Kujikosoa ni mtihani, unapowanyoshea wengine kidole, vitatu vinakuelekea wewe na  kidole gumba kinasema Mungu ni shahidi. Kwa msingi huu kujikosoa ni mtihani.

“Si namna tunavyofanya makosa kunakotutambulisha bali namna tunavyoyasahihisha,” alisema Rachel Wolchin. Kuna kitendawili kisemacho: “Kipo lakini hukioni.” Jibu ni ‘kisogo’.

Kama kisogo kipo lakini hatukioni, kuna makosa yetu yapo lakini hatuyaoni. “Macho yangu nitazame na mimi pia.” Ni methali ya kabila linaloitwa Ovambo.

Kwa muda mwingi tunawatazama wengine bila kujitazama, methali hii inasisitiza kujikosoa. “Si ishara ya udhaifu, bali ni ishara ya ukomavu wa hali ya juu kupanda na kufikia ngazi ya kujikosoa,” alisema Martin Luther King Junior.

Kwa muda mwingi tunawatazama wengine bila kujitazama, tunaita majina ya watu wengine bila kutaja majina yetu. Katika mtazamo huo tunaweza kutaka kuwabadili wengine bila kwanza kubadilika sisi.

Lakini tunakumbushwa na wazee wetu wa zamani kuwa, kabla ya kuwatibu wengine jitibu, hauwezi kumaliza kiu kwa kuwakilishwa. Hakuna anayekunywa dawa kwa niaba ya mgonjwa.

Kuna wanandoa waliohama kutoka Sinza kwenda Mbezi Mwisho. Walipohamia waliweza kuona nguo za jirani zimetundikwa. Walijadili juu ya uchafu wa hizo nguo.

Kila walipokuwa mezani wanapata kifungua kinywa au mlo wa mchana waliongelea nguo za jirani kuwa hazikufuliwa vizuri. Asubuhi moja mwanamke alipochungulia kupitia kioo cha dirisha aliona nguo zimefuliwa na kutakata.

Alimuuliza mume wake: “Vipi, umewashauri kuosha vizuri nguo?” Mume alijibu: “Nimeamka asubuhi na mapema na kuosha dirisha letu lilikuwa chafu.” Nguo hazikuwa chafu, bali dirisha, safisha dirisha lako, safisha mtazamo wako.

Makosa uliyoyafanya yawe somo katika kujikosoa. “Watu wote hufanya makosa, lakini watu wenye busara tu ndio hujifunza kutokana na makosa yao,” alisema Winston Churchill wa Uingereza.

Nilipokuwa darasa la kwanza nilitumia kalamu ya penseli, ilikuwa rahisi ukikosea unafuta. Darasa la tatu mambo hayakuwa rahisi, nilikosea na kujaribu kufuta neno lililoandikwa kwa wino na kutia mate.

Matokeo yake nilitoboa karatasi, mwalimu aliniambia pitisha kalamu mara moja endelea kuandika. Ukijikosoa pitisha kalamu mara moja, omba msamaha kwa Mungu na endelea mbele.

“Unafanya makosa, hayakufanyi,” alisema Maxwell Maltz. Lakini usipojifunza kutokana na makosa, ukayarekebisha, makosa yatakutambulisha wewe ni nani, yatakubainisha wewe ni nani.

“Unapofanya kosa, kuna mambo matatu ambayo lazima ufanye juu ya kosa: likubali, jifunze kutokana na kosa, na usirudie tena,” alisema Paul Bear Bryant.

Nilikutana na baba mmoja aliyekuwa na vidonda viwili kwenye masikio. Nilimuuliza amekuwaje mbona ana vidonda viwili kwenye masikio, aliniambia alikuwa ananyosha nguo wakati amelewa pombe.

Kuna mtu alimpigia simu, badala ya kuchukua simu, alichukua pasi na kuweka kwenye sikio. Nilimuuliza na juu ya sikio la pili vipi? Aliniambia: “Huyo mtu alipiga tena.” Baba huyo hakujifunza kutokana na kosa lake.

Safari ngumu kufanya ni ya kwenda moyoni ili kujikosoa, sauti ya ndani ya kujikosoa usiifunike kwa kujilinganisha na wenye makosa makubwa zaidi yako. Usiifunike kwa kulaumu wengine kama Adamu baada ya kula tunda alivyomlaumu mke wake Eva na Mungu ambaye alikuwa baba mkwe wake.

Kioo hakidanganyi, tunakitumia kurekebisha tulipochafuka usoni. Tuwatumie watu waliofanikiwa maishani kama kioo. Tujirekebishe tunapokosea. Kujikosoa ni mtihani lakini unaweza kuushinda. Lisilowezekana linawezekana.

By Jamhuri