MAJALIWA : UKIKUTWA NA MWANAFUNZI KICHOCHOLONI TUTAKUKAMATA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kuwalinda watoto wa kike na ndiyo maana tunawataka watoe taarifa za watu wanaotaka kuwakwamisha kimasomo kwa watendaji wa vijiji kwenye maeneo yao.

Alitoa agizo hilo wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wakazi wa wilaya ya Masasi akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi mkoani Mtwara.

Waziri Mkuu alisema watoto wa kike wanatakiwa kuheshimiwa katika jamii kwa kuachwa waendelee na masomo yao bila ya usumbufu wa aina yoyote na atakayebainika kukatisha masomo atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Alisema Serikali itatoa adhabu kali ya kifungo cha miaka 30 jela kwa mtu atakayekatisha elimu ya mtoto wa kike iwe kwa kumuoa, kumpa ujauzo na hata ukikutwa naye nyumbani kwako, katika nyumba ya wageni.

“Tukikukuta na binti wa shule katika kona isiyoeleweka tunakukamata na kukuchukulia hatua za kisheria. Ole wenu vijana, mkibainika mmewapa mimba mabinti wanaosoma, adhabu yake ni miaka 30 jela.”

Waziri Mkuu alisema kwa wazazi au walezi watakaowaozesha watoto kike ambao bado wanafunzi na kwa upande wa wazazi watakaomsindikiza mtoto kwenda kuoa mwanafunzi wote watachukuliwa hatua za kisheria.

Pia Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwataka wanafunzi wote kusoma kwa bidii ili watimize ndoto zao na wasikubali kushawishika kwa sababu watashindwa kufikia masomo yao.