Na Albano Midelo

Uamuzi ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk.John Magufuli, kuzuia uagizaji wa makaa ya mawe toka nje, badala yake watumiaji wote kutumia makaa ya mawe toka mgodi wa Ngaka Wilaya ya Mbinga Mkoa wa Ruvuma, yamesababisha soko la makaa hayo kupanda.

Kaimu Meneja Uzalishaji wa kampuni ya TANCOAL katika mgodi wa Ngaka, Edward Mwanga, ameliambia gazdetin la JAMHURI, mgodi wa Ngaka, unamilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania yenye asilimia 30, na Kampuni ya Intra Energy ya Australia yenye hisa asilimia 70.

Amesema uzalishaji rasmi wa makaa ulianza mwaka 2011 kwa kusuasua kwa sababu kampuni ilikuwa haijajitangaza vya kutosha na ilikuwa katika utafutaji wa kutambua kiwango cha makaa ya mawe yalipo kwenye eneo la Ngaka.

 

“Mwaka 2014 ndipo makaa ya mawe yalianza kufahamika na kutambuliwa hasa kutokana na kuongoza kwa ubora duniani ukilinganisha na makaa mengine hali ambayo ilianza kuleta neema kwa Kampuni baada ya kutambulika vilivyo na kupata msukumo wa kuongeza uzalishaji,” amesema Mwanga.

 

Mwaka 2014 uwezo wa kuzalisha makaa ya mawe wa kampuni hiyo ulikuwa chini kwa sababu wateja walikuwa wachache hali ambayo ilisababisha uzalishaji kuwa kati ya tani 15,000 hadi 20,000 kwa mwezi.

 

Mwanga amesema kampuni hiyo ilikuwa inauza tani zisizozidi 15,000, huku ikitegemea zaidi viwanda vinavyozalisha saruji vilivyopo hapa nchini, hasa baada ya serikali kuzuia uagizaji wa makaa ya mawe toka nje mwanzoni mwaka 2017,ulikuja msukumo wa mahitaji makubwa ya makaa ya mawe.

 

Amesema wateja walikuja kwa kasi na kuhitaji makaa ya mawe toka Ngaka hali iliyosababisha kampuni ya TANCOAL kuongeza mitambo ya kuzalisha ili kuongeza uzalishaji.

 

Kwa mujibu wa Mwanga, katika mwaka wa fedha 2016/2017 uzalishaji wa makaa ya mawe katika mgodi wa Ngaka uliongezeka mara dufu kutoka tani 20,000 hadi 40,000 kwa mwezi na kwamba hadi kufikia Juni 2017 kampuni hiyo iliongeza uzalishaji hadi kufikia tani 100,000 kwa mwezi.

 

Hata hivyo amesema licha ya soko kuongezeka mauzo kwa mwezi ni kati ya tani 40,000 hadi 50,000 na kwamba kampuni hiyo inataraji uhitaji utaongezeka zaidi.

 

Ameyataja malengo ya kampuni hiyo kuwa ni kuongeza uzalishaji zaidi ili kuhakikisha wanatosheleza soko la ndani na nje ya nchi ambapo anawataja wateja wa soko la nje ya nchi kuwa ni nchi za Kenya, Rwanda, Malawi, Madagascar na Uganda.

 

Kuhusu maisha ya wananchi wa eneo lenye rasilimali kunufaika na uwepo wa rasilimali hizo badala ya rasilimali hizo kuwanufaisha zaidi wawekezaji, Kaimu Meneja uzalishaji huyo amesema uwepo wa Mgodi wa Ngaka unavinufaisha vijiji vinavyozunguka mgodi huo.

 

“Hata wakandarasi wetu wapya tumewaelekeza kuchukua wafanyakazi wanaotoka mazingira ya mgodi kulingana na ujuzi walionao na mahitaji, kwa hiyo kwanza wananufaika na ajira na mgodi unachangia huduma mbalimbali za kijamii,” amesema

 

Amezitaja huduma hizo kuwa ni kuchangia miradi ya ujenzi kama shule na zahanati, huduma ya maji ya bomba katika kijiji cha Ntunduwaro, kampuni inatoa kila mwaka Sh milioni 4, kwa vijiji vya Ntunduwaro na Ruanda kuchangia maendeleo.

 

Diwani wa Kata ya Ruanda, Edimund Nditi, ameliambia gazeti la JAMHURI kwamba kulikuwa na makubaliano ambayo kampuni hiyo inayozalisha makaa ya mawe, ilitakiwa kufanya ikiwemo kutoa huduma ya maji kwa wananchi wanaozunguka mgodi, ujenzi wa barabara ya lami, kuleta umeme na utunzaji wa mazingira ikiwemo kudhibiti vumbi linalotokana na shughuli za uchimbaji.

 

Nditi amesema baadhi ya vitu vimetekelezwa, ambapo changamoto kubwa ni upatikanaji wa maji safi na salama katika vijiji vya Ntunduwaro na Paradiso, vijiji hivyo vinapata athari kubwa za kimazingira kutokana na vumbi ambalo linaathiri wananchi kutokana na magari mengi yanayobeba makaa ya mawe kila siku.

 

Nditi amesema kiasi cha pesa ambacho kinatolewa na kampuni ya TANCOAL kila mwaka ni kidogo ukilinganisha na kiwango cha uzalishaji wa makaa ya mawe kwa mwaka na kwamba vijiji vinaathirika kimazingira kutokana na usafirishaji wa makaa ya mawe.

 

“Ina maana kijiji kinavyoathirika kwa mwaka mzima kutokana na shughuli za uchimbaji kinapewa milioni mbili tu sawa na kila baada ya miezi mitatu laki tano kwa kila kijiji, lazima pesa iongezwe,’’ amesisitiza Nditi.

 

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ntunduwaro, John Nyimbo, amesema kiasi cha pesa kinachotolewa na kampuni ya TANCOAL mkataba unaonesha ilitakiwa kutumika kwa ajili ya shughuli za ofisi,hata hivyo kutokana na mazingira ya kijijini fedha hiyo inaingizwa kwenye miradi ya maendeleo ya kijiji kama ujenzi wa soko ambalo linatumiwa na wananchi.

 

Mwenyekiti Nyimbo, amesema uongozi wa sasa wa kampuni ya TANCOAL unajitahidi kushirikiana na wananchi ukilinganisha na uongozi uliopita ambapo Januari 30, mwaka huu ulizinduliwa ujenzi wa mradi wa maji safi na salama unaofadhiliwa na kampuni hiyo wenye thamani ya zaidi ya Sh.milioni 37.

 

“Mradi wa maji ya visima ili kujaza matangi mawili moja lenye ujazo wa lita 100,000, na tangi jingine lenye ujazo wa lita 50,000 ili kusambaza mitaa kadhaa katika kijiji cha Ntunduwaro, mradi huo utamaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama hapa kijijini mwaka huu,’’ amesisitiza Nyimbo.

 

Mwenyekiti wa Kijiji cha Paradiso chenye wakazi 1742, Steven Challe, amesema licha ya kijiji hicho kuwa eneo la mradi wa makaa ya mawe hadi sasa hakuna huduma ya maji safi na salama, huku wananchi wanatumia maji ya mito ambayo yanachafuliwa na vumbi la makaa yam awe.

 

“Serikali ya halmashauri ya wilaya ya Mbinga katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 ilitenga bajeti ya Sh. milioni 320 kwa ajili ya mradi wa maji katika kijiji cha Paradiso na tuliambiwa hadi kufika Juni 2017 mradi huo ungekuwa tayari,’’ amesema Challe.

 

Hata hivyo Challe amethibitisha kwamba hadi sasa hakuna kinachoendelea, maji ambayo wananchi wanatumia hayafai kwa matumizi ya binadamu na kwamba watu wanaendelea kuathiriwa na maji hayo.

 

Naye Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Fransis Nchimbi, amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2017/2018 halmashauri hiyo kwa kutumia chanzo cha mapato cha makaa ya mawe ilitarajia kukusanya Sh. milioni 452.2,hata hivyo hadi kufikia Desemba 2017, halmashauri ilikusanya milioni 197.6 kama ushuru wa huduma (service levy).

 

Nchimbi amebainisha kuwa halmashauri ya wilaya ya Mbinga inakusanya ushuru wa makaa ya mawe katika eneo la Kitai unaotokana na magari yanayobeba makaa ya mawe ambapo katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 hadi kufikia Desemba 2017, halmashauri ilikusanya Sh. milioni 45.6

 

“Katika kipindi cha mwaka 2017/2018 kupitia mapato yetu ya ndani, tulitarajia kukusanya zaidi ya bilioni tisa,hata hivyo hadi kufikia Desemba 2017 tulikuwa tumekusanya zaidi ya milioni 900 kutoka vyanzo mbalimbali vikiwemo chanzo cha makaa ya mawe,zao la kahawa na mazao ya misitu’’,anasema Nchimbi.

 

Hata hivyo Afisa Mipango huyo amekiri mgodi wa makaa ya mawe Ngaka ni moja ya chanzo muhimu cha mapato katika halmashauri hiyo kwa kuwa fedha ambazo zinapatikana kwenye chanzo hicho zinaisaidia kufanya mambo mengi ikiwemo miradi mbalimbali ya maendeleo.

 

Kwa mujibu wa Nchimbi, mgodi wa makaa ya mawe umeisaidia halmashauri hiyo kuagiza vifaa vya viwandani ambapo hadi sasa halmashauri hiyo imeagiza vifaa vyenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 400, fedha ambazo zinatokana na chanzo cha makaa ya mawe.

 

Licha ya mafanikio hayo changamoto za ukusanyaji mapato katika chanzo cha makaa ya mawe amezitaja kuwa ni baadhi ya watendaji wa mgodi huo kutokuwa waaminifu kwa sababu mrahaba wa shilingi milioni 102 wa mwaka wa fedha wa 2017/2018 ulileta changamoto kubwa kwa Halmashauri hadi kufanikiwa kupata.

 

“Baadhi ya watendaji waliopo kwenye mgodi sio waaminifu hawaleti mrejesho wa mapato ulio sahihi kwamba sisi halmashauri kiasi chetu sahihi cha kupata kutoka kwenye makaa ya mawe hiki,hali inayosababisha Halmashauri kupata mapato ambayo sio sahihi,” amesema Nchimbi.

 

Ameitaja changamoto kubwa ni halmashauri kutokuwa na uwezo wa kupata takwimu halisi za mapato yanayotokana na mgodi wa makaa ya mawe, hivyo ameshauri halmashauri hiyo ingekuwa na kifaa cha kieletroniki kwenye mgodi wa makaa ya mawe ili kupata takwimu sahihi ili kuepuka udanganyifu.

 

Akizungumzia kiasi cha fedha Sh. milioni 2, zinazotolewa kwa vijiji viwili katika eneo la mgodi kila mwaka, Nchimbi amesema kiwango hicho ni kidogo kwa sababu uzalishaji wa makaa ya mawe unaofanywa na kampuni hiyo kwa mwaka ni zaidi ya tani 3000.

 

“Ninaposema wanazalisha zaidi ya tani 3000 kwa mwaka ni kiwango cha chini lakini wanazalisha makaa ya mawe kiwango kikubwa, gari moja tu la kubeba makaa ya mawe wanakodi na kulipa shilingi milioni tatu, wana magari zaidi ya 70 ambayo yapo kila siku barabarani kutoka mgodini hadi Kitai, milioni 2 kuwalipa wananchi kwa mwaka ni kuwanyonya,’’ amesisitiza afisa mipango huyo.

 

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Dk.Patrick Banzi amesema katika kukabiliana na changamoto ya kutopata takwimu za sahihi za mapato yanayotokana na mgodi wa Ngaka, halmashauri imejipanga kufanya mazungumzo na uongozi wa mgodi ili kufahamu mapato halisi kwa mwaka kulingana na kiasi halisi kinachozalishwa.

 

Dk. Banzi amesema kuwa mapato ya mrabaha ambao ni asilimia 0.003 yanayotolewa na Kampuni hiyo licha ya kuwa kidogo, lakini Kampuni hiyo imekuwa haitoi kwa wakati na kwamba wanaamini kuwa kuna udanganyifu katika takwimu.

 

Amezitaja changamoto nyingine zinazoikabili halmashauri hiyo ya Mbinga wakati wa ukusanyaji wa mapato kutokana na chanzo hicho, ni pamoja na upungufu wa vifaa vya kielekroniki (POS) vinavyotumika kukusanya mapato ambapo hadi sasa zinazofanyakazi ni mashine 16 tu.

 

“Halmashauri ina upungufu wa rasilimali watu wenye utalaam wa kutumia POS, hivyo halmashauri imewapeleka watalaam Dodoma kujifunza matumizi sahihi ya POS hali ambayo itaongeza makusanyo na kufikia malengo yetu,’’ amesisitiza Dk.Banzi.

 

Wakati huohuo, Meneja Uzalishaji wa Mgodi wa Ngaka David Kamenya amesema makaa ya mawe katika mgodi huo wali yalikuwa yanapatikana mita tano chini ardhini ambapo hivi sasa baada ya uzalishaji kuongezeka madini hayo yanapatikana kati ya mita 40 hadi 50 ardhini.

 

Kwa mujibu wa Kamenya, makaa ya mawe yanayochimbwa katika mgodi huo yanatengenezwa kwa ukubwa wa kati ya milimita 0 hadi 450 na kwamba hivi sasa wamepata wateja kutoka viwanda vyote katika nchi nzima kikiwemo kiwanda cha Dangote cha Mtwara ambacho kinanunua kila mwezi tani 8000 za makaa ya mawe.

 

Meneja Udhibiti Ubora wa Makaa ya Mawe wa TANCOAL, Bosco Mabena, amesema makaa ya mawe ambayo yanazalishwa kwenye mgodi wa ngaka hayana uchafu wa aina yeyote ukilinganisha na makaa mengine nchini na nje ya nchi.

 

Utafiti uliofanywa mwaka 2008 unaonesha kuwa makaa ya mawe ya Ngaka yanaongoza kwa ubora duniani. Katika eneo hilo ambalo zimegundulika tani milioni 400 za makaa ya mawe ambazo zinatarajiwa kuchimbwa kwa miaka zaidi ya 50 ijayo.

Kwa mujibu wa utafiti, madini ya makaa ya mawe Ngaka yamesambaa maeneo yote ya Kijiji cha Ntunduwaro na maeneo jirani ya Kata ya Ruanda.

Licha ya makaa ya mawe ya Ngaka kuuzwa na kutumika viwandani ni muhimu kutumia makaa ya mawe kuzalishia umeme kwa sababu gharama zake ni nafuu kwa wananchi na pia umeme huu utachochea ukuaji wa viwanda nchini hasa katika awamu ya tano ambayo inasisitiza serikali ya viwanda.

Utafiti umebaini kuwa umeme unaotokana na madini hayo ndio unaotegemewa zaidi na mataifa mengi yaliyoendelea duniani.

Takwimu zinaonesha kuwa makaa ya mawe yanachangia asilimia 41 ya umeme unaozalishwa duniani, umeme wa maji asilimia 16,umeme wa gesi asilia asilimia 20, nyukilia asilimia 15 na  umeme wa mafuta kwa kutumia jenereta ni asilimia 6 tu.

Miongoni mwa mataifa yaliyoendelea kiuchumi duniani ni yale ambayo yanatumia umeme wa makaa ya mawe. Mataifa hayo ni Afrika Kusini inayotumia asilimia 93 ya umeme wa makaa ya mawe,Poland asilimia 92 na China asilimia 79.

Nchi nyingine ni Australia asilimia 77, Kazakhstan asilimia 70, India asilimia 69, Israel asilimia 63, Jamhuri ya Czech asilimia 60, Morocco asilimia 55,Ugiriki asilimia 52,Marekani asilimia 49 na Ujerumani asilimia 46.

Katika kutekeleza dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025, Tanzania inatarajia kuzalisha umeme wa makaa ya mawe ambayo yameenea katika mikoa ya kusini hususan mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Iringa na Njombe.

 

Sera Taifa ya madini ya mwaka 1997 inasisitiza juu ya sekta binafsi kuendeleza madini ambapo Serikali katika sera hiyo ina jukumu la kuidhibiti, kuikuza na kuiendeleza sekta hiyo.

 

Sekta ya madini inachangia takribani asilimia 3.5 ya Pato la Taifa, ambayo inakadiriwa kufikia asilimia 10 ifikapo 2025.

 

Makala hii imeandikwa chini ya udhamini wa wakfu wa vyombo vya habari Tanzania (TMF).

By Jamhuri