foleniKwa muda mrefu sasa nina dukuduku la kuuliza Wanatanzania wenzangu hasa wale wachumi waliobobea kama akina Profesa Ibrahim Lipumba au Profesa Simon Mbilinyi vile.
  Suali langu; ni vigezo gani katika Taifa linaloendelea vinaonesha kukua kwa uchumi katika Taifa?


  Wako wachumi wengi hapa nchini lakini hapa nimewataja hawa maprofesa wawili kwa vile kila mmoja kwa muda fulani aliwahi kuwa Mshauri wa Rais pale Ikulu katika masuala ya uchumi.
  Profesa Mbilinyi aliwahi kuwa mshauri wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wakati fulani miaka ile ya 1970 na kitu. Profesa Lipumba naye aliwahi kuwa mshauri wa Rais Mwinyi ‘Mzee Ruksa’ pale Ikulu miaka ile ya 1985 na ushei. Ilivyo, wote wawili hawa wamehusika na hali ya uchumi wa Taifa letu katika ngazi ya Taifa.


 Wote wawili hawa wameshughulika na uchumi wa Taifa kiuzalendo na hivyo wanatazama kule tulikotoka na hapa tulipo sasa, basi kwa ulinganisho tu wanaweza kunijibia  kwa ufasaha swali langu hilo.
  Huwa nasikia wataalam wa uchumi wakisema, uchumi wa Taifa letu unakua kwa asilimia fulani kila mwaka. Hapo ndipo ninapopenda nielimishwe huko kukua kwa uchumi vigezo vyake kimataifa ni vipi? Mizania gani inatumika kitaifa katika nchi mbalimbali kuonesha kuwa uchumi wa taifa fulani unakua au uko pale pale umetuama, au unaporomoka na hivyo kuelekea mwanguko.


 Watu wengi wa kawaida hapa nchini wanasifia wingi wa magari. Nchi hii sasa inafurika kwa aina za vipando; yapo mapikipiki, yapo magari madogo madogo, yapo mabasi ya kubeba abiria na yapo malori ya kubeba mizigo. Kwa kifupi yapo magari chungu nzima katika mabarabara yetu yote.
 Basi huku kuwapo kwa hayo magari mengi sana nchini wengine ndiyo wanaona uchumi wa nchi yetu umepanda sana. Magari hayanunuliwi kwa fedha za madafu bali yananunuliwa kwa fedha za kigeni na ni dola za Marekani, au yuro za Ulaya. Hapo ndipo watu kama sisi wa kawaida tunapojiuliza; magari mengi namna hii Taifa linaagiza kutoka Ujapani, lazima Taifa letu lina fedha nyingi sana za kigeni. Basi tu matajiri! Inawezekanaje kuagiza gari bila fedha?


 Dhana nyingine inapingana na hiyo. Hii inajiuliza, Watanzania tumelogwa na hawa watengeneza magari haya hata tujione lazima tununue magari ya anasa (kama haya magari madogo), au tuna biashara nyingi hata tununue magari ya mizigo makubwa makubwa haya tusombee mizigo yetu kutoka bandarini kuwapelekea majirani zetu huko Ruanda, Burundi na Jamhuri ya Kongo au Zambia? Mawazo namna hii ndiyo yanayosababisha wananchi tujiulize sisi ni nchi tajiri au sisi tu malofa?


 Zipo kumbukumbu za maangalizo alizotuachia Baba wa Taifa tangu mwaka 1966 pale alipolionya Taifa hili kutofuja rasilimali za nchi hii. Kwanza alitaka Taifa lilenge kwenye maisha ya Ujamaa. Pili alionya Taifa lisijitumbukize kwenye ulevi au ugonjwa wa maisha ya anasa.
  Haya alionya kwa kufahamu kuwa baada ya Uhuru, wale viongozi waliopigania Uhuru wengetarajia kufaidi jasho lao kwa kuwa kama mabwana (Wazungu wakoloni wale) tuliowaondoa. Ilitazamiwa kuwa ni wakati wa kufaidi maisha. Dalili za hali hiyo zilianza kuonekana tangu mwaka ule wa 1963 pale viongozi walipokionesha mbwembwe za kutawala.


 Viongozi wa chama tawala na Serikali, wakati huo wakijitafutia utukufu! Naita utukufu kwa makusudi maana ulifika wakati kila Mkuu wa Wilaya, Mkoa, Waziri alidai atambulike kuwa amekalia kiti cha utawala na sharti watu watambue hivyo.
 Mwalimu kwa kuhofia hali hiyo ingekuja kuzua balaa la matabaka miongoni mwa watawala na watawaliwa, na kwa kile kiona mbali chake katika maisha ya watu wote, alilazimika kutoa mwongozo kukomesha hali namna ile.


  Narejea maneno yake yalikuwa haya nanukuu, “…. I was obliged to speak publicly against something which I have been complaining about for some time: that is the growing tendency within the government to confuse dignity with what I consider to be sheer pomposity” yaani nililazimika kutamka hadharani juu ya kile nilichokuwa nakilalamikia kwa muda: nacho ni ile tabia au mwelekeo katika Serikali unaojitokeza wa kuchanganya HADHI na MBWEMBWE tupu.


  Akaendelea kuelezea HADHI YA JAMHURI na heshima kwa Serikali ya Jamhuri vitofautishwe. Kwa maneno yake kwa Kiingereza alisema hivi: This is a tendency which must be checked at once if it is not to destroy the very thing, it is, presumably intended to emphasize – the dignity of the Republic and the respect due to the government of the Republic.
 Ndipo Mwalimu alipoyataja baadhi ya matendo yale ya mbwembwe katika mwongozo wake ule. Matendo kama yale ya viongozi kudai waimbiwe wimbo wa Taifa kila wafikapo katika vikao au mikutano ya hadhara, jingine ni kudai misafara yao iongozwe na polisi kwa mapikipiki na magari. Hapo Mwalimu alikomesha hiyo tabia ya kudai heshima na utukufu na namna hii.


 Akaendelea kusema kuwa viongozi wasijidanganye kwa mbwembwe hizo. Huo siyo mtindo wa demokrasia bali ni unyanyasaji. Ndipo akamalizia mwongozo wake ule kwa yale maneno makali kusema, “TUACHE tabia hii mara moja “this is a tendency which must be checked at once…” na mbwembwe zikemewe kwa nguvu zote. Hadhi haihitaji mbwembwe lakini mbwembwe ya aina yoyote ile ni utovu, basi ni wajibu wetu viongozi kuikomesha (Nyerere: Uhuru na Umoja – Kichwa “Pomposity” hotuba ya tarehe 07/07/1963) tabia hii ya mbwembwe.
 Jambo jingine Baba wa Taifa alilolizuia tangu mwanzoni mwa Uhuru lilikuwa matumizi ya magari ya kifahari katika Taifa letu changa na fukara. Kwa hili Mwalimu alikuwa mkali kweli na akatumia neno “FRUGALITY” yaani UBADHIRIFU.


 Hapa Mwalimu aliongelea ubadhirifu katika kutumia magari yaliyoko nchini kwa faida yetu sote. Alitolea mfano wa Uchina alikozuru mwaka ule 1965 akaona namna watumishi wa Serikali na mashirka ya umma wanavyotumia mabasi au magari ya umma pamoja kwenda na kurudi kutoka kazini. Akaomba Watanganyika tujenge tabia ya ubadhirifu katika usafiri wetu hapa nchini. Kule nchini Uchina magari binafsi wakati ule yalikuwa machache kweli. Njia kuu ya usafiri mijini ilikuwa ni kwa mabasi ya makampuni ya umma.
 Kuanzia enzi za ukoloni hapa nchini kama baadhi ya wazee wanavyoweza kukumbuka, tulikuwa na mabasi ya kampuni ya DMT (Dar es Salaam Motor Transport), sijui kama wengine waliyaona haya. Baba wa Taifa miaka ile ya 1967 akaleta mabasi yakiitwa IKARUS (kumbakumba), haya yalienea mji mzima na watu tukawa tunakwenda kwa hayo mabasi ya umma bila taabu. Kulikuwa na kampuni ya usafirishaji hapa ya Dar es Salaam iliyomiliki mabasi yale.


 Kabla ya Uhuru hapa Dar es Salaam, yalikuwapo hata mabasi ya ghoroka kama yale ya kule London, Uingereza, yakitumika katika barabara ya Uhuru kutoka katikati ya mji mpaka Ilala. Usafiri ule wa umma ulizoeleka na watu hatukuchelewa kufika makazini.
 Ningali nakumbuka wakoloni wakati ule katika kutangaza magari yao hapa Tanganyika, waliandika kipeperushi katika yale mabasi yote kilichosomeka “GO BUY BUS OR BUY FORD” yaani safiri kwa basi au nunua gari aina ya Ford utumie! Nani enzi hizo aliweza kununua hiyo motokari ya aina ya Ford? Ni Wazungu na Wahindi tu. Sisi Waafrika tulitumia mabasi tu.


 Mwalimu kwa kuwahimiza wananchi kutokulimbukia magari ya fahari katika nchi fukara hii, alisema hivi: Namnukuu “….the Chinese government is one of those which is making money and technicians available to Tanzania to help us with our Development Plan. But they are able to do this only because they are frugal people; they husband their resources very carefully indeed and only spend money on things which are absolutely essential….” (Nyerere: UHURU NA UMOJA uk. 332).


Kwa tafsiri yangu ya maneno hayo ya Mwalimu ningesema hivi: Serikali ya Uchina ni moja ya wale wanaotoa fedha na wataalamu wao kuja kutusaidia katika mpango wetu wa maendeleo. Haya wanayaweza tu kwa sababu ni watu wabadhirifu sana. Wanatumia rasilimali zao kwa uangalifu sana, wanatumia fedha zao kwa mambo muhimu tu.
 Sasa mtu ukitafakari maneno haya ya Mwalimu, unajiuliza sisi Watanzania wa leo tunayafuata maongozi haya? Kweli fedha zetu kitaifa zinatumika kwa mambo yale yenye kipaumbele cha mahitaji ya Taifa letu? Kama tungefuata maelekezo namna ile siamini kama nchi hii ingekuwa na magari namna hii. Wachumi wangeshauri vilivyo, nadhani matrekta na pembejeo vingepewa kipaumbele cha kwanza katika kukuza uchumi wetu, sidhani kama wachumi wazalendo wangeshauri Serikali ikopeshe wafanyakazi wake magari ya anasa namna hii.


 Miaka ile ya 1960-1975, mazao ya nchi hii yaliongezeka sana. Tukawa na viwanda vya nguo kama Urafiki, Mwatex, Mutex na Sungura, tukawa na viwanda vya korosho Mtwara, Lindi, Tunduru hapa Dar es Salaam, kile cha Kibaha na cha Mbagala. Sasa majengo yote haya ni “MAGOFU” (Waingereza waliita white elephants) yanatusimanga. Je, hapo uchumi wetu umekua? Wachumi tusaidieni kutuelimisha katika hali hii. Kwa nini imetokea hali kama hii hapa nchini?


 Siyo kwa upande wa kilimo tu tulikoporomoka, lakini mimi naona tumejiingiza sana katika anasa na starehe. Tunapenda kuwa na TV kubwa kubwa, vipando vya kifahari (mashangingi) na Serikali imerahisisha upatikanaji wa hizo anasa kwa kuwezesha kimikopo wafanyakazi wanunue magari na hizo TV. Lakini cha kujiuliza; ni kweli kila mfanyakazi anahitaji kuwa na gari lake ndipo amudu vyema hiyo kazi yake?

>>ITAENDELEA

2624 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!