*Sasa aanza kutumbua mawakala wa ushuru
*MaxMalipo na wenzake awapeperushia njiwa
 
NA MICHAEL SARUNGI
 
Baada ya kuwanyoosha watumishi wa umma wa Serikali Kuu, Rais John Magufuli sasa ameingia kwenye “ushoroba” wa wazabuni, ambao wamekuwa wakipata malipo yasiyolinga na kazi wanayofanya, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.
Fagio la Rais Magufuli sasa limeanza kuzikumba kampuni zilizokuwa zinatoa huduma ya kukusanya ushuru na mapato kwa ajili ya Jeshi la Polisi (makosa ya barabarani), ushuru wa maegesho katika majiji na miji mbalimbali nchini na uuzaji wa huduma za jamii kama maji na umeme.
Imebainika kuwa mawakala hawa wamekuwa wakipata hadi asilimia 7 ya makusanyo ya mauzo yote yanayotokana na uwekezaji uliofanywa na Serikali, wakati kuna uwezekano wa huduma hizo kuuzwa kupitia simu za mkononi bila malipo yoyote, hali iliyolitia taifa hasara kubwa hadi sasa.
Akizungumza katika mahojiano maalum na JAMHURI, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka Jijini Dar es Salaam (DAWASCO), Cyprian Luhemeja amesema DAWASCO imebakiza miezi miwili kumaliza mkataba wake na kampuni ya Maxmalipo na haina mpango wa kuongeza mkataba mwingine.
“Mkataba utakapomalizika hatuna mpango wa kuingia mkataba mwingine na Maxmalipo. Kama taasisi tunaagalia namna nzuri na rahisi ya kuweza kuwapa huduma wateja wetu bila matatizo” amesema Luhemeja.
Amesema alipoingia madarakani miaka miwili iliyopita alikuta DAWASCO inatozwa asilimia 7 na kampuni ya Maxmalipo kama tozo ya huduma inayotolewa na kampuni hiyo, ila yeye akapendekeza mkataba upitiwe upya.
“Tuliwaeleza Maxmalipo wapunguze tozo baada ya kubaini kuwa kulikuwa na matatizo kwenye mkataba wa awali ambao Dawasco walikuwa hawapati huduma sahihi kulingana na gharama walizokuwa anatozwa,” anasema.
Amesema baada ya mabishano ya kisheria ya muda mrefu hatimaye pande zote zilifikia makubaliano ya kupunguza asilimia ya tozo kutoka 7 hadi 4, hali iliyosaidia kuokoa mamilio ya fedha za serikali.
“Ni kweli mara baada ya kuupitia mkataba kwa kushirikiana na mwanasheria wa kampuni tuligundua baadhi ya mapungufu hali iliyopelekea kuwaita wahusika na kukaanao mezani na kuafikiana wapunguze tozo yao,” amesema Luhemeja.
Amesema nia na madhumuni ya taasisi ni kuongeza upatikanaji wa huduma ya majisafi kutoka asilimia 67 hadi zaidi ya asilimia 90, ifikapo mwaka 2020.
 
Amesema lengo na madhumuni ya DAWASCO kwa sasa ni kuhakikisha inatoa huduma stahiki kwa wateja wake kwa kuhakikisha huduma zinawafikia kwa wakati na kwa bei nafuu.
Amesema kuongezeka kwa uzalishaji wa maji kutaongeza idadi ya wateja kwani maji yataongezeka kutoka lita za ujazo milioni 160 kwa siku hadi kufikia lita za ujazo milioni 271 kwa siku ambazo ni sawa na asilimia 100.37 ya lengo la upatikanaji wa maji kwa kiwango cha sasa cha lita milioni 270 kwa siku.
Amesema vizimba 560 (gati za kuuzia maji) vimeunganishwa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi ikiwa ni mwendelezo wa kuongeza kasi ya usambazaji na upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni MaxMalipo Juma Rajabu amesema  kampuni yake inapitia wakati mgumu kutokana na baadhi ya kampuni za Serikali kusitisha mikataba nao.
Amesema  miaka ya karibuni kumeibuka na matabaka ya watu wasio heshimu juhudi zinazofanywa na wazawa wenye nia ya kusaidiana kimaisha na Watanzania wenzao.
Mkurugenzi huyo amesema watu hao kazi yao kila mara ni kubeza mambo mazuri yanayofanywa na Watanzania wazalendo na wamekuwa wakishirikiana na  wawekezaji wa nje kuwakandamiza wazawa wanaojaribu kubuni miradi ya kujikwamua.
“Kampuni yetu ni ya kizalendo iliyoanzishwa na Watanzania na kufanikiwa kutoa ajira kwa watu zaidi ya 800 ndani na nje, endapo hali hiyo ikitokea  kuna watu wengi sana watarudi vijiweni,” amesema Rajabu.
Amesema hata Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli imeahidi kuwasaidia na kuwaunga mkono wawekezaji wote wa ndani, lakini inashangaza kuona baadhi ya watendaji wamegeuka kuwa mawakala wa wageni.
Amesema Tanzania ni nchi yenye utajiri wa rasilimali, fursa ya masoko, nguvukazi na mazingira mazuri ya uwekezaji, hivyo ni wakati mwafaka kwa Watanzania kuamka kutoka usingizini kuchangamkia fursa.
“Mchango wetu kama taifa kiuchumi duniani bado uko chini ya asilimia tano, ili tuweze kufikia malengo ya kukua kiuchumi. Ni lazima tujiulize kwa nini bado tupo kuliko wengine, halafu tuanze kujitathmini wenyewe,” amesema Rajabu.
Amesema kuendelea  kutoa kipaumbele kwa wawekezaji wa nje, hakuwezi kuwa na faida kwetu zaidi ya hasara na kushuhudia Watanzania walio wengi wakiendelea kuwa masikini.
 Amesema kampuni yake pamoja na kupigwa vita na washindani wao kibiashara, lakini ni moja ya kampuni ambazo tayari zimekamilisha taratibu za kujiunga na soko la hisa nchini.
Amesema tarehe 5 Mei 2017 Maxcom kwa kushirikiana na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ilizindua mfumo wa mauzo na manunuzi ya hisa kwa njia ya mtandao wa intaneti.
Katika uzinduzi huo Maxcom Africa ambao ni wavumbuzi wa mfumo huu walibainisha kuwa mtumiaji yeyote anaweza kununua hisa na kulipia kwa njia  ya mitandao ya simu iliyopo Tanzania na kadi za benki (Visa au Master Card).
Amesema hatua hiyo ilidhihirisha kuwa kampuni hiyo ni miongoni mwa kampuni za kizalendo nchini zinazoendesha shughulizake kihalali kwa kulipa kodi za serikali.
“Umefika wakati kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kuvipenda na kuviheshimu vya kwetu kuliko kuendelea kujengeana chuki sisi wenyewe kwa wenyewe bila ya sababu,” amesema Rajabu.
Ameongeza kuwa DAWASCO iliingia mkataba na Maxmalipo miaka miwili iliyopita kabla ya Serikali mwaka huu kuingia madarakani na nia ya kubadili mfumo kwa taasisi zake namna ya kufanya malipo.
Amesema serikali imekuja na mpango mahususi wa kuanzisha mfumo uitwayo Government Payments Platfom (GPP) ili kuhakikisha inadhibiti mapato yake kwa kuziamuru taasisi zote zilizokuwa zinahusika na ukusanyaji wa mapato kuwajibika moja kwa moja kwa Wizara ya Fedha na Mipango.
Kutokana na mfumo huo, kampuni zinazotoa huduma ya uwakala kwa kukusanya ushuru na mapato mbalimbali ya Serikali wanapaswa kuingia mkataba moja kwa moja na Wizara ya Fedha badala ya taasisi za serikali kama ilivyokuwa awali.
Kutokana na maagizo hayo, taasisi zote za serikali zitalazimika kusitisha mikataba kuendana na mfumo mpya huo wa serikali unaolenga kuimarisha upatikanaji wa mapato ya serikali.
“Tulikuwa na mtindo wa kulipa ‘Commission’ badala ya kulipa kwa gharama ambazo ni ‘fixed’ kwa sababu ya kufidia gharama za uendeshaji kwa kuwalipa wafanyakazi waliokuwa wanatumika baada ya kufanya kazi,” amesema Rajabu.
Amesema hakuna kampuni yoyote ya kibiashara inayoweza kuukwepa mtindo huo vinginevyo inaweza kujikuta ikifunga ofisi kwa kipindi cha miezi mitatu ya kufanya biashara hii inatokana na kushindwa kulipa wafanyakazi na gharama nyingine za ofisi.
Ameongeza kuwa katika kipindi chote cha mkataba kati ya kampuni yake ya MaxMalipo na taasisi za Serikali kwa mfano DAWASCO waliiwezesha kampuni hiyo kuongeza mapato yake, kusogeza huduma karibu na wateja na kupunguza usumbufu kwao.
“Kama utakumbuka miaka ya nyuma kabla hatujaanza kutoa huduma zetu katika makampuni mengi ya Serikali watu walivyokuwa wakihangaika kupanga foleni kupata huduma mbalimbali nchi nzima lakini baada ya sisi kuingia kila kitu kimebadilika,” amesema Rajabu. 

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Ugavi Umeme (Tanesco), Dk. Tito Mwinuka, amesema suala la shirika hilo kuendelea ama kutoendelea na mkataba na Maxmalipo litatolewa ufafanuzi wakati mwafaka ukifika.

JESHI LA POLISI
Jeshi la Polisi ni miongoni mwa taasisi za serikali ambazo ziliingia mkataba na makampuni kwa ajili kukusanya matapo kwa nja ya mtandao.
Msemaji wa Jeshi la polisi nchini Barnabasi Mwakalukwa amesema suala la mikataba ni la hiari kwa pande mbili husika na kama upande mmoja haukubaliani na mwingine una hiyari ya kuamua kuendelea au kujitoa.
“Nikweli Jeshi la Polisi ilikuwa na mkataba na MaxMalipo kwa kipindi cha miaka miwili, lakini ni hiyari ya uongozi kuangalia je, katika kipindi cha mkataba limenufaika kwa kiwango cha kutosha au la,” amesema Mwakalukwa.
Amesema kuna mikataba na taasisi mbalimbali nchini na mara nyingi kila mwisho wa kila mkataba huwa wanasheria wake wanakaa chini na kufanya tathmini kama kuna haja ya kuendelea au la.
Ameongeza kuwa kimsingi hakuna sheria inayomlazimisha mtu kuendelea na mkataba pale anapogundua upungufu mkataba unapokuwa umefikia kikomo.
“Kama wanasheria watajiridhisha na utendaji wa Maxmalipo watarejea katika meza ya mazungumzo na kampuni husika kusaini mkataba mwingine,” amesema Mwakalukwa.
Habari za kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zinaonyesha kuwa sakata hili la MaxMalipo limewagharibu nafasi zao za kiutendaji, ambapo wengine wamehamishwa kwa kunyang’anywa nafasi za kitaifa na kupelekwa mikoani.
Habari zinasema Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro alipoteuliwa tu ndani ya wiki ya kwanza akasema kuna harufu kubwa ya ufisadi katika faini zinazotozwa na polisi kwa wenye magari na madereva kwa kutumia mawakala.
Kunaelezwa kuwa wakati Polisi wamekuwa wakitangaza kupata Sh bilioni moja kwa mwezi wakati mwingine, kiwango kama hicho au zaidi kimekuwa kikiishia mikononi mwa watu wasio waaminifu.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa E-government, Dk. Jabir Bakari amesema idara yake inasimamia uhakiki wa mifumo yote iliyowekwa kwa mujibu wa sheria za nchi kama inatumika ipasavyo.
Amesema kitengo hicho cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kina lengo la kutoa huduma za kitaalamu juu ya matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano hapa nchini kwa kuzingatia weledi wa kisheria.
“Kwa ujumla kazi ya kitengo hiki ni kusimamia uhakiki wa mifumo yote iliyowekwa kwa kufuata sheria na taratibu za nchi na wale wote wanaoitumia bila ya kuipindisha kwa makusudi,” amesema Bakari.
Amesema kama kuna malalamiko yanayotokana na makubaliano ya makampuni au taasisi zinazohusiana na masuala ya fedha wenye mamlaka ya kuyazungumzia ni Wizara ya Fedha na si kwingine.
Mkurugenzi huyo amesema kazi yao nyingine ni kutayarisha mpango mkakati  kuhusu Teknolojia ya habari na Mawasiliano, Miongozo na taratibu kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na si vingine.
2791 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!