Uvimbe na kutokwa damu kwenye njia ya haja kubwa

Unaweza kuhisi una uvimbe mdogo sehemu ya nje ya njia ya haja kubwa inayoambatana na muwasho na maumivu na wakati mwingine ukienda haja kubwa, kinyesi kinatoka kwa tabu sana na kadri unavyotumia nguvu kukisukuma ndipo maumivu kwenye ile njia ya haja kubwa yanazidi kuwa makali zaidi na hata kinyesi kikitoka kinachanganyika na damu. Hili ni tatizo la kiafya ambalo kitaalamu linaitwa ‘Hemorrhoids’. cha kusikitisha ni kwamba wagonjwa wengi hawapati tiba sahihi inayostahili kwa kuwa wanaona aibu kuwaona watoa huduma wa afya kwa ajili ya ushauri na tiba kutokana na namna tatizo lenyewe lilivyo na kuishia kwenye maduka ya dawa na kununua dawa bila ushauri wa daktari kwa matumaini ya kulikabili tatizo. Ni vyema kutambua ukweli kwamba, kutokwa damu sehemu za siri kunahitaji msaada zaidi wa daktari kuliko kutumia bila ushauri bila kujua chanzo hasa cha tatizo.

Wajawazito wanakua hatarini zaidi kupata tatizo hili. kadri mimba inayvoongezeka kukua, mwanamke hupata mabadiliko mbalimbali ya kimaumbile likiwemo mfuko wa uzazi kupanuka na kuongezeka uzito na kusababisha mkandamizo kwenye utumbo mpana. kadhalika wazee kutokana na mfumo wa kinga mwilini kufifia kunakotokana na sababu za kiumri. Lakini tusisahau kua tatizo hili linaweza kumpata mtu yeyote, sio mjamzito au mzee tu. Mtu anapopatwa na tatizo hili, mara nyingi kwenye sehemu ya ndani ya ngozi ya njia haja kubwa huvimba na kutokeza nje na kuambtana na maumivu makali wakati wa haja kubwa, na haja kuambatana na damu pia.

Tatizo hili linatibika iwapo mgonjwa atapata msaada wa kitabibu mapema hivyo mgonjwa anashauriwa kumuona daktari haraka mara tu aonapo dalili za awali kama vile, kutokwa na damu kusikoambtana na maumivu au maumivu ya kawaida, muwasho ndani na nje ya sehemu ya haja kubwa, maumivu kwenye sehemu ya haja kubwa hasa wakati ukiwa umekaa, kuhisi uvimbe sehemu ya haja kubwa na kuhisi sehemu ya ndani ya haja kubwa imetokeza nje. Mtu yeyote anaepitia dalili hizi anapaswa kumuona daktari haraka.
Naomba ifahamike kuwa, baadhi ya matatizo makubwa ya kiafya kama vile saratani ya utumbo na saratani ya njia ya haja kubwa zinasababisha utokaji damu sehemu ya haja kubwa hivyo ni kosa kubwa kubwa sana kudhani kuwa, kutokwa na damu kwenye njia ya kubwa ni tatizo la kawaida tu na hivyo kupuuzia kupata ushauri wa daktari. Wakati mwingine mgonjwa hulazimika kufanyiwa upasuaji mdogo iwapo anakua amechelewa kupata tiba kwa muda sahihi.

Tatizo hili linatokea wakati ambapo mishipa midogo midogo kwenye njia ya haja kubwa hutanuka na kusababisha ngozi ya sehemu ya ndani ya sehemu ya haja kubwa kutokeza nje kutokana na maambukizi mbalimbali.
Sababu nyingine kubwa zinasababisha tatizo hili ni mwili kukosa kiwango stahiki cha maji. Mwili unahitaji kiasi cha kutosha cha maji ili chakula kiweze kumeng’enywa vizuri tumboni, hivyo upungufu wa maji mwilini unaweza kuathiri mmeng’enyo wa chakula na hivyo kusababisha mtu kutoa kinyesi kigumu ambacho sasa kutokana na ugumu wake kinasababisha michubuko kwenye njia ya haja kubwa wakati wa kutoka na michubuko hii hatimae inasabaisha maambukizi. Ulaji wa mboga za majani na matunda kwa wingi unasaidia kukabiliana na tatizo hili kutokana na nyuzi lishe zinazopatikana kwenye kundi hili la vyakula.