’Yeye anayesubiria kuvaa viatu vya marehemu anaweza kutembea pekupeku kwa muda mrefu’’.

                                                -Methali ya kifaransa

”Ulizaliwa ili kushinda lakini ili kuwa mshindi lazima upange kushinda, ujiandae kushinda na utegemee kushinda”.

                                                                    -Zig Ziglar

Mwanasayansi Albert Einstein alipata kushauri, “ukifikiri mwaka mmoja ujao panda mbegu. Ukifikiri miaka 10 ijayo panda mti. Ukifikiri miaka 100 ijayo elemisha watu”.

Mwanasayansi huyu alikuwa na maana hii, kwa kupanda mbegu utavuna mara moja. Inapendeza. Kwa kupanda mti utavuna mara 10. Inapendeza kiasi.

Kwa kuelimisha watu utajenga kizazi kinachojitambua. Inapendeza. Maisha ni malengo. Hakuna maisha ya mkato. Ishi kwa malengo.

Tusiichi kwa sababu tunaishi. Tuishi kwa malengo, kwa sababu Mungu ametuumba tuishi kwa malengo. Ungana na Henry James kuamini maneno haya, “ni muda mwafaka wa kuishi maisha ambayo umeyafikiria kwa muda mrefu.’’

Binadamu wengi wanaishi ni kwa sababu wanaishi. Hawaishi kwa malengo. Kupanga ni kuchagua.

Mwanafalsafa Benjamin Frankln anasema, “ukishindwa kujiandaa, umejiandaa kushindwaa.’’ Hakuna anayepanga kushindwa ila wengi wanashindwa kupanga.

Mwandishi Vicent Lombardi amesema, “kila mtu anapenda kufanikiwa ila ni wachache wanapenda kujiandaa kufanikiwa.’

Kuna methali ya kifaransa inayosema hivi, “yeye anayengoja kuvaa viatu vya marehemu anaweza kutembea pekupeku kwa muda mrefu’’.

Kusubiri maendeleo yatokee pasipo kufanya kazi kwa bidii ni kama unaishi kwa kusubiri viatu vya marehemu. Kulalamika kwa kila jambo pasipo kubuni mbinu na mikakati ya kukuinua kiroho, kimaadili, kisiasa, kiafya na kiuchumi ni kama unaishi kwa kusubiri viatu vya marehemu.

Kukaa na ukimsubiri mwanaume mwenye pesa ajitokeze kukuoa ni kama unaishi kwa kusubiri viatu vya marehemu.

Methali ya Kiswahili inaupambanua ukweli huo kwa maneno haya, “ mtegemea cha ndugu hufa maskini.’’ Mtu anayeweza kukuokoa ni wewe mwenyewe.

Ni wewe unayeweza kujiandikia historia nzuri au mbaya. Ni wewe unayeweza kuwa chachu ya mabadiliko au mhanga wa mabadiliko.

Ishi kadri ya uwezo wako, usiishi kama  watu wengine wanavyotaka uishi. Methali ya Kiswahili inatukumbusha maneno haya, “miluzi mingi humpoteza mbwa.’’

Watu wengi walioshindwa kufanikiwa kimaisha, kiroho, kimaadili ni wale walioishi kadiri ya watu walivyowapendekezea waishi.

Usijaribu kuishi kwa kumfurahisha mwanadamu, ishi kwa kumfurahisha Mungu. Ukiishi kwa kumfurahisha mwanadamu, ipo siku huyo mwanadamu uliyeishi kwa kumfurahisha atakusaliti.

Mhubiri wa injili, Israel Ayivor alipata kusema, “yule aliyekusaidia kuzungumza mambo mabaya kuhusu mwenzako, ndiye atakayemsaidia mtu mwingine kuzungumza uovu juu yako.’’ Maneno haya yana ukweli ndani yake. Ndivyo binadamu tulivyo. Tuna tabia ya undumila-kwili.

Maisha hayaongozwi kwa mihemko na papara zisizo na dira. Maisha hayaongozwi kwa dhuluma. Maisha yanaongozwa kwa hekima, busara, maono na jitihada binafsi.

Hauwezi ukawa kama unavyotaka uwe kama haujawa na dhamira ya dhati ya kubadilika. George Benerd Shaw alipata kuandika haya, “maendeleo hayawezekani bila mabadiliko ya fikra na wale ambao hawawezi kubadilika namna wanavyofikiri hawawezi kubadili chochote.”

Stephen Richards anaamini kwamba, “namna yetu ya kufikiri inatengeneza matokeo mazuri au mabaya.’’

Ukosefu wa fikra sahihi na bainifu kwa maisha ya mwanadamu yeyote ni ugonjwa. Ni ugonjwa usioonekana kwa vipimo vya kisayansi, lakini ni ugonjwa unaoua kwa haraka kuliko magonjwa mengine.

Ni ugonjwa unaoonekana kwa vitendo na kwa maamzi mbalimbali ya mhusika. Fikra sahihi zinaishi. Badilika kwanza. Badili mtazamo wako katika kufikiri. Badili mtazamo wako kwa kuupenda ukweli ulivyo na uhalisia wake.

Badili mtazamo wako kwa kusoma tafiti za wasomi mbalimbali, vitabu, magazeti, na majarida mbalimbali. Lisilowezekana linawezekana kwa kubadili namna ya kufikiri. Maisha ni malengo. Baba wa kiroho Sai Baba alipata kuyatafsiri maisha kwa namna hii;

“Maisha ni wimbo-uimbe, ni mchezo-ucheze, ni changamoto-ikabili, ni ndoto-ielewe, ni sadaka-itoe, ni upendo-ufaidi, ni lengo-lifikie, ni kengele-igonge, ni barabara-ipite na ni mti-upande.’’

Kwa hakika maisha ni wimbo, imba kadri ya uwezo wako. Maisha ni mchezo, cheza kadri uwezavyo. Maisha ni changamoto, kabiliana na changamoto unazokutana nazo katika maisha yako.

Maisha ni ndoto, timiza ndoto ulizonazo katika maisha yako. Msanii wa nyimbo za hip pop, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Mbeya Mjini, katika kibao chake cha ‘’muziki na maisha’’ anatufundisha falsafa inayosema, ‘’maisha ni ubishi’’.

Maisha ni kuanguka na kuinuka. Ukianguka inuka. Ukianguka amini unaweza bado kufanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Maisha bila malengo ni kama suruali isiyo na zipu!  Katika filamu ya Chariotos of fire, mkimbiaji wa Olympic Eric Liddell amesema, “Mungu  aliniumba kwa malengo.’’

Kama anavyosema kwa ufasaha kabisa Ethel Waters kwamba, “Mungu haumbi takataka.’’  Kuna watu wanaofikiri kwamba wapo duniani kwa bahati mbaya. Sio kweli.

Hapa duniani hakuna binadamu aliyeumbwa kwa bahati mbaya. Mchungaji Rick Warren amesema, “hapo zamani kabla hujawa katika tumbo la mama yako, ulikuwa katika mawazo ya Mungu.’’

Kuzaliwa kwako hakukutokana na makosa wala bahati mbaya. Mungu hana sifa ya kukosea. Mungu hana sifa ya kubuni.

Mungu ana sifa za uhakika. Mungu ana sifa ya umilele. Uko hai kwa sababu Mungu alitaka kukuumba ili uwe sehemu ya viumbe walioumbwa na Mwenyezi Mungu.

Upo ukweli unaopendwa kutumiwa na watu wengi, ukweli huo unasema hivi, “kazi ya Mungu haina makosa.’’

Ni ukweli kwamba hujaumbwa kwa makosa wala kwa bahati nasibu. Mwanasayansi Albert Einstein anasema, “Mungu hachezi bahati nasibu.’’

Mshairi Russel Kelfer amesema, “wewe ni wewe kwa kusudi.  Wewe ni sehemu ya mpango wa ajabu. Wewe ni wa thamani na chombo maalumu kikamilifu. Unaitwa mtu mwanaume au mwanamke maalumu wa Mungu.’’

Biblia Takatifu imesema, “umeumbwa kwa namna ya ajabu.’’ Neno kwa namna ya ajabu ni zito kulifafanua kwa ufahamu wetu wa kibinadamu.

Lakini neno kwa namna ya ajabu kwa sehemu yangu na uelewa wangu naweza kulifafanua kwa namna ifuatayo; binadamu ni kiumbe aliyepewa upendeleo wa aina yake katika uumbaji.

Kiumbe huyu ana uwezo wa kujenga au kubomoa, ana uwezo wa kufikiri, kutenda na kuamua, ana uwezo wa kubadili kile anachokiona na ana uwezo wa kutawala viumbe wengine kutaja machache.

Sifa nyingine ya binadamu ni Kubadilika; Binadamu sio kama gogo ambalo linaweza kukaa miaka mingi kwenye maji lakini lisibadilike hata siku moja na kuwa mamba.

Binadamu anabadilika na anabadili. Na yote katika yote ni kwamba mwanadamu amepewa upendeleo wa aina yake, wa kuumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kuumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ni zawadi. Ni muujiza. Ni maajabu.

Hujaumbwa kwa bahati mbaya. Umeumbwa kwa malengo. Hivyo basi furahia namna ulivyoumbwa. Furahia namna walivyoumbwa wengine.

Furahia namna dunia ilivyoumbwa kwa ustadi mkubwa. Furahia kuitwa raia wa taifa lako. Yape maisha yako mhuri wa malengo. Yape maisha yako mhuri wa utakatifu.

Yape maisha yako mhuri wa upendo. Yape maisha yako mhuri wa msamaha. Yape maisha yako mhuri wa Uadilifu. Yape maisha yako mhuri wa unyenyekevu. Yape maisha yako mhuri wa bidii katika kazi, bidii katika kumtumikia Mungu aliyekupa zawadi ya uhai.

Kila siku amka na malengo ya juu. Amka na mbinu mpya, mawazo mapya, ushauri mpya, upendo mpya kutaja machache. Usiwe mtu wa kufikiri kwa karibu. Amini unaweza kuyatimiza malengo yako. Usikate tamaa.

Methali ya kichina inatutia moyo kwa maneno haya, “dunia ni ya wale ambao wanavuka madaraja mengi katika kufikia kwao kabla ya wengine kuona daraja hata moja.’’

Dunia ni ya watu wasiokata tamaa. Uliwekwa duniani kutoa mchango wako. Mabadiliko yanaanza na wewe. Mafanikio yanaanza na wewe. Anza kwa kuonesha njia. Penye nia pana njia. Vipaumbele vinatuagiza; kuhesabu visivyohesabika.

Kuwekea muda kinachoishi milele. Kuwekea umbo kisichoweza kuumbika. Kutafuta thamani ya kisichopimika. Kuwekea mipaka kisichokuwa na mwisho. Kuwekea taswira kisichoweza kuwa na sura.

Kuanzisha kisicho na mwanzo. Barack Obama Rais wa 44 wa Marekani amesema, “mabadiliko hayawezi kutokea kama utamsubiri mtu mwigine au muda fulani. Sisi ndio mabadiliko tuliyoyasubiri muda mrefu.’’

Kila kukicha mwanadamu anakabiliwa na zoezi la kufanya uchaguzi fulani. Ulimwengu huu hauna nafasi kwa watu wanaopuuzia maarifa ya mhimu.

Kila kukicha yeyote anaalikwa kuukaribisha utajiri na kuuaga umaskini au kuuaga utajiri na kuukaribisha umaskini. Lakini yote katika yote tunahitaji kuandika upya historia mpya ya maisha yetu na taifa letu.

Tuyatazame mazingira yetu tunayoishi kwa jicho la ushindi. Tuutazame huu ulimwengu kwa jicho la ushindi. Wahenga walipata kunena, “penye nia pana njia.’’

Hannibal [183-247] mgunduzi wa silaha za kivita anashauri, “lazima tuone njia kama haipo tuitengeneze.’’ Ni wakati sasa wa kuitengeneza njia upya!

Hatuwezi kubadili kilichotokea, kwani ni historia tayari. Na sasa Tufungue macho yetu tuzione fursa zinazotuzunguka.

Mwandishi wa Kihispania Anais Nin amesema, “hatuoni vitu kama vilivyo, tunaviona kama tulivyo.’’ Huu ni wakati wa kuviona vitu vilivyo na sio wakati wa kujiona tulivyo.

Kila mtu sasa na ajihisi kama mvumbuzi, mtafiti na mtatuzi wa matatizo yanayoikabili jamii yetu. Uhodari wa kuishi si uhodari wa kuishi miaka mingi, lahasha!

Ni uhodari wa kuwa msaada katika jamii inayokuzunguka na ulimwengu kwa ujumla wake. Tutafanikiwa kiroho, kimaadili, kisiasa, kijamii na kiuchumi endapo kila mtu atawajibika kufanya kazi kwa maadili mema kwa nafasi yake aliyopo.

Mafanikio yako yanategemeana na maamzi yako uliofanya. James Allen amesema, “leo uko pale ambapo mawazo yako yamekuleta, kesho utakuwa pale ambapo mawazo yako yamekupeleka.

Jenga leo yako vizuri ili kesho yako iwe nzuri zaidi. Mchezaji wa mpira Jerry Rice amesema, “leo nitafanya ambayo wengine hawatataka kufanya ili kesho niweze kutimiza ambayo wengine hawataweza kutimiza.’’

By Jamhuri