Kutafuta pesa ni mtihani. “Pesa ni kama mgeni; inakuja leo na kuondoka kesho.” (Methali ya Malawi). Namna ya kupata pesa na namna ya kuitumia ni mtihani. “Kutengeneza pesa ni kama kuchimba kwa sindano, kuitumia ni kama kumwaga maji mchangani.” (Methali ya Japan).

Methali hiyo ya Kijapani inabainisha ukweli kuwa pesa inapatikana kwa kutoa jasho. Methali hii inasisitiza umakini katika kutumia pesa. Usiweke pesa mfukoni bila kutazama kama kuna tundu.

Pesa inaweza kukimbia. “Pesa haina masikio lakini inasikia; haina miguu lakini inatembea. Inaweza kutembea na kukuacha.” (Methali ya Japan).  Kutafuta pesa ni mtihani. Unaweza kuiacha ulipo bila kujua kama ipo na ukaenda kuitafuta kwingine.

Katika kitabu cha Russel H. Conwell ‘Acres of Diamonds’, kuna hadithi ya kushangaza. Ali Hafed, tajiri wa Persia ambaye alikuwa ameliridhika kwa utajiri wake mpaka siku aliyojifunza juu ya almasi. Kabla ya hapo alikuwa hajawahi kufikiria juu ya almasi na alikuwa hana taarifa juu yake.

Baada ya kupata taarifa juu ya almasi alianza kuwaza kiasi cha utajiri ambacho almasi itamletea. Hatimaye alitoka nyumbani kwake na kuanza kutafuta almasi. Baada ya kipindi kirefu cha kutafuta almasi alitumia pesa yake yote katika kutafuta almasi.

Aliaga dunia akiwa maskini kwenye fukwe ya rasi ya Barcelona. Huko Persia mtu aliyenunua shamba la Ali Hafed aligundua ‘changarawe’ ya ajabu ambapo Ali Hafed alinywesha ng’ombe wake. Kumbe ‘changarawe’ ilikuwa ni almasi.

Palikuwepo almasi chungu nzima. Ni sehemu hiyo ulizaliwa mgodi wa almasi uitwao Golconda. Vito vingi vya mataji ya vichwa vya watu wa Ulaya vimepatikana katika mgodi huu. Chimba ‘dhahabu’ ulipo. Chimba ‘almasi’ ulipo.

Pesa ni mtihani. Tajiri anapoanguka wanasema ni ajali; maskini anapoanguka wanasema alikuwa amelewa. Maskini haokoti, akiokota huambiwa kaiba. Hakuna amwaminiye maskini hata ikiwa amepata kwa njia halali. Maskini hajui kula na mkwasi (tajiri), akianza kula samaki huanzia kichwani.

Maskini hana miiko. Maskini halali mchana. “Maskini hana muda wa ziada.” (Methali ya Japan). Maskini hapiki kombe la wali mpaka mwaka wa mavuno. Mashua ya maskini huzama mtoni. Mambo ya maskini hayatengemei kutokana na uwezo wake mdogo.

Pesa ni mtihani. Matajari wanawahitaji maskini kuliko maskini wanavyowahitaji matajiri. Maskini anaweza kumhitaji tajiri kwa sababu ya kusaidiwa. Maskini anaweza kupata msaada wa vitu kutoka kwa tajiri. Lakini tajiri anamhitaji maskini kama mteja na kwa sababu za kiroho.

Tajiri mwenye duka kubwa atawahitaji wateja, wengine ni maskini. Tajiri anawahitaji maskini aweze kutimiza wajibu wake wa kiukarimu na matumizi ya mali ya ziada. “Ukitaka kujisikia tajiri hesabu vitu vyote ulivyonavyo ambavyo pesa haiwezi kununua.” (Daniel Webster). Pesa haiwezi kununua ukarimu.

Kutafuta pesa ni mtihani. “Okoa pesa na pesa itakuokoa.” (Methali ya Jamaica). “Fedha ni jibu la kila kitu.”(Mhubiri 10:19. Lakini tusisahau kuwa Mungu ni jibu). Ukibaini ukweli huo lazima kuikoa.  Ili kuokoa pesa unahitaji kuwekeza na kuweka akiba.

“Wekeza tu katika bidhaa unayoielewa, pamoja na watu unaowafahamu na unaweza kuwaamini. Wakati mwingine uwekezaji mzuri ni ule ambao hauufanyi,” alisema Donald Trump katika kitabu chake: “How to Get Rich.” Okoa pesa kwa kuweka akiba.

 Tuwaige wadudu kama chunguchungu ambao huweka akiba. “Chunguchungu – taifa lisilo na nguvu, lakini wakati wa hari hujiwekea chakula.” (Mithali 30:25).

970 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!