Mahakama ya Kadhi fupa gumu bungeni

Kabla ya kuwasilishwa bungeni Aprili mosi, mwaka huu muswada wa Mahakama ya Kadhi, ulipata ugumu wa aina yake kwenye semina ya wa wabunge iliyolenga kuwaongezea ufahamu juu ya uanzishwaji wa mahakama hiyo.
 Hata hivyo, kile kilichotokea kwenye semina hiyo iliyofanyika Ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma, ilitosha mamlaka husika kuondoa muswaada bungeni. Semina hiyo iliandaliwa na Wizara ya Katiba na Sheria.
Mambo yalikuwaje, gazeti hili linakuletea mtiririko wa matukio yaliyojiri katika semina hiyo aliyokuwa na vitimbwi vya hapa na pale.


 Mwenyekiti wa Semina hiyo alikuwa ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, ilhali mgeni rasmi alikuwa Wairi Mkuu, Mizengo Pinda.
  Mtoa mada alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Robert Mkaramba, aliyeambatana na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, Naibu wake Ummy Mwalimu na Katibu Mkuu, Maimuna Tarishi.
Ngeleja: Tutambue na kumpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa hotuba yake aliyoitoa Machi 28,  mwaka huu iliyozungumzia Mahakama ya kadhi.


  Mara, James Mbatia anaingilia: Mwenyekiti nina ombi; jambo linalojadiliwa ni muhimu kwa Taifa linaleta wasiwasi na hofu kubwa kwa jamii, ushauri wangu ni kuwa, tuzungumze sisi wenyewe ndani kwa ndani bila kushirikisha vyombo vya habari, ni vyema waandishi wa habari wakatupisha.
Mhandisi Athumani Mfutakamba: Naunga mkono hoja ya Mbatia kwa asilimia 100.
 Dk. Pudenciana Kikwembe: Hii sio siri kama vyombo vya habari havitokuwepo nami natoka nje.


Marry Chatanda: Naunga mkono hoja ya Mbatia, pia ni vyema tukafunga na mitandao ya simu.
Murtaza Mangungu: Mmoja kati ya watu ninaowaheshimu ni Mbatia, waandishi wa habari ni waelewa, ni vyema wawepo wasikie ili wasiseme tumejifungia. Waandishi wabakie waandike kile kilichozungumzwa.
George Masaju (Mwanasheria Mkuu wa Serikali-AG): Semina hii ni mahususi kwa uelewa wa muswada uliopo mbele yetu, wananchi hatuwezi kuwapigia simu kuwaeleza, waandishi wa habari wabaki wafanye kazi yao.
Ngeleja: Hatujavunja Katiba, tuvumiliane hili jambo ni la kwetu sote.


Sabreena Sungura: Uvumilivu unaweza kupotea hii yote ni kutokana na kauli zinazotoka huku nyuma.
Dk. Migiro: We may have different religions and colour but, ningependa kutoa rai kwenu kuwa kutumbuke sote ni watoto wa taifa hili watoto wa Tanzania.


Waziri Mkuu Pinda: Wote najua mnajua tumekutana kwa nini, jambo hili liliibuka katika Bunge la Katiba. Leo tuko hapa, lakini kabla suala hili halijawasilishwa hapa tumekuwa na juhudi ili kuelimisha jamii, tuliweza kukutaka pale Julius Nyerere na hata White Sands. Nimekuwana na masheikh na maaskofu, katika juhudi zangu za kuelimishana.
 Rais Kikwete katika mkutano ulioutisha akiwa na Kamati ya Amani alitoa msimamo, matarajio ni kuboresha muswada kwa taratibu tunaziamini zinaweza kusaidia.
 Mambo yaliyoonyesha kutoeleweka kwa jambo lenyewe au kupotoshwa ni kama ifuatavyo;


    1.    Je, Serikali inaanzisha Mahakama ya Kadhi? – Hapana haianzishwi na Serikali kama wengi tunavyofikiria, mahakama hizi zipo tangu mwaka 2012 na zinafanyakazi.
    2.    Serikali kuiweka katika Katiba inayopendekezwa?- Sasa tunasubiri kura ya maoni hilo jambo halipo, kuna hisia Serikali kufanya ujanja jambo hili kuliweka katika katiba.


    3.    Je, maeneo gani mahakama itashughulika nayo?- Nilipokuwa katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere baadhi ya wachungaji waliuliza kama mahakama hii itasikiliza kesi za jinai, hapana katika utekelezaji wa majukumu yao ni ndoa, talaka, mirathi na wakfu tu.
    4.    Itagharamiwa na nani?- Mahakama hizi zitagharamikiwa na wao wenyewe, hakuna mkono wa serikali wa uwezeshwaji.


    5.    Je, tunavunja katiba? Bahati nzuri Ndassa amelieleza hilo, katiba ile isome na ibara ya 3 ukisoma ibara ya 19 (i,ii) huu ndio msingi wa Serikali katika masuala ya kijamii.
Lakini pamoja na utambuzi huo jambo hili limeibua hisia mfano mzuri ni Mchungaji Gwajima alipokuwa anaeleza jambo hili. Mahakama ya kadhi inavyoeleweka kidogo inaleta taabu, basi tuone tunalipelekaje mbele kwa manufaa ya wote maana wakati mbwingine linavuta hisia sana.
Jaji Makaramba: Ninasimama hapa kwa nafasi yangu binafsi sio kama Jaji wa Mahakama Kuu nchini. Nafasi ya matumizi ya sheria za dini nchini, nchi yetu ina dola isiyo na dini.


Tanzania ni nchi ya Mungu sio taifa la Mungu, nchi ya Mungu ni Israel. Viapo vya viongozi vinamtaja Mungu, Serikali za wanadamu zinaundwa na wanadamu sio Mungu. Katiba Inayopendekezwa imefafanua vizuri kifungu hiki, serikali haiwezi kuwa na dini sababu sio wanadamu. Seikali inalinda imani za wanadamu dola isiyofungamana.


    1.    Inahusu masuala binafsi tu
    2.    Kukatana mikono na kupigana mawe haipo kwenye Quran tukufu
    3.    Ndoa, talaka, mirathi na wakfu hayo ni masuala binafsi
    4.    Shetia iliyokuwa inasimamia masuala ya kiislam ilipitishwa na kutumika bila idhini ya bunge pia kuna sheria zilifutwa bila idhini ya bunge.
    5.    Uhuru wa kuabudu umefafanuliwa na katiba pendekezwa, ukikashifu dini ya mwenzio umevunja katiba, chuki za kidini ni ukiukwaji wa katiba, chuki za kidini zimesababisha mapigano.

Mimi sipigi kampeni hapa, hazinihusu. Mkishapiga kampeni mtaniletea tu.
AG Masaju: Katika sheria hii mabadiliko kifungu cha 3 wanazuoni walikubaliana ni sheria zipi zitumike. Tunaleta marekebisho hayo hizi mahakama zilizokwishaanzishwa ziweze kutumika, haihusiani na masuala ya jinai. Waziri wa sheria atatengeneza kanuni namna mahakama itajiendesha na kujigharamia, serikali haitoweka mkono wake, watakaokwenda kule ni wale watakaoenda kwa utashi wao wenyewe.


Kadhi ni mtu aliyefanya kazi chini ya Chifu Kadhi atakayeteuliwa na Mufti.
Deogratias Ntukamazina: Wadau walipoitwa walikuja makundi mawili moja kundi la Bwakata, pili makundi 11 yasiyokubalina na Bakwata.
Walikataa kuletwa bungeni bila wao waislam kufikia maridhiano, sababu wahamtambui Mufti kuwa na majukumu makubwa.


Makundi yote mawili walimpinga Jaji Makaramba katika yote aliyoyasema Jaji. Former Justice wa Kenya alipokuja alitwambia tusifuate mfumo wa Kenya. Maaskofu walisema tuendelee kuheshimu waasisi wa taifa, walituachia nchi isiyo na dini.
 
Anne Makinda (Spika wa Bunge ): Kwa heshima zote za kibinadamu, kimaumbile tuheshimiane, tabia zetu si sifa hata kwa Mungu, tumuogope Mungu.
 
Rukia Kassim: Serikali kuwalazimisha watu kupitia Bakwata sio sahihi, Waziri Mkuu anajua hasa suluhisho la tatizo hili. Pinda ndiye chanzo cha matatizo yote anachonganisha waislam, huu muswada hatuukubali.
 
Moses Machali: Dini ni watu na maisha ya watu, unapozungumzia masuala ya kidini unazungumzia imani za watu. Suala la Mahakama ya Kadhi linakinzana na ibara ya 19 ya katiba ya nchi. Ukiangalia muswada na Rukia ametudokezea kuwa ndani ya waislam kuna mgawanyiko, serikali inaleta kitu ambacho hawajaridhia tunawakosea waislam.
Alileta suala hili kwa malengo yake binafsi, suala hili likiingizwa bungeni nasi mnataka tulete dhehebu moja moja kuleta madai ya mahakama za dini zao. Tunahatarisha nchi yetu, hili suala lisije ndani ya bunge.
Nyambari Nyangwine: Walikuja Masheikh na taasisi 11 wote walikataa, Masheikh walilalamikia kutengwa na Bakwata, wana chuki kubwa, ni lazima utafiti na elimu itolewe kwa wadau. Mimi ni mpagani ikitokea siku moja nikaleta hoja ya kupitisha mahakama yetu ya kipagani mtakubali?
 
Joseph Selasini: Kama tusipoangalia tunakwenda kuvunja umoja na amani ya nchi. Sitaki kuwa mmoja wapo, nchi yetu inavunjwa, tunafanya mchezo wa kutoa jini kwenye chupa.
Maaskofu na wachungaji wanatoa kauli hamsikii, kwanini Serikali haikai na viongozi hawa? Serikali inawatumia waislam kutafuta kura, inawakosea waislam, haiwatendei haki. Wakristo wana hofu, kuna tishio la baadhi ya wananchi kuleta udini nchini, interjensia iki kimya, acheni kutoa jinni katika chupa lililofungwa na Nyerere na Karume.
Marry Mwanjelwa: Sio siri maaskofu na wachungaji wanasema hili ni jambo ni hatari litaligharimu taifa, Nyerere na Karume waliliona. Hili jambo lisiingie bungeni, hekima na busara zitumike nchi inakwenda kuvunjika vipande vipande, utulivu sasa haupo umeshatoweka.
Khalifa Suleiman Khalifa: Katika sura ya 4 aya ya 38 surat Maida hiyo ndiyo aya iliyosema watu wakatwe mikoni. Ni wazi kufuatia mazingira tunaelekea pabaya, Serikali haikujipanga kuleta Mahakama ya Kadhi, kama kweli wana lengo kama walivyoahidi wakati wanaomba kura.


Huu ni unafki, na Mungu hapendi wanafki, Waziri Mkuu Pinda anasema mahakama hiyo ipo tangu mwaka 2012 sasa mnaleta ya nini? Nchi zote zina Mahakama za Kadhi hakuna mtu aliyekatwa mkono, ni wazi kuwa muswada huu haujaiva msiulete bungeni. Tusilete hili jambo tutawanyike tukafanye mambo mengine.
David Silinde: Kwa hili la sasa Pinda umechemka, yaani umechemsha. Nalisema hili kwa sababu ndiye aliahidi kulileta bungeni. Suala la imani, sio siasa hii, imani, kumuaminisha mtu jambo jingine haiwezekani. Nchi mnataka kuipeleka pabaya, inawezekana huu ni mwisho wa CCM. Suala la imani limevuka mipaka ya vyama, msituchezee, rais alishasema kuwa waislam wenyewe wataanzisha Mahakama ya Kadhi.
 
Seleman Jafo: Hili jambo halihitaji ushabiki, Tanzania haina watu wa matabaka, daraja la kwanza na daraja la pili. Muswada unazungumziahaki ya makundi husika, tusifanye masihara muswada huu usiingie bungeni. Watu wamekaa vikao kufanya uamuzi katika muswada huu, naitahadharisha serikali  katika muswada huu.
Saa 7:17 ziliibuka vurugu kiasi cha wabunge kutaka kupigana, Waziri Mkuu akatoka nje na kuanza kufanya mawasiliano huku wabunge wakitukanana na kurushiana vijembe kwa dakika 20 kila kitu kilisimama.
 
Spika Makinda: Usikivu na busara ni muhimu tuheshimiane.
Haji Juma Sereweji: Zanzibar ipo mahakama ya kadhi toka enzi za mkoloni. Karume aliikubali mahakama ya kadhi, nasikitishwa na kamati ya sheria wanasema sijui nani kakataa. Nimemsikiliza rais Kikwete, amesema serikali haitijihusisha ma mahakama ya kadhi, sio kuwa haitaki. Muswada huu uletwe bungeni tusiwasikilize waliotoka bungeni.


Mch. Luckson Mwanjale: Juzi nilikuwa na mkutano na wachungaji 150 waliukataa muswada huu, presha ni kubwa mno, tukichukulia hivi tutaumia sana. Serikali haikutoa elimu ya kutosha kwa wadau, suala hili lingetulia kwanza, mahakama ya kadhi ni suala kubwa lenye mambo mengi yanayotisha mnaleta jambo moja tu.
Haiwezekani naiomba serikali iangalie, mwingine anasema waislamu tukutane, mwingine wakristo tukutane, tunaipasua nchi. Hili suala nila imani, linamgusa mtu mmoj mmoja, serikali ihusike kutoa elimu, kikao hatuwezi kuendelea nacho bora tumalize.


Mangungu: Nimekuwa nikishirikiana na wenzangu wa dini nyinyine. Humu ndani wapo wanafiki na leo wamebainika, kwa kuwa wamejijenga kwenye imani yao ya kinafiki ndiyo hao unaowasikia wanapayuka huko nyuma. Haitofika wakati Waislamu kukaa na kukubaliana, mimi mwenyewe sikubaliani na Mufti kutuchagulia makadhi.
 
Hasnain Murji: Mangungu ni muislam anavaa kanzu lakini haendi kuswali, sio kweli kuwa hatuelewani.
Saa 8:38 Askari polisi waingizwa katika ukumbi wa semina. Majadiliano yaliendelea kwa utulivu na amani, huku baadhi ya wabunge wakitoka ndani ya ukumbi wa semina, ilipotimu saa tisa na robo (15:15) Waziri Mkuu alitoka tena nje ya ukumbi na kuongea na simu kwa muda mrefu kisha kurudi ukumbini.
Mhandisi Hamad Masauni: Maamuzi yote tutakayoyatoa ni vyema tukazingatia amani ya nchi. Naona kuna watu wanaliingiza katika vyama wanadhani wakilipinga wataikomoa CCM na Waziri Mkuu Pinda.


Kuna viongozi wa dini wanatumiwa na vyama vya siasa, nani anapinga kwamba waislam wanasemewa na Bakwata, Jaji Robert amezungumza kwa umakini. Tuna dhamana kubwa kulilinda taifa. Tujiulize jambo hili lisipopitishwa Waislam watajisikiaje? Kwani tunaanzisha mahakama ya kadhi hapa? tusifike pahala tukaangalia ushabiki binafsi.
Tundu Lissu: Kama inawezekana naomba nizungumze kwa utaratibu, mjomba wangu ni Sheikh hili jambo haliwahusu Waislamu peke yao. Jaji Makaramba ameletwa hapa hakutwambia kile alichokisema kwenye kamati ya sheria.


Maoni ya Profesa Ibrahim Majamba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Desemba 2010, serikali ipo tayari kusaidia kuudwa kwa Mahakama ya Kadhi, kama vile majengo, mafunzo n.k. Jambo hili limepata Baraka za Rais Kikwete, uongo wa aina hii usisababishe hofu.
Serikali inaleta uongo hapa, maana kwa nyaraka hizi hapa nilizonazo Serikali ndiyo itakayoigharamia Makahama ya Kadhi, pia Jaji hajatwambia ya kuwa yeye ndiye alikuwa akiikataa mahakama hii ya kadhi, leo anakuja hapa kutuletea habari nyingine kabisa.


Ali Kessy: Serikali inataka kuleta fujo nchini, Bakwata wameteua makadhi nchini hawatambuliwi. Nguzo za kiislam zipo tano, hakuna Mahakama ya Kadhi, Bakwata ndiyo wanaoongoza kwa kuuza mali za waislam. Tupo bungeni siku ya Ijumaa hawaendi kuswali, lakini wanakimbilia Mahakama ya Kadhi.
Tofauti ya muislam na kafri ni kuswali, nguzo za Kiislam zinajulikana haipo mahakama ya kadhi. Iwapo mtaleta bungeni mimi ndiyo nitakuwa mtu wa kwanza kuipinga.


Jaji Makaramba: Nashukuru mmenisaidia katika utafiti wangu mgongano wa mawazo ndiyo unaosaidia, yote aliyoyasema Lissu niliyasema wala sipingi na sibadilishi. Sikuja hapa kwa hila yoyote sikutaka kuwatafunieni majibu hiyo ndiyo kazi yangu kama mwalimu na jaji.
Nimepokea ushauri na hatimaye baada ya kutoka hapa nitachukua likizo nikajifunze kama mlivyonitaka.
AG: Kwangu mimi suala la umoja na amani ya taifa ni namba moja, muswada huu hauvunji katiba. Suala nyaraka za Lissu hilo sijui, ila kitakachofanyika ni muswada, Serikali haitagharamia mahakama hii. Nitatumia madaraka yangu.
Pinda: Mambo mengine hamnitendei haki mimi nilichukua msalaba huo nikauleta kwa niaba ya Serikali, mengine niliyoyasikia niseme tu kwamba sijayasikia.