Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya MNM Engineering Service Ltd, Mhandisi Godwin Mshana aliyejenga ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu cha Mkwawa (MUCE) cha mjini Iringa amefikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka matatu yanayomkabili, likiwamo shtaka la uhujumu uchumi.

Mhandisi huyo alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa jana na kusomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi, David Ngunyale.

Akisoma mashtaka hayo, Wakili wa Serikali, Blandina Manyamba alisema mshtakiwa anakabiliwa na makosa ya uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara ya TZS 2 bilioni, kughushi nyaraka na kujipatia TZS 3 bilioni kwa njia ya udanganyifu.

Wakili aliiambia mahakama kuwa mtuhumiwa huyo alitenda makosa hayo kati ya mwaka 2010 na 2012 wakati wa ujenzi wa ukumbi wa mikutano chuo cha MUCE.

Upande wa mashtaka ulisema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Upande wa utetezi haukutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi.

Mshtakiwa amepelekwa mahabusu na shauri hilo limeahirishwa hadi Mei 22 mwaka huu.

Mshana alikamatwa Mei 3 mwaka huu kufuatia agizo lililotolewa Mei 2 chuoni hapo na Rais Dk John Magufuli la kufuatilia madai ya kuwepo kwa ubadhirifu wa fedha katika ujenzi wa ukumbi huo liogharimu TZS 8 bilioni.

1803 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!