Mojawapo ya makubaliano ya mwafaka yaliyoafikiwa baina ya wakulima na wafugaji iliweka utaratibu wa kuzuia migogoro na migongano baina yao kwa wao. Makubaliano hayo yalitekelezwa kwa wahusika kutenga mipaka ya maeneo ya kuendesha shughuli za wakulima na wafugaji. Mwafaka wa aina hiyo umeendelea kudumishwa na makabila yote. Kwa mfano wa Wasukuma au Wahehe (na makabila mengine yote) miongoni mwao kuna ambao ni wakulima, wengine wafugaji. Kutokana na jadi ya mwafaka makundi ya wakulima na wafugaji hao hupangiana mipaka ya kuendeshea shughuli zao za kimaisha. Ni kwa sababu hiyo kwamba mapigano yanayovuma sana hivi leo nchini kote kati ya wakulima na wafugaji kamwe hayahusu wala kusumbua Serikali katika jamii za aina hiyo. Tatizo lililokuwa likitokea na hivyo hadi leo hii ni wizi wa mifugo au mazao ya mashambani miongoni mwa jamii ya makundi hayo. Wizi huo hutokana na hulka binafsi ya mtu mmoja mmoja; tatizo ambalo huwa kosa la kijinai. Vinginevyo ni marufuku kwa mtu yeyote kuvunja makubaliano ya mwafaka ulioafikiwa kupanga maeneo ya shughuli za maisha ya makundi hayo mawili. Kila mwanajamii alitambua na hutambua kuwa mwafaka hulenga kuhakiki kuwepo kwa amani na utengemano wa kudumu miongoni mwao.

 

Baada ya vita Kuu ya Kwanza 1914

Baada ya Wajerumani kurudi makwao 1917 Gavana wa kwanza wa Uingereza Horace Byatt; aliafiki uamuzi wa watangulizi wake kupanga mipaka ya wilaya za kuishi makundi mbalimbali ya wenyeji. Lakini alikwenda mbali zaidi kuhusu Wamasai kwa kuwapangia HODHI ya malisho yao [(Umasaini – Monduli) wakiungana na Wamasai wenzao kutoka Kenya] na kuamuru kuwa wasivuke mipaka yao kwenda wilaya za wakulima. Gavana wa pili wa Tanganyika alikuwa Donald Cameron ambaye alikuwa mtu mwenye mawazo mapana ya kutaka kuwawezesha Wafrika “kusimama peke yao” kwa misingi iliyokuwa imeamuliwa na Jumuia ya Muungano wa Mataifa. Cameron alitumwa na Uingereza kuwa Mtekelezaji Mtukuka wa sera za uoanishaji wa demokrasia ya kisasa ya Uingereza na demokrasia-shirikishi ya kweli ya Wafrika ya mwafaka. Ndiye mwasisi wa mfumo wa serikali za mitaa ambao unatumika hadi leo hii Tanzania.

Baada ya kuuchambua kizamilifu mfumo wa mwafaka; Cameron alipania kutekeleza uoanishaji (grafting-in) kwa vitendo na kidhati. Aliuita mfumo wa oanisho hilo Mfumo wa Serikali za Mitaa za Kiafrika (asili uamuzi wa Jumuia ya Muungano wa Mataifa). Yeye aliamini kuwa mfumo huo wa namna ya kipekee kabisa ndio ungeliwawezesha wenyeji wa Tanganyika kuishi “kwa upendo, mshikamano na tumaini” kwa kuwa mfumo huo ulimfanya kila Mwafrika kupewa hadhi na haki yake. Tamanio kuu la panio lake likawa kwamba mfumo huo ungelitumika na Serikali Kuu ya Tanganyika na Legco (Bunge) jambo ambalo lingeliwezesha kuwa na Madiwani-Bunge (sio kama sasa Wabunge-Diwani) kutoka kwenye halmashauri za Serikali za Mitaa za Kiafrika kuingia Bungeni lengo likiwa kuanzisha demokrasia-shirikishi ya kweli nchini. Alikusudia kwamba mfumo wa Serikali Kuu ya Kiafrika na Serikali za Mitaa za Kiafrika  kutoka Tanganyika ungeliigwa na kunukuliwa na nchi zote za Afrika Mashariki, Afrika ya Kati na Bara lote la Afrika ili kusimika umoja, upendo, mshikamano na ushirikiano wa dhati miongoni mwa Wafrika kila watu nchini kwao. Cameron alitaka mfumo wa Serikali za Mifaa za Kiafrika kutoka Tanganyika uwe ndio “mwenge” wa kuigwa na nchi zote za Afrika (Cameron 1939 – My Tanganyika Service and some Nigeria). Yeye anasema kwamba ni Gavana wa Southern Rhodesia (Zimbambwe) pekee aliyekubali wazo hili lakini magavana wengine walikirihi jambo hilo.

Aliuona Mfumo wa Serikali za Mitaa za Kiafrika kama mwenge ambao ungeliwashwa Tanganyika kama kizio cha umoja miongoni mwa makundi mbalimbali ya wenyeji wa mataifa yao. Labda mapigano na magomvi yanayorindima Kti ya wananchi na ndugu zao katika nchi nyingi za Afrika huru imafaima mapigano kati ya wakulima na wafugaji nchini Tanzania hivi sasa yote YANGELIYEYUSHWA na “mwenge wa upendo, umoja, mshkamano na tumaini” kama yangeiga mfumo wa Serikali Kuu za Kiafrika na Serikali za Mitaa za Kiafrika za Tanganyika alioupaniia Cameron miaka zaidi ya 90 iliyopita. 

Mojawapo ya maeneo ya maoanisho kutokana na kusudio la Cameron lilikuwa kufanikisha azma ya mwafaka wa kijadi iliyotumika kuzuia migogoro na ugomvi kati ya wakulima na wafugaji kwa kupangia mipaka mahsusi kati ya makundi hayo mawili kwa misingi ilivyoelezwa hapo juu. Alifanya hilo kimatendo kwa kutunga Sheria ya Sura 72 tarehe 1 Februari 1927 iliyoitwa Native Authority Ordinance. Wakati wa kutunga sheria hiyo alichimbia vifungu kadhaa vyenye lengo la kuiwezesha Serikali kupunguza wigo wa uhuru wa wenyeji kuondoka kwenye maeneo ya mipaka (maskani) yao kuhamia mahali pengine. Kwa mfano Kifungu cha 9 (i) na (l) cha sheria hiyo kilielekeza ifuatavyo:-

“ … Mamlaka  ya wenyeji (yaani machifu) yaweza … kutoa amri kwa njia ya tamko au kwa maandishi; amri ambazo hazina budi kwa kila mwenyeji au wenyeji wote kuzitii wanaoishi katika eneo la milki ya himaya ya mamlaka ya wenyeji husika … kwa madhumuni yafuatayo:-

Kupiga marufuku, kuweka mipaka au kudhibiti kitendo cha uhamaji wa wenyeji kutoka au kuingia ndani ya eneo lililo chini ya himaya ya mamlaka (chifu) ya wenyeji;

Kupiga marufuku, kuweka mipaka au kudhibiti uzururaji au kupitisha kwa mifugo kuingia au kupitia ndani ya eneo la himaya yake pasna idhini yake kwa mujibu wa madaraka yake”.

Sheria hiyo iliainisha upeo wa madaraka ya machifu (Serikali za Mitaa za Kiafrika) walivyotakiwa kutoa amri zilizowazuia au kuwapunguzia wenyeji wigo wa uhuru wa kwenda kuendesha shughuli zao za kimaisha popote walipotaka bila ‘kibali’ cha mamlaka hizo. Sheria hiyo iliendelea kutumika hadi mwaka 1953 wakati Gavana Twining alipofanyia marekebisho na kukazia Sheria hiyo kwa kutunga Sura 333 mwaka 1954. Wakati wa marekebisho hayo maelekezo yaliyoainishwa hapo juu (kuhusu upangaji wa mipaka) yaliboreshwa kwa kuziwezesha Halmashauri za Serikali za Mitaa kutunga (mbadala wa machifu) Sheria Ndogo Ndogo (Bye Laws) za kudhibiti muingiliano kati ya wafugaji na wakulima. Jambo hilo lilielekezwa kwa mujibu wa Kifungu cha 52 (1) (II) cha Sura 333 kwamba:-

”… mamlaka ya serikali za mitaa italazimika au itaweza kushughulikia …  jambo lifuatalo … katika eneo la himaya yake:-

(II) kupiga marufuku, kudhibiti au kuwekea mipaka uzururaji au kupitisha kwa mifugo ndani ya eneo la himaya yake”.

Ni kutokana na maelekezo haya kwamba Amri za tangu 1927 ziliendelea kutekelezwa wakati wote wa udhaminisho wa Uingereza hadi siku ya Uhuru. Kwa mfano Wamasai hawakuwahi kuvuka mipaka ya HODHI yao kuhama na mifugo yao kwenda nje ya eneo lao walakini wao wenyewe wangeliweza kwenda kuishi popote walipotaka. Mamlaka za serikali za mitaa ziliimarishwa sana katika kipindi hicho kuziwezesha kutekeleza majukumu yao ilivyopasa.

Baada ya uhuru Wamasai na Mifugo yao wavuka mipaka ya HODHI na kusababisha migogoro mingi na wakulima

Mara tu baada ya uhuru, Wamasai wafugaji walielimishwa na wanachama wa TANU na Serikali Kuu kwamba wao kama Watanganyika wengine walikuwa huru kwenda kuishi mahali popote pale nchini. Walielewa vizuri na kufurahia tafsiri ya Ibara ya 17 (i) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika (hivi sasa ya Tanzania) inayoelekeza kwamba:-

“Kila raia … anayo haki ya kwenda kokote katika Jamhuri ya Muungano na kuishi katika sehemu yoyote … katika Jamhuri ya Muungano”.

 

>>ITAENDELEA>>

 

Mwandishi wa makala hii, Jeremiah Kilembe ni mtumishi mstaafu wa Serikali za Mitaa. Anapatikana kupitia barua pepe: jckilembe@gmail.co

Simu: 0685214691

2239 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!