Asoma na kujibu kiubabaishaji tuhuma kwenye magazeti aliyodai awali kuwa ni ya kufungia maandazi. Kwa muda mrefu sasa baadhi ya magazeti hapa nchini yamekuwa yakiujuza umma ukweli kuhusu Lazaro Nyalandu, ambaye kwa takriban miezi tisa sasa ni Waziri wa Maliasili na Utalii. Habari kumhusu Nyalandu zilianza kutolewa hata kabla hajawa Naibu Waziri wa Wizara hiyo, wakati angali Naibu Waziri katika Wizara ya Viwanda na Biashara, chini ya Cyril Chami wakati huo. Katibu Mkuu wa Wizara hiyo wakati huo alikuwa Joyce Mapunjo.

Kwa bahati mbaya, kwa upande wa Nyalandu mwenyewe habari nyingi kumhusu zimekuwa ni juu ya jinsi asivyoweza na asivyofaa kuongoza wizara yoyote, achilia mbali ile ya Maliasili na Utalii. Kati ya habari kubwa ni ile iliyoandikwa na gazeti la Jamhuri la Agosti 19 – 25, 2014, ISSN Na. 1821-8156, Toleo Na. 150, iliyobeba kichwa cha ‘KASHFA IKULU’.

Ingawa habari hiyo ilikuwa kubwa na yenye kuanika uozo wa Waziri huyo, yeye alikaa kimya kwa zaidi ya miezi miwili bila kuitolea maelezo hadi juma lililopita ambako alitoa alichokiita Taarifa kwa Umma akijaribu kukanusha. Swali ambalo Taarifa hiyo kwa Umma ilipaswa kuanza kulijibu ni, ni kwanini imechukua zaidi ya miezi miwili kwa Nyalandu kutolea taarifa habari hiyo? Mimi naamini, kwa jinsi nilivyoiona ile habari ya Agosti, sababu ni kwamba Nyalandu hakuwa na, na bado hana, maelezo ya kujitosheleza na hivyo aliogopa kujitokeza – angeueleza nini umma ukamwelewa.

Na, je, ni kwa nini kajitokeza sasa, zaidi ya miezi miwili baadaye? Tumetaarifiwa na gazeti la Jamhuri toleo lililopita kuwa, katika kikao chake cha hivi karibuni, Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliikataa taarifa ya Waziri Nyalandu. Hii si dalili njema kwake kwenye vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano linaloanza vikao vyake mjini Dodoma wiki hii.

Kwa maana hiyo anatapatapa kujaribu kupunguza makali ya wabunge. Hana hofu na Ikulu aliyoichafua, kwani alikwishasema kuwa Ikulu haiwezi kumwajibisha! Hofu yake pekee ni kwa wabunge.

Taarifa ya Nyalandu kwa Umma inaanza kwa kudai kuwa: “Wizara ya Maliasili na Utalii inapenda kuufahamisha umma kuwa, tuhuma hizi si za kweli. Tuhuma hizi zimetolewa na watu wenye nia ovu  na zimelenga kuchafua jina la Wizara ya Maliasili na Utalii na kumchafua Mheshimiwa Waziri Lazaro Nyalandu, kumshushia heshima, kumdhalilisha kwa umma ili kumpunguzia dhamira, malengo na  kasi ya kupambana na ujangili.”

Ninajaribu kuilazimisha akili yangu ikubali maelezo kuwa tuhuma zilizotolewa Agosti dhidi ya Nyalandu hazikuwa za kweli. Lakini, kama nilivyokwishaeleza hapo juu, ni kwa nini imemchukua Nyalandu zaidi ya miezi mitatu kusema tu kuwa tuhuma hizo si za kweli? Zitolewapo tuhuma za uongo kunakuwapo na vielelezo vya kutumia kuzikanusha. Je, kigugumizi cha kusema tu hivyo kilisababishwa na nini? Ingawa maelezo haya yalipaswa kuwapo mwanzoni kabisa, hili halionekani kabisa kwenye Taarifa kwa Umma iliyotolewa na Nyalandu.

Kama inavyosomeka katika aya iliyotangulia, taarifa hiyo ya Wizara kwa Umma (ingawa taarifa za uhakika ni kuwa haikuandaliwa na kitengo cha mawasiliano cha Wizara – na wao wameiona tu kwenye vyombo vya habari) inadai pia kuwa: “Tuhuma hizi zimetolewa na watu wenye nia ovu …” Kauli hii si ngeni katika masikio yetu Watanzania. Kila viongozi wanapovurunda, uozo wao ukitolewa kwenye vyombo vya habari hulalama kwamba waliofanya hivyo wamefanya kwa nia ovu. Kauli hii ni ya kawaida kutolewa na viongozi wenye imani kuwa wao wana haki miliki ya nchi hii. Ni kawaida pia kutolewa na viongozi wenye imani potofu kuwa ni peke yao wanaoweza kufikiri na kutafakari kupambanua yaliyo maovu na mema.

Pia, ni kauli za kawaida kwa viongozi watenda maovu ambao, baada ya kutenda uovu wao, hukimbilia kudai huruma ya wananchi kwa kudai kuwa wao na taasisi wanazoziongoza wanachafuliwa majina au sifa. Lakini, nimelisoma tena toleo hilo la Gazeti la Jamhuri, sioni mahali Wizara ya Maliasili na Utalii inachafuliwa jina, bali kwa mtazamo wangu, habari ile ilifichua uozo na uovu wa kiongozi wa Wizara hiyo, yaani Waziri Nyalandu. Kwa mantiki hii habari hiyo inaisaidia Wizara kumrekebisha kiongozi wao kwani, kwa mfumo wa utumishi wa umma Tanzania, watumishi wizarani pale hawawezi kufanya hilo.

Hoja kwamba habari ile kwenye Gazeti la Jamhuri imemchafua Waziri Nyalandu, imemshushia heshima, imemdhalilisha kwa umma ili kumpunguzia dhamira, malengo na kasi ya kupambana na ujangili pia inalenga kuwahadaa Watanzania. Kama haya yanayosemwa sasa yangekuwa na ukweli basi, Taarifa hii kwa Umma ingetolewa mara tu gazeti la Jamhuri lilipoandika habari ile mwezi Agosti. Na mbona, hata baada ya habari hiyo kuandikwa, Nyalandu ameendelea kufanya mambo yanayoiabisha Serikali na mteuzi wake?

Yameandikwa na kusemwa kwenye vyombo vya habari. Mimi ninaamini, kama mwandishi mmoja alivyopata kuandika, kuwa Nyalandu ni janga la kitaifa na tukiri tu hivyo. Kama mamlaka yake ya nidhamu haioni haja ya kuchukua hatua, ingawa wanaelewa, na Katiba ya nchi inawalinda; basi tuwalaumu wao na Katiba.

Taarifa ya Nyalandu kwa Umma inadai kuwa “… Familia ya Freidkin ilipewa Leseni Maalum/Leseni ya Rais (Special License/President’s License) ya kuwinda kwa mujibu wa Kifungu cha 58 (1) cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 ikisomwa kwa pamoja na Tangazo la Serikali Na. 273 la mwaka 1974 …” Hapa napo kuna dalili zote za kuudangaya umma, kama si kuuongopea zaidi. Kwa imani kwamba ‘ukitaka kuwaficha Watanzania kitu basi kiweke kwenye maandishi’ kwa sababu hawana utamaduni wa kujisomea, Nyalandu anadhani atauaminisha umma kuwa alichokifanya ni sahihi kisheria na kwamba Gazeti hili (na mengine yote yaliyopata kumwandika) limemzushia uongo.

 

Tafadhali Watanzania tuelewe kuwa kifungu 58(1) cha sheria na. 5 ya 2009 hakimpi Mkurugenzi wa Wanyamapori wala yeye Nyalandu, kama Waziri mwenye dhamana ya wanyamapori, mamlaka ya kufanya alichokifanya kwa kushirikiana na ‘Bwana Ndiyo’ wake Sarakikya. Asiyeamini ninalolisema akajisomee mwenyewe kwani sheria hiyo inapatikana maktaba na kwenye tovuti ya Bunge na ile ya Serikali Kuu. Ukiisoma sheria utaepuka kudanganywa na aidha mwandishi wa makala hii au na Nyalandu. Utauelewa ukweli na utaweza kuhukumu ‘kesi’ hii ya Nyalandu dhidi ya Gazeti la Jamhuri kwa usahihi. Utajua mkweli ni yupi na muongo ni yupi na, kama utakuta muongo ni Nyalandu, ninashauri utafute jibu la swali kama Katiba na sheria za Tanzania vinaruhusu kuwapo mawaziri waongo. Kama haviruhusu, basi ungana na wazalendo wengine kudai Waziri wa aina hii ang’olewe kwani hatakiwi kuwapo madarakani. Hatupaswi kujenga jamii ya watu waongo.

Nyalandu aoneshe agizo la Mheshimiwa Rais akielekeza familia hiyo ipatiwe leseni yoyote, achilia mbali Leseni Maalum. Lakini udanganyifu wa Nyalandu hauishii hapo tu kwani, Tangazo la Serikali na. 273 la mwaka 1974 lilihusu uwindaji kwa mujibu wa Sheria na. 12 ya mwaka 1974 ambayo iliruhusu uwepo wa Leseni ya Rais. Sheria Na. 12 ya mwaka 1974 ilifutwa (was repealed) na Sheria Na. 5 ya mwaka 2009. Katika Sheria na. 5 ya mwaka 2009 hakuna Leseni ya Rais, bali kuna Leseni Maalum na malengo yake ni tofauti.

Sasa Nyalandu atuambie Watanzania kuwa, sheria inayohusika na tangazo la serikali ikifutwa tangazo lenyewe linaendelea kutumika, tena miaka mitano baada ya sheria mpya kuwa inatumika! Kama anataka tumwachie huru awathibitishie Watanzania kuwa familia hiyo ya Wamarekani walikuwa kweli ni wageni wa Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, kwamba hawakuwa wageni wake yeye na kwamba kulikuwa na agizo la Mheshimiwa Rais kuwa Wamarekani hao wapatiwe Leseni Maalum.

Nyalandu anaelewa kuwa, kwa hulka ya Watanzania ya kutojisomea na kutozijua sheria za nchi, akibandika vifungu vya sheria na namba za matangazo ya Serikali kwenye Taarifa yake kwa Umma, hata kama ni vya uongo, Watanzania watamwamini tu. Kwa nini wasimwamini ilhali yeye ni Waziri, tena mwenye dhamana ya wanyamapori! Asiyeamini kuwa Tangazo la Serikali Na. 273 la mwaka 1974 lilikwishafutwa aombe ufafanuzi kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Angalia kichekesho kingine cha Nyalandu: Anadai katika Taarifa yake kwa Umma kuwa, “Freidkin na familia yake walipewa Leseni Maalum/Leseni ya Rais kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 243 la mwaka 2010 Kanuni ya 19(2) ambalo linaeleza kuwa mwenye Leseni ya Rais anaruhusiwa kuwinda eneo lolote kama atakavyoelekeza Mkurugenzi wa Wanyamapori.” Eti msomaji, bado hujaona uongo hapa? Nyalandu alitumia Tangazo la Serikali Na. 273 la mwaka 1974 au Na. 243 la mwaka 2010? La mwanzo tumeona kuwa lilikwishafutwa. Hili la pili linaelekea kuwa la kujitungia kwani haliwezi kuongelea Leseni ya Rais ambayo haitambuliwi na haipo katika Sheria Na. 5 ya mwaka 2009. Ni ajabu kuona kuwa sasa, badala ya Nyalandu kukiri na kutubu makosa yake, anawazushia uongo waliomwanika hadharani na kuanza kusaka huruma ya Watanzania kwa kuwaongopea zaidi. Watanzania wa leo si mazezeta.

 

Nyalandu amekiri mwenyewe katika Taarifa yake kwa Umma kuwa Leseni Maalum hutolewa kwa ajili ya utafiti wa kisayansi, makumbusho, elimu, utamaduni au chakula wakati wa dharura. Alipaswa vile vile atuambie Watanzania ni kwa lipi kati ya hayo matano ambalo familia ya Friedkin ilikuwa inahitaji wanyama wetu. Hapa ninaomba niwahimize ndugu zangu wabunge kuwa Waziri huyu asifumbiwe macho. Nyote mnaelewa kuwa mamlaka yake ya nidhamu imeamua kuweka zip kwenye midomo. Tumaini la wananchi limebakia kwenu kuchukua hatua stahiki.

Nyalandu anaeleza kuwa “Maslahi ya taifa ni pamoja na leseni kutolewa kwa watu mashuhuri kama vile … watu ambao katika utendaji wao wametoa michango yenye manufaa maalum kitaifa au michango mikubwa katika shughuli za uhifadhi wa wanyamapori.”

Mtu anaposema ‘maslahi ya taifa’ msomaji anatarajia kuona maana ikitolewa, lakini Nyalandu ameshindwa kufanya hivyo. Hata hivyo, maslahi ya Tanzania kama taifa yanayotokana na familia ya Friedkin ikilinganishwa na wamiliki wengine wa kampuni za uwindaji hapa nchini na kusababisha Nyalandu aipe familia hiyo Leseni Maalum hayakuwekwa wazi. Kuna wamiliki wa kampuni kubwa za uwindaji (majina tunayo) ambao wameendesha biashara zao hapa nchini kuanzia miaka ya 1980 au kabla na miaka yote wamekuwa wakichangia zaidi ya vitu alivyovitaja Nyalandu kwenye Taarifa yake kwa Umma kama utetezi wa kuwahonga Wamarekani wake rasilimali za nchi yetu.

Mbona hao hakuwapa wala hajafikiria kuwapa hiyo Leseni Maalum? Alitumia vigezo gani na alishirikisha mamlaka gani katika uamuzi wake? Je, hii si sawa na linalofanyika la kuteua marafiki wasio na sifa hata chembe kuwa kwenye bodi za mashirika ya umma?

Nyalandu anadai kuwa aliwapa rafiki zake Wamarekani Leseni Maalum eti kwa kuwa “FCF imekuwa ikitoa michango mikubwa hususan ya kukabiliana na ujangili. Bw. Freidkin kwa kupitia Taasisi hii amekuwa akichangia na hata kushiriki katika shughuli za kuzuia ujangili …”

Mbona zipo kampuni nyingi zilizotoa michango mikubwa zaidi na kwa muda mrefu zaidi? Ilikuwaje wao wasipatiwe hizo Leseni Maalum? Hata hivyo, swali ninalohangaika kulipatia jibu na Nyalandu amekwepa kulijibu ni, je, mmiliki wa kampuni za uwindaji – kwa maana nyingine mteja wa Wizara ya Maliasili na Utalii – anayo haki kisheria kupatiwa Leseni Maalum? Je, mtu huyo anaweza kuhesabiwa kama mgeni wa Rais?

Watanzania tutambue kuwa kumekuwa na utapeli mkubwa unaofanywa na Wamerekani hawa. Mfano mmoja tu kati ya mingi ni kumkabidhi Nyalandu mwenyewe – aidha akijua au bila kujua kuwa ulikuwa utapeli – hundi ya fedha nyingi kwa ajili ya kupambana na ujangili ambazo hata hazikufika serikalini. Hundi hii alikabidhiwa kwake Nyalandu akihitimisha matembezi ya kupinga ujangili wa tembo kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es salaam, mwaka jana. Hebu aeleze fedha hizo zilikwenda wapi na, kama atasema haikuwa zikabidhiwe serikalini, aeleze ni kwa nini alikabidhiwa yeye hundi hiyo.

Kama ilivyokwisharipotiwa na magazeti huko nyuma, ni Wamarekani hawa hawa ambao wamevuruga na wanaendelea kuvuruga uwindaji wa kitalii hapa nchini kwa kunyang’anya kimabavu vitalu vya uwindaji vilivyogawiwa kwa kampuni nyingine kisheria na kihalali kabisa. Wanakingiwa vifua na Nyalandu huyo huyo akishirikiana na James Lembeli ambaye anatumia vibaya kofia yake kama mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira. Wote wawili wanafanya hivyo si kwa maslahi ya taifa, bali kwa maslahi yao binafsi.

Pia, ni Wamarekani hawa hawa ambao walishangilia na kufanya sherehe alipojiuzulu Balozi Kagasheki na kumpongeza Nyalandu kwa shangwe za ajabu alipoteuliwa. Ni hawa hawa waliompatia helikopta aliyozunguka nayo kuwazuga wateuzi wake kuwa yeye alifaa kuvaa viatu vya Balozi Khamis Kagasheki kama Waziri wa Maliasili na Utalii; helikopta ambayo alipatiwa bure. Tujue hakuna vya bure na sasa ilikuwa zamu yake kulipa fadhila. Badala ya kulipa kutoka mfukoni kwake, akaamua kuipatia familia hiyo kibali cha kuwinda rasilimali za umma wa Watanzania, baadhi yao wakiwa watoto, wasioruhusiwa na sheria kuwinda hapa nchini.

Katika Taarifa yake kwa Umma, Nyalandu anadai kuwa familia hiyo rafiki zake eti walipatiwa Leseni Maalumu kihalali na kisheria kuwinda wanyama 704. Anaeleza pia kuwa, tofauti na leseni za aina hiyo nyingine tatu zilizotolewa, Wamarekani wake walilipia ada ya vibali (permit fee), ada ya nyara (trophy handling fee) na ada ya uhifadhi (conservation fee). Hata hivyo, ameshindwa kabisa kuonesha vielelezo vya malipo hayo. Pia, Wamarekani wake walipokurupushwa na kukimbia walikuwa wamekwishaua wanyama kadhaa. Ingawa Taarifa yake kwa Umma ameitoa zaidi ya miezi miwili baada ya uwindaji kufanyika, Nyalandu haelezi na kutoa uthibitisho kuwa aliyoiita ada ya wanyamapori imekwishalipwa na hao Wamarekani wake.

Lakini, hebu tujiulize kidogo. Je, mtu anayekuwa ameruhusiwa kufanya kitu fulani kisheria na kihalali, tena kwa malipo, hukimbia na kutokomea pale anapokutwa akifanya hivyo? Ninauliza swali hili kwa sababu Wamarekani wa Nyalandu waliitisha ndege haraka-haraka wakakimbia na kuarejea kwao mara tu waliporipotiwa na Gazeti la Jamhuri kwamba walikuwa porini kule Ziwa Natron wakiwinda kwa (Leseni ya Rais) Leseni Maalum na kwamba walikuwa wakifanya hivyo kwenye kitalu ambacho hakikuwa cha kwao kisheria. Katika Taarifa yake kwa Umma, Nyalandu ameshindwa kutueleza Watanzania ni kwa nini Wamarekani wake walikimbia na ni kwa nini hawakuendelea na uwindaji wao. Si walikuwa wanafanya hivyo kisheria na kihalali katika nyanja zote na, kwa maelezo ya Nyalandu, walikuwa wamelipia? Kwanini wakimbie baada ya kuandikwa?

Nyalandu anaeleza katika Taarifa yake kwa Umma kuwa, “Vibali vilivyotajwa na Gazeti la Jamhuri la tarehe 19/08/2014, Toleo la 150 vilitolewa kwa familia ya Freidkin ya watu wanane (8) kwa ajili ya uwindaji kuanzia tarehe 1 hadi 21 Agosti 2014 kwenye vitalu vya Lake Natron, Makao open na Makao Wildlife Management Area (WMA), Maswa Kimali na Maswa Mbono kupitia kampuni ya Tanzania Game Trackers Safaris Ltd.”

Anaeleza pia kuwa, “Maeneo hayo yaliyowindwa hayahusiani na ugawaji wa vitalu kama ilivyoelezwa na Gazeti la Jamhuri ya kuwa Waziri Nyalandu amegawa vitalu zaidi ya vitano kwa kampuni moja.”

Watanzania tusidanganywe kwa maneno ya kufunikafunika. Nyalandu anazo ‘kesi’ za kujibu angalao nne hapa. Moja ni kunyang’anya vitalu kampuni zilizogawiwa kisheria na kihalali na kuwahonga Wamarekani wake kwa kuvunja sheria wazi wazi, sheria anazopaswa kuzisimamia yeye. Hili amekwepa kulijibu.

Pili, ni kujichukulia mamlaka ya kugawa kitalu kinachomilikiwa na jumuia ya vijiji (Makao WMA).

Tatu, ni kugawa kwa kampuni moja kwa makusudi vitalu vingi zaidi ya vile vilivyoruhusiwa kisheria – sheria iko wazi kabisa juu ya hili. Hili nalo amekwepa kulitolea maelezo.

Na nne, tuna taarifa kuwa utaratibu ni kwamba wanaopatiwa Leseni Maalum kwa maslahi ya taifa huwinda kupitia kampuni zilizopo kisheria na katika vitalu vilivyopo kisheria. Nyalandu aweke wazi orodha ya vitalu vilivyotengwa kisheria na kampuni zilizogawiwa na aueleze umma kama Makao Open ni kitalu kilicho kwenye orodha hiyo. Kama kitalu hicho hakimo kwenye orodha aueleze umma kakikitoa wapi, kwa utaratibu upi na kwa mamlaka yapi ya kisheria. Taratibu za kutenga vitalu vya uwindaji zinajulikana.

Nyalandu anakanusha tuhuma kuwa: “amekiuka kifungu kinachoweka ukomo wa idadi ya vitalu ambavyo ni vitalu vitano kwa kampuni.” Ukweli utadhihirika Nyalandu atakapotoa hadharani orodha ya vitalu vyote na wamiliki wake, baada ya mabadiliko aliyoyafanya kinyume cha sheria kwa kuwahonga Wamarekani wake.

Kifungu 58(3) cha sheria na. 5 ya 2009 kinasema: “A special licence granted under subsection (I) shall not be used for commercial purposes or personal gain.” Kwa tafsiri isiyo rasmi kinasema kuwa Leseni Maalum inayotolewa chini ya kifungu kidogo cha 1 kamwe kisitumike kwa malengo ya kibiashara au kupata faida au manufaa binafsi. Ndivyo sheri inavyosema.

Ninaamini kuwa alipokuwa anaandaa au anaandaliwa Taarifa yake kwa Umma kukanusha tuhuma dhidi yake, Nyalandu alikisoma kifungu hiki pia – kumbuka kuwa alisoma na kukitumia kifungu 58(1) katika maelezo yake. Cha kushangaza ni kuwa, kwa makusudi, ameepa kuueleza umma kama alichowaruhusu Wamarekani wake wafanye hakikuwa kwa malengo ya kibiashara au manufaa binafsi kwao na yeye.

Nyalandu amekwepa kulitolea maelezo hili kwani anajua wazi kuwa walikuwa wanawinda kwa angalao lengo mojawapo kati ya hayo – biashara au manufaa binafsi. Kwa maana hiyo uwindaji wao ulikuwa kinyume cha Sheria Namba 5 ya mwaka 2009. Nyalandu analijua hilo. Alijua kuwa kwa kuwapa kibali hicho alikuwa anavunja sheria ya nchi anayopaswa kuisimamia, lakini kwa sababu ya kiburi aliamua kuivunja sheria hiyo ili kuwafurahisha rafiki zake Wamarekani.

 

Katika Taarifa yake kwa Umma Nyalandu anadai kuwa Wamarekani wake hawakuwinda simba wala wala tembo wanane aliowaruhusu, eti kwa kuwa waliowaona wote hawakuwa wamefikia ubora unaotakiwa. Na, kwa hiyo, anadai kuwa tuhuma zilizotolewa kwake ni za uongo. Huyu ni waziri wa ajabu kweli kweli.

Maelezo haya yanathibitisha kutapatapa kwa Nyalandu kwani, Gazeti la Jamhuri katu halikuripoti kuwa simba na tembo hao walikuwa wamewindwa, bali kwamba kibali kilitolewa wawindwe na wawindaji walikuwa porini wakiwawinda. Na, ni wazi kwamba, hawakuwindwa kwa sababu wawindaji waliamua kukatisha uwindaji wao na kukimbia, baada ya taarifa zao kuripotiwa na Gazeti la Jamhuri. Kule kukimbia tu ni uthibitisho kwamba walikuwa wakifanya uhalifu. Hili Nyalandu analijua na amekwepa kwa makusudi kulitolea maelezo.

Nimeeleza hapo juu kuwa, kwa makusudi, Nyalandu ameepa kuwaeleza Watanzania kama alichowaruhusu Wamarekani wake wafanye hakikuwa kwa malengo ya kibiashara au manufaa binafsi kwao na/au yeye.

Ninaamini kuwa Nyalandu alijua fika kuwa, kutokana na ujangili wa tembo kukithiri hapa nchini, tembo wachache waliosalia ni wadogo wadogo, ambao hawawezi kufikia viwango vya ubora vilivyowekwa kisheria. Swali alilokwepa kujibu ni, kwa nini, pamoja na kufahamu hivyo, bado aliwapa kibali familia moja wawinde tembo wanane? Haelezi pia meno 16 ambayo yangepatikana yangepelekwa wapi na Wamarekani hao wakati inaeleweka kuwa wasingeyaingiza nchini kwao kutokana na kupigwa marufuku. Kwa mujibu wa Shirika la Samaki na Wanyamapori la Marekani (US Fish and Wildlife Service – USFWS), hatua hiyo imechukuliwa na Marekani kutokana na usimamizi unaotia shaka, kushindwa kusimamia sheria na utawala mbaya katika sekta ya maliasili nchini Tanzania kiasi cha kusababisha wanyamapori, hasa ndovu kupungua mno.

Je, mtu akidai walikuwa wanamwindia yeye atasemaje?  Si tumesoma na kusikia kwenye vyombo vya habari kuwa na yeye ni mtuhumiwa wa ujangili?

 

Taarifa ya Nyalandu kwa Umma indai kuwa: “Idadi ya wanyamapori wanaotolewa kwenye leseni yoyote kupitia kampuni za uwindaji wa kitalii hutolewa kwa kufuata ‘Safari Package”’. Ni vizuri analitambua hilo, kama hakuandaliwa tu Taarifa yake kwa Umma. Lakini sentesi hii inazua maswali mengi. Kama Wamarekani hawa walinunua ‘Safari Package’ kama wawindaji wengine wowote – Nyalandu amesema walilipia ada zote – ilikuwaje wakapewa Leseni Maalum/Leseni ya Rais? Kama walinunua ‘Safari Package’ na kuwindishwa na kampuni ya uwindaji wa kitalii, ilikuwaje Nyalandu awaruhusu kuwinda nje ya vitalu vilivyotengwa rasmi kwa uwindaji huo? Kwa nini Nyalandu alitoa kibali kwa mtoto mdogo (chini ya umri unaoruhusiwa) kuwinda hali akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria? Ikumbukwe kuwa adhabu aliyoitoa kwa kampuni ya Green Mile ilitokana, pamoja na mambo mengine, kuwindisha watoto.

Nyalandu anaeleza kuwa: “Tanzania imekuwa ikiwinda tembo 50 kwa miaka ya 1990 na baadaye kwenye miaka 2000 tembo 200 idadi ya tembo ilipoongezeka. Hata hivyo, mwezi Juni 2014 Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii alipunguza idadi hiyo kwa asilimia 50 kutokana na kupungua kwa idadi ya tembo wenye ubora wa  kuwindwa.”

Kwanza, kwa kuwa Waziri anatambua kushuka kwa idadi ya tembo na kupungua kwa ubora wa nyara zao, tulitegemea Nyalandu, kama Waziri mwenye dhamana, angesitisha uwindaji wa tembo. Huenda Taarifa yake kwa Umma hapakuwa mahali mwafaka kwake kutoa maelezo hayo. Hata hivyo, tulitegemea kuwa, baada ya maelezo yake hayo, Nyalandu angetueleza Watanzania sababu za yeye kutoa asilimia nane (8%) ya alioruhusu wawindwe kwa mwaka kwa familia moja tu, tena ya rafiki zake.

Kuhusu anayoiita: “Tuhuma ya Kuruhusu wageni kuwinda katika vitalu ambavyo siyo vya kampuni husika”; Nyalandu anadai kuwa si za kweli na kudai kuwa: “Tuhuma hizi zina nia ovu ya kudhoofisha kasi ya kupambana na ujangili.” Hili linaweza kumfanya hata bubu akaongea. Kwanza kuruhusu wageni kuwinda katika vitalu visivyomilikiwa na kampuni husika haina uhusiano hata kwa mbali na suala la ujangili. Sasa unajiuliza kama Nyalandu na aliyemsaidia kuandika walikuwa hawana usingizi wakati wanaandaa Taarifa yao kwa Umma. Kwa ufupi utetezi uliotolewa, kwa lugha ya John Cheyo (Mzee Mapesa), ni OUT. Lakini pia Watanzania mtakumbuka kuwa utetezi huu umekuwa ndio wimbo wa Nyalandu tangu alipoanza manjonjo yake. Kila linalosemwa dhidi yake utetezi mara zote ni kuwa wanaomsema wana nia ovu ya kudhoohofisha kasi yake ya kupambana na ujangili. Hiki sasa kinageuka kuwa kichekesho.

Kama yuko bize na kusaka na kuwakamata majangili popote walipo mbona hajamkamata pweza tuyeambiwa? Anapambana na majangili wapi wakati aliodai anawafahamu hajatukamatia? Je, sasa tembo hawauawi? Mbona tunaambiwa kuwa anawanyamazisha wanahabari wasiandike habari za mauaji ya tembo asijekuonekana kashindwa? Wiki mbili zilizopita wameuawa tembo wakubwa watatu mkoani Mara, na wengine wa idadi kama hiyo wameuawa wiki iliyopita Makuyuni, Arusha. Habari haziandikwi kwa sababu baadhi ya wanahabari ameshawaziba midomo ili wasitangaze wala kuandika na hatimaye akaonekana amefeli licha ya tambo zake nyingi. Watanzania tuamke, vinginevyo kwa Nyalandu tutavuna mabua.

By Jamhuri