Tendawili: Tega! ‘Ananifanya nichukiwe na kila mtu.’ Jibu ni ‘Majivuno’.
Majivuno ni jeraha lisiloponyeka katika maisha. Ni donda ndugu. Machi, 12-16 Agosti, 2013, Jarida la ‘New People’ la nchini Kenya, lilichapisha makala yangu iliyokuwa inasema, ‘Holy family’’. Padre Erickson Wangai wa Jimbo Kuu Katoliki la Nairobi alibahatika kusoma makala ya ‘Holy family’.

Padre Erickson baada ya kuisoma makala ile, alinitumia ujumbe mfupi kwa njia ya barua pepe. Katika ujumbe huo aliandika hivi: ‘Binadamu hawezi kuishi bila upendo, lakini anaweza kuishi bila majivuno’.
Katika makala hii nitapata fursa ya kutafakari umuhimu wa kuishi maisha ya upendo, na hasara ya kuishi maisha ya majivuno.
Ninakualika wewe uliyepata fursa ya kusoma makala hii tusafiri pamoja katika hali ya ukimya na tafakuri mwanana. Mwanateolojia wa Kanisa Katoliki, Augustino wa Hippo, anasema; Majivuno yaliwabadili malaika wakawa mashetani. Unyenyekevu huwafanya watu wawe kama malaika. Swali ambalo unaweza kuniuliza ni hili; Nifanye nini ili niishi maisha yanayoongozwa na unyenyekevu na siyo majivuno?
Usiwe na shaka jibu linapatikana, tunasoma hivi katika Maandiko Matakatifu; Kila ajikwezaye atashushwa, na kila ajishushaye atakwezwa (Lk 14:11). Ukijishusha utainuliwa ukijikweza utashushwa.
Kwa upande mwingine Mwanateolojia Augustino wa Hippo anatoa ushauri huu, Mungu ni mwenye uwezo wa juu sana, jinyenyekeze atakushukia, lakini ukijitukuza atakukimbia. Dhambi kubwa sana ambayo iliwahi kutokea huko mbinguni na ambayo inatendeka hapa duniani ni majivuno.

Majivuno yaliwabadilisha malaika wakawa mashetani. Majivuno yalimwondoa malaika Lucifer mbinguni. Lucifer kabla hajaondolewa mbinguni kwa sababu ya majivuno yake alikuwa Malaika Mkuu. Muulize kilichomtokea baada ya kuwa amekumbatia majivuno.
R. Newton anaandika, ‘Ngoja nikupe historia ya majivuno katika sura fupi tatu. Mwanzo wa majivuno ulikuwa mbinguni. Mwendelezo wa majivuno ni duniani. Mwisho wa majivuno ni motoni.
Historia inaonesha majivuno ambavyo yanaleta karaha. Majivuno yanakutoa sehemu nzuri na kukupeleka sehemu mbaya. Majivuno hujenga ukuta kati ya watu, unyenyekevu hujenga daraja.

Unyenyekevu ni mafuta yanayolainisha na kuvuta mahusiano. Padre Dkt. Faustine Kamugisha anasema; Majivuno si ushindi hata kidogo. Kanuni ya kwanza ya mafanikio ni unyenyekevu. Ya pili ni unyenyekevu. Ya tatu ni unyenyekevu.
Na kanuni ya kwanza ya kushindwa ni majivuno. Ya pili ni majivuno. Ya tatu ni majivuno. Tuepuke kuishi maisha ya majivuno. Mwandishi Nadeem Kazi anatufundisha kwamba hatuwezi kupanda juu kwa kuwashusha wengine chini.
Tunapanda juu kwa kuwasaidia wengine kupanda. Katika maisha lazima pia tujifunze kuwasaidia wengine. Huwezi kufanikiwa kiroho, kiuchumi, kifamilia, kiutawala, kielimu, kimaadili na kiafya kwa kuwaangusha wengine chini.
Yule anayejitolea kuwasaidia wengine ndiye huinuliwa na watu aliowasaidia kuinuka. Bila shaka umewahi kujiuliza; Kwa nini fulani amefungua biashara yake lakini imestawi kwa miaka michache halafu ikafa?
Napenda nilijibu swali hili katika mada hii tunayoendelea nayo. Iko hivi, mtu yeyote anapoanzisha biashara au mradi huwa ana unyenyekevu na upole wa hali ya juu sana kwake yeye mwenyewe na kwa wasaidizi wake kama anao na kwa wateja wake pia. Mara biashara inapostawi, majivuno yanaota mizizi.

Majivuno yanapoota mizizi na kukomaa anaanza kuwaona wafanyakazi wake kama vikaragosi. Anawadharau. Huo ndiyo unakuwa mwanzo wa anguko la biashara yake ama mradi wake. Padre Yohane Vianei ni padre Mkatoliki aliyeishi maisha ya unyenyekevu sana. Siku moja alipata barua mbili ambazo haijulikani ziliandikwa na nani.
Barua moja ilimtaja kama Mtakatifu, barua nyingine ilimtaja kama mnafiki na mpiga porojo. Padre Vianei baada ya kuisoma barua ya kwanza alisema hainiongezei chochote. Ya pili alisema, hainipunguzii chochote, mbele ya Mungu tunapimwa kwa kuishi maisha ya unyeyekevu.

Mimi najitahidi kuishi maisha ya unyenyekevu ili nipate nafasi katika ufalme wa Mungu. Maisha ya majivuno hayana faida yoyote, isipokuwa yana hasara isiyolipika kwa urahisi. Mwandishi James Mathew Barrie anasema; Maisha ni somo refu katika unyenyekevu.
Tuishi maisha yanayotawaliwa na upendo. Maisha ni upendo. Maisha yanazungumza katika upendo. Ukitaka kuuona upendo ishi upendo. Upendo ni lugha ambayo kiziwi anaweza kuisikia na ambayo kipofu anaweza kuiona. Uruhusu upendo uyatawale maisha yako. Usiruhusu hata siku moja ipite pasipo kupanda mbegu ya upendo wa kweli, upendo usio wa kinafiki, upendo utokao moyoni na upendo ushindao majaribu. Yesu Kristo aliwahimiza wanafunzi wake kwa nasaha hii, Pendaneni kama nilivyowapenda ninyi (Yn 13:34).
Ni lazima tujitahidi kuyajenga maisha yetu katika msingi wa upendo. Furaha kamili ipo katika kuishi maisha ya upendo. Tupendane. Mwandishi Freidrich Rucket anasema, upendo ni kitu kikubwa sana ambacho Mungu anaweza kutupa, na kitu kikubwa sana ambacho tunaweza kumpa Mungu.

Katika makala hii ninaomba tupate fursa ya kutafakari maisha yetu. Sisi sote tulio dhaifu kiroho, kimwili, kiakili, kiutashi na kimapendo tunahitaji huruma ya Mungu. Tunahitaji huruma ya Mungu ili maisha yetu na matendo yetu yaongozwe na tabia ya upendo. Lengo letu la kwanza katika maisha ni kuwasaidia wengine, kama hatuwezi kuwasaidia wengine basi tusiwaumize.
Fumbua macho yako utazame. Tazama upya mahusiano yako na Mungu wako. Tazama upya mahusiano yako na mke/mume wako. Tazama upya mahusiano yako na watoto wako. Tazama upya mahusiano yako na majirani zako. Tazama upya uhusiano wako na kazi yako. Tazama upya mahusiano yako na wafanyakazi wenzako. Baada ya kutazama umebaini nini?

Je, umebaini kasoro za kimahusiano? Jifunze kumwomba msamaha aliyekukosea na uliyemkosea pasipo kusita. Siku yako ya ushindi ni siku ile unayomwomba msamaha aliyekukosea na uliyemkosea. Kumbuka: Mungu anakutafuta ili urekebishe mambo ambayo hayaendi sawa. Usikate tamaa bado unayo nafasi ya kuboresha mahusiano na Mungu wako, mke wako, watoto wako, jirani zako na wafanyakazi wenzako.
Upendo ni nguvu ya Kimungu inayomwezesha kila mmoja wetu kushinda hofu yake ya upweke na kujiunga na wengine, lakini wakati huo huo bila kupoteza hadhi yake au ya wengine na kubaki hivyo daima. Upendo kwa hiyo unaonekana kama sharti la kibinadamu ambalo linamwokoa mtu kutoka katika maisha ya janga la kujitenga na wengine na kumwongoza katika maisha ya kuunganika na wengine.
Hebu tuone kinyume cha neno upendo yaani chuki. Tujiulize swali hili kwa usikivu mwanana. Hivi ni nani kati yetu binadamu tulio hai anaweza kuishi maisha ya chuki halafu akawa na amani katika nafsi yake? Ni nani kati yetu binadamu tulio hai anaweza kuishi maisha ya chuki halafu akawa mpatanishi wa amani katika taifa lake au familia yake?

Nani anafahamu mzigo wa chuki? Pengine unaweza ukawa hufahamu mzigo wa chuki. Niulize nikwambie, chuki ni sumu isiyo na tiba ya kisayansi wala tiba ya kiasili. Tiba ya chuki ni upendo. Njia rahisi ya kuepuka chuki ni kuishi maisha ya upendo.
Mwanaharakati Martin Luther King Jr anasema, nimeamua kujishughulisha na upendo. Chuki ni mzingo mzito sana ambao haubebeki. Upendo ni mzigo mwepesi ambao unabebeka.
Mtawa wa Kanisa Katoliki Mt. Fransisko wa Asizi alipata kutunga Sala ya kusali kila siku. Sala hii ilimfaa yeye kwa wakati wake, inakufaa wewe kwa wakati wako na inanifaa na mimi kila wakati. Alisali hivi;
Bwana nifanye niwe chombo cha amani.
Mahali palipo na chuki nilete upendo.
Mahali palipo na ghadhabu nilete msamaha.
Mahali palipo na utengano nilete umoja.
Mahali palipo na wasiwasi nilete amani.
Mahali palipo na uongo nilete ukweli.
Mahali palipo na kukata tama nilete tumaini.
Mahali palipo na huzuni nilete furaha.
Mahali palipo na giza nilete mwanga.

0719700446

By Jamhuri