Ujauzito unachangia mabadiliko mbalimbali ya mwili tangu mwezi wa kwanza hadi mwezi wa tisa, mwanamke anapojifungua.

Baadhi ya matatizo hayo yamekuwa ni ya kawaida, lakini hayatakiwi kufumbiwa macho, hivyo ni vyema kwa mjamzito kuwa karibu na upatikanaji wa  huduma za afya mara kwa mara, badala ya kusubiri hadi siku ya kuhudhuria kiliniki au muda wa kukaribia kujifungua.

Haya ni baadhi ya matatizo  yanayojitokeza mara kwa mama mjamzito na namna ya kukabiliana nayo:-

Pica

Ni ukweli usiopingika kuwa, wajawazito wengi hupendelea kula vitu ambayo kwa mtu mwenye afya ya kawaida hawezi kuvila.

Ulaji wa udongo, vitu vyenye asidi na ukakasi kwa wingi hususani matunda mabichi kama vile maembe malimau na vitu vingine vichachu umekithiri sana kwa wajawazito kutokana na mabadiliko yanayojitokeza mwilini,k yanayopelekea kuvuruguka na ladha midomoni.

Tabia hii inawaweka hatarini wajawazito kupata ugonjwa unaoitwa pica. Huenda ni ugonjwa ambao wengi hawaufahamu, pica ni ugonjwa unaotokana na ulaji wa vitu ambavyo havipo kwenye kundi la chakula ambalo mtu anapaswa kutumia kama mlo.

Wajawazito wapo hatarini zaidi kupata ugonjwa huu kutokana  na na tabia ya kula vitu ambavyo haviendani na mahitaji ya lishe ya mjamzito.

Wajawazito wanashauriwa kuacha tabia ya kula vitu ambavyo haviendani na lishe ya mjamzito, ili kuepukana na magonjwa kama pica ambayo inaweza kuathiri mfumo wa chakula wa mjamzito na hata kuzaa mtoto njiti.

Maumivu ya kichwa ya mara kwa mara

Wajawazito wengi hupata maumivu ya kichwa ya mara kwa hasa katika kipindi cha miezi mitano ya kwanza  ya ujauzito na hua yanaisha mwanzo wa muhula wa tatu, yaani mwanzo ni mwa mwezi wa sita.

Maumivu haya ni kawaida kutokea kutokana na mabadiliko yanayojitokeza kwenye mfumo wa homoni na mjamzito anaweza kuyakabili kwa kutumia dawa za kupunguza maumivu chini ya ushauri wa daktari.

Lakini wakati mwingine maumivu haya ya kichwa yakidumu kwa zaidi ya miezi sita mfululizo yanaweza kuashiria tatizo lingine kubwa zaidi ya kichwa chenyewe.

Ni muhimu  kwa wakati huu kupata msaada wa kitabibu mara kwa mara ili kubaini tatizo hasa, kwa sababu maumivu yeyote ya kichwa anayoyapata mjamzito yakidumu kwa muda mrefu, yanaweza kuashiria matatizo kama  yanayojitokeza kwenye ubungo ikiwemo, uvimbe kwenye ubongo na kuvuja damu ndani ya ubongo.

Mbali na maumivu ya kichwa, dalili zingine zinaweza kuwa, kutetemeka na  mwili kukosa nguvu.

Miguu kuvimba

Huku kunawapata takribani wajawazito wote. Hili haliashirii tatizo lolote kubwa la kiafya hasa tukizingatia ukweli kwama, kutokana na sababu za kimaumbile, mwanamke huwa na uhifadhi mkubwa wa maji na hivyo kusababisha kiasi fulani cha maji kujitokeza kwenye sehemu mbali mbali za mwili zikiwemo miguuni na kwenye maungio ya miguuni.

Mara nyingi hutokea kuanzia mwezi wa tano  wa ujauzito, hua haimbatani na maumivu yeyote makali wala homa.

Ikumbukwe kuwa hali ya kuvimba au kuonekana imejaa maji huwa inatokea miguuni tu na sio sehemu nyingine za mwili.

Lakini hali hii ikijitokeza na sehemu nyingine ya mwili, ni vyema kupata kupata ushauri wa daktari na vipimo haraka sana kwa sababu hali ya kujaa maji kwenye sehemu mbali mbali za mwili ni ishara kuwa figo zinasimama kufanya kazi.

By Jamhuri