataalamu wetu wamekamilisha kazi na wamefanikiwa kukusanya taarifa za kutosha kuhusiana na rasilimali ya mafuta na gesi asilia hapa Zanzibar,” amesema Katibu Mkuu Mirza.

Katibu Mkuu amesema, awali kazi hiyo ilipangwa kufanyika kwa muda wa miezi miwili. “Mwezi mmoja ndiyo utafiti wenyewe, lakini wakaweka na mwezi mwingine ikiwa kutatokezea dharura yoyote ambapo haikuweza kutokezea na hivyo kukamilisha ndani ya wiki tatu,” amesema.

Kiongozi wa timu ya watafiti kutoka Kampuni ya Bell Geospace Enterprises Limited ya Uingereza, Stefan Kuna, anasema suala la kuwapo au kutokuwapo kwa rasilimali ya mafuta na gesi asilia kutategemea uchambuzi wa taarifa walizokusanya wakati wa utafiti.

“Sisi tulifanya FTG ( Airborne Full Tensor Gravity Gradiometry Survey), tunachofanya ni kukusanya taarifa na kuziwasilisha kwa ajili ya uchambuzi ambapo naamini kutakuwa na matokeo mazuri,” amesema Stefan.

Stefan amesema wametumia muda wa wiki tatu kufanya kazi hiyo tofauti na makisio ya awali ya miezi miwili kutokana na kuanza kwa kipindi cha mvua za masika, kwani vifaa wanavyotumia vina unyeti fulani usiotakiwa kuingiliwa na chochote kisichohusika kama vile sauti au mtikisiko.

“Ndege yetu ina vifaa ambavyo havihitaji vishindo, kama tutaruka wakati wa mvua na ngurumo za radi, basi inaweza kuingia katika kurekodiwa kitu ambacho sisi hatukuhitaji katika utafiti wetu na kwa sababu hiyo ilitulazimu kufanya kazi muda mwingi zaidi,” amesema mtaalamu huyo.

Kiongozi huyo wa timu ya wataalamu amesema kazi yao ilikuwa ni kukagua miamba iliyoko chini ya ardhi ambapo kwa kitaalamu kazi hii inajulikana kama “Airborne Full Tensor Gravity Gradiometry Survey (FTG).”

Amesema katika kitalu cha Pemba-Zanzibar wameona chembechembe za mafuta, lakini taarifa zaidi ya kuwapo kwa rasilimali ya mafuta na gesi asilia itapatikana baada ya kukamilika kwa kazi ya uchambuzi wa taarifa yao watakayoiwasilisha makao makuu ya kampuni ya Bell Geospace ya Uingereza.

Amesema kazi ya uchambuzi wa taarifa za kitafiti walizokusanya itakamilika ndani ya mwezi mmoja, na wataikabidhi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Kampuni ya RAKGAS ya Ras Khaimah, Falme za Kiarabu.

Naye mtaalamu wa masuala ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta kutoka Kampuni ya RAKGAS ya Ras Khaimah, Graham Cunningham, ambaye pia ni Meneja Mkaazi wa RAKGAS Zanzibar, amesema kimsingi kazi iliyoko mbele ni kubwa zaidi kwani huu ni utafiti wa awali tu.

“Kuna kazi ni kubwa mbele yetu. Utafiti huu uliofanywa tunauita FTG (Airborne Full Tensor Gravity Gradiometry Survey), utatusaidia kujua object ilipo, lakini kazi bado inaendelea,” amesema mtaalamu huyo.

Amesema katika kipindi cha miezi mitatu au minne, wanatarajia kuanza awamu ya pili ya utafiti kwa kutumia meli maalumu ambayo itakuwa na kazi ya utafiti wa mafuta na gesi asilia katika mwambao wa pwani ya Zanzibar katika kitalu cha Pemba-Zanzibar.

Mtaalamu huyo amesema pia utafiti huo utahusisha gari maalumu litakalokuwa likitafiti katika maeneo ya ardhini katika sehemu ambazo taarifa zake zimetolewa katika utafiti wa awali uliofanywa na ndege ya Kampuni ya Bell Geospace.

“Zanzibar ni eneo muhimu sana kwa sasa kuhusu rasilimali ya mafuta na gesi asilia, tunaamini Zanzibar inaweza kushangaza ulimwengu katika rasilimali hii. Jambo muhimu kwa sasa ni kukamilisha utafiti kuweza kupata uhakika zaidi juu ya kiwango cha mafuta kilichopo,” anasema mtaalamu huyo kutoka RAKGAS.

Kampuni hiyo ya kigeni inasaidiwa kazi na kampuni ya kizalendo ya Brunswick Zanzibar Limited, ambayo inahusika na shughuli za uombaji wa vibali kutoka serikalini kwa ajili ya ufanikishaji wa kazi ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia hapa Zanzibar.

Kazi ya utafiti wa utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia Zanzibar ilianza rasmi Machi 18, baada ya uzinduzi uliofanywa na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, Machi 14, kwa Kampuni ya Bell Geospace Enterprises Limited ya Uingereza kufanya utafiti huo kwa niaba ya Kampuni ya RAKGAS ya Ras Khaimah, Falme za Kiarabu.

Wakati kazi ya uchambuzi wa taarifa za utafiti ikiendelea nchini Uingereza, wananchi wa Zanzibar wanasubiri kwa shauku kubwa ripoti ya uchambuzi huo ambayo bila shaka inaweza kubadili mwelekeo mzima wa uchumi wa visiwa hivi.

Suleiman Ame, mkazi wa Mkokotoni, Mkoa wa Kaskazini Unguja, anasema ugunduzi wa mafuta na gesi asilia utawafanya kubadili shughuli zao za kujitafutia kipato, badala ya kupoteza muda mwingi katika shughuli zisizokuwa na tija wanaweza kunufaika na neema ya mafuta.

“Sisi bwana tunasubiri kwa hamu hiyo ripoti ya watafiti, lakini jambo la muhimu ni kuwa Zanzibar mafuta yapo, hili hakuna ubishi na ndiyo maana makampuni yanaanza kuyatafuta hakuna mtu anayeweza kupoteza pesa zake tena nyingi kwa jambo la kubahatisha,” amesema Ali Makame Issa, mkazi wa Malindi, Mkoa Mjini Magharibi Unguja.

Ali Makame anasema yeye amewahi kusikia simulizi nyingi kuhusiana na kuwapo kwa rasilimali ya mafuta Zanzibar. 

“Mimi nakumbuka tangu nipo mdogo nawasikia watu wazima wakizungumza juu ya kuwapo kwa mafuta, lakini sasa napata matumaini baada ya kuja hawa wataalamu kuanza utafiti,” anasema Ali Makame, ambaye kwa sasa umri wake ni mtu mzima.

2264 Total Views 3 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!