Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameliweka njiapanda Bunge la Jamhuri ya Muungano, baada ya kuwalazimisha wabunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitisha muswada wa Mahakama ya Kadhi.
Mkutano huo ulifanyika katika Ukumbi wa Msekwa Machi 21, mwaka huu. Katika mkutano huo aliwataka wabunge hao kuhakikisha muswada huo wanaupitisha kwa nguvu.


Baadhi ya wabunge waliozungumza na gazeti hili walieleza kukasirishwa na kitendo cha Pinda kuitisha mkutano wa wabunge wa CCM kutaka suala la kuupa nafasi muswada wa Mahakama ya Kadhi.
Taarifa zinasema kwamba mkutano huo uliomalizika saa tatu usiku, ulikuwa na ajenda mbili  ambazo ni mfumo wa upigaji kura za maoni wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu utakaohusisha madiwani, wabunge na rais.
Pia ajenda ya pili ilikuwa ni miswada ambayo imekuwa ikijadiliwa katika Bunge la 19.


Ajenda ya mchakato wa upigaji kura ilijadiliwa na kukubaliana kutumika kwa mfumo wa kuwapo kwa utaratibu wa kuwapa kipaumbele wabunge waliofanya vizuri katika majimbo yao ya uchaguzi, kwa kutimiza Ilani ya CCM na kufanikisha ushindi wa chama katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliomalizika mwishoni mwa mwaka jana.
  “Kuwapo kwa utaratibu wa watu waliofanya vizuri wasiwe na wapinzani ndani ya chama, matokeo katika Serikali za Mitaa, wale waliojitahidi kupigania chama na kutekeleza ilani wathaminiwe na kutiwa moyo,” anasema mmoja wa wabunge waliokuwa ndani ya kikao hicho.


Akaongeza; “Chama tayari kimeanza kutumia watu wake kufuatilia haya tuliyoafikiana ili kuweza kuokoa baadhi ya majimbo, maana bila kufanya hivyo majimbo mengi yatapotea.”
Hata hivyo, katika kikao hicho, Waziri Mkuu Pinda alijikuta katika wakati mgumu pale alipowataka wabunge hao kuhakikisha wanaunga mkono na kupitisha muswada wa Mahakama ya Kadhi unaotarajiwa kusomwa bungeni leo.


Baadhi ya wabunge walipinga kauli hiyo ya Waziri Mkuu huku wakimueleza kuwa kauli yake hiyo inasigana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ambayo inaeleza nchi kutokuwa na dini bali watu wake ndiyo wenye dini, hivyo alikuwa anavunja Katiba.
“Waziri Mkuu anatueleza jambo hilo lisikuzwe maana tayari makadhi wapo, anatutaka kupitisha muswada huo, anatumia nguvu kubwa kutulazimisha kitu ambacho hakiwezekani, ndiyo maana tuliamua kutoka nje kutokana na hii tabia ya kulazimishana mambo ambayo hayawezekani, viongozi wote wanataka jambo hilo lipite nasi hatukubaliani na hilo,” anasema.


Hata hivyo, kikao hicho hakikuhudhuriwa na wabunge wote wa CCM ambapo nusu ya waliohudhuria kikao hicho, walilazimika kutoka nje kutokana na kutokubaliana na kauli ya Waziri Mkuu aliyekuwa mwenyekiti wa kikao.
Pamoja na wabunge hao ‘kumsusia’ Pinda, gazeti hili limedokezwa kuwa muswada huo umepingwa vikali na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ambao hawakubaliani na muswada huo kuingizwa bungeni wakati huu huku ukiwa haujafikishwa katika kamati hiyo.
 Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo waliozungumza na na gazeti hili, wanasema kuwa asilimia 80 ya wajumbe kamati hiyo hawakubaliani na muswada huo kusomwa bungeni kama ulivyopangwa.


“Hili suala ni gumu, lakini Waziri Mkuu analisukuma kwa nguvu lifanyike kwa sababu tu ni ahadi yake ambayo aliitoa wakati wa Bunge la Katiba. Busara ya Serikali  lazima itumike katika kulinda umoja wa kitaifa, ni vyema ikafanya utaratibu wa kuutungia sheria tofauti ndipo uletwe bungeni la sivyo ni kuvunja Katiba ya nchi ambayo tuliapa kuilinda,” anasema mmoja wa wajumbe.
Aidha, wanasema kuwa ni vyema Serikali ikazingatia maoni ya wabunge wengi ambao wamesema ni muhimu viongozi wa madhehebu yote ya dini kukutana na kuridhia jambo hilo kabla halijaletwa bungeni.


Wabunge hawa wanasema kuwa Pinda hakuwa na mamlaka ya kutoa ahadi ya kuletwa muswada huo katika Bunge la Jamhuri kama alivyoahidi hapo awali, kutokana na kutofuata sheria na taratibu zinazohitaji kufuatwa.
“Pinda aliposema kuwa muswada wa Mahakama ya Kadhi utapelekwa bungeni katika Bunge la mwezi wa kwanza, hakuwa na mamlaka hayo kwa sababu hakuwa ameshirikisha Baraza la Mawaziri, hakupata ridhaa ya Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi, hakuwa amemshirikisha Rais Kikwete ili kutoa ahadi hiyo.
“Alikurupuka kutoa ahadi isiyo na mamlaka shirikishi kwa sababu ya Katiba, lazima kila kitu kiende sambamba na utumishi wa maoni ya dhamana ya rais,” anasema mjumbe huyo kwa sharti la kutotajwa jina.


“Wabunge wanaitaka Serikali kutofikisha muswada huo bungeni maana utaweza kusababisha mvutano mkubwa ambao utaligawa Taifa huku ukihofiwa kuhusisha kurushiana kauli ambazo zitakuwa chanzo cha uvunjifu wa amani na utulivu ulipo nchini,” anaongeza.
 Akasisitiza, “Unajua, ni vyema suala hili likaangaliwa kwa makini hasa katika kipindi hiki, tunatambua ya kuwa Waziri Mkuu anatumia turufu hii katika harakati zake za kuusaka urais, lakini hatuwezi kukubaliana na hilo.”


Waziri wa Sera, Uratibu na Bunge, Katibu wa wabunge wa CCM, Jenista Mhagama, akizungumzia suala hilo anasema kuwa  hakuna mbunge yeyote aliyetoka nje katika kikao chao ambaye hakupendezwa na kilichokuwa kikijadiliwa.
Mhagama anasema kuwa kikao hicho kilikuwa cha kawaida na kilichokuwa na ajenda za chama ambazo zilikuwa zimeshajadiliwa katika kikao kilichofanyika Machi 15, mwaka huu kabla ya kuanza kwa Bunge la 19.


“Kikao kilikuwa cha kawaida cha ajenda zetu za chama, kiliisha kwa  ajenda tulizokuwa nazo na kiliisha vyema na ajenda zote. Hiki ni kikao mwendelezo wa kikao kilichotangulia cha Jumapili ya kwanza kabla ya Bunge la 19, ajenda zilikuwa zaidi ya moja… hayo mengine unayosema mimi binafsi siyajui wala sikuyaona,” anasema Mhagama.


Hata hivyo, Ijumaa iliyopita ratiba ya vikao vya Bunge ilibadilishwa na muswada huo wa Mahakama ya Kadhi kuondolewa katika ratiba ya shughuli za Bunge hivyo kutojadiliwa katika Bunge hili.
Muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali ndiyo uliochukua nafasi ya muswada wa Mahakama ya Kadhi. Mabadiliko hayo yanaelezwa kutokana na kikao cha kamati ya uongozi kilichoketi kwa saa tatu Machi 26, mwaka huu.


 Muswada huo umekuwa ukipingwa na kuleta mzozo baina ya wadau ambako wiki mbili zilizopita, Maaskofu wa Jukwaa la Wakristo Tanzania linaloundwa na Taasisi za Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) walitoa tamko.
Maaskofu hao waliokutana Machi 10, mwaka huu walisema kwamba walijadili kwa kina kuhusu hali ya usalama wa nchi ilivyo sasa na mustakabali wake, Katiba Inayopendekezwa na uanzishaji wa Mahakama ya Kadhi.


Baada ya kutafakari yote hayo, Jukwaa limefikia maazimio ya kupinga wakisema, “Kuhusu suala uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi nchini kama tulivyotoa maoni yetu kwa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria (Januari 16, 2015); barua yetu kwa Waziri Mkuu na matamko mbalimbali yaliyokwisha kutolewa kuhusu jambo hili; Mahakama ya Kadhi inakiuka misingi ya Taifa hili kuwa na Serikali isiyokuwa na dini wala mfumo wa sheria unaobagua raia wake kwa misingi ya dini.


“Pia mjadala unaoendelea unavunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 Ibara ya 19. Kwa kuendelea kujadili suala hili katika Ilani za Vyama vya Siasa, Majukwaa ya Kisiasa na Bungeni, limeligawa Taifa letu, Serikali, Bunge, Mahakama na wananchi.


“Mahakama ya Kadhi imekuwa ikiendelea kutumiwa na wanasiasa kama mtaji wao wa kujipatia madaraka kwa gharama za kuleta chuki za kidini. Kwa dhamiri safi, Jukwaa linatamka wazi kuwa mjadala unaoendelea kati ya Serikali na vikundi vya kidini kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi kikatiba na kisheria ufungwe na badala yake ziachiwe taasisi husika za kidini kuamua juu ya masuala hayo bila kuihusisha Serikali wala waumini wa dini nyingine.”

2603 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!