TANGA

Na Oscar Assenga

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima, amewatumia salamu mawakala wa wahamiaji haramu ambao wanautumia mkoa huo kuwapitisha na wale wanaopitisha dawa za kulevya, akionya wasijaribu kufanya hivyo, maana watakachokutana nacho kitakuwa historia kwao.

Malima ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Tanga ambapo amesema mkoa huo hautakuwa njia ya kupitisha wahamiaji haramu na kama kuna watu wanadhani anatania wafanye hivyo waone watakachokumbana nacho.

Amesisitiza kuwa Tanga kamwe haitakuwa sehemu ya vitendo haramu nchini na kwamba yeye na timu yake wamejipanga kuhakikisha vitendo vya namna hiyo havifanyiki mkoani humo.

“Ndani ya wiki mbili wahamiaji haramu wameongezeka, naomba wasiufanye Mkoa wa Tanga kuwa ni dezo ya wao kupitia, na niwaambie kwamba Tanga hautakuwa mkoa wa kupitisha mauzauza yao na hata wale ambao wanafikiria kwamba wanaweza kupitisha dawa za kulevya wasijaribu zari, kwani tumejipanga kuwashughulikia,” anasema.

Anasema wahamiaji haramu hao hupitia Tanga kwenda mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na Bagamoyo, kwa hiyo amewataka waandishi wa habari kufikisha salamu kwa wanaojijua wazi kwamba hushiriki katika biashara ya kusafirisha binadamu.

Anasema ‘shehena’ hiyo huchukuliwa Mkinga na aghalabu husafirishwa usiku kwa usiku.

“Njia na mbinu zao tunazifahamu. Watu hawa wanaoshiriki kusafirisha binadamu huwatoa Wilaya ya Mkinga na kuwasafirisha usiku kwa usiku!

“Wengine wanapita Korogwe, wanatokea Kilindi, wanachana Korogwe hadi Handeni. Wanapitia Mkata kisha wanaingia Pwani.

“Wengine wanatokea Mvomero, pia kuna eneo la Gairo. Hilo ni tatizo kubwa na hawawezi kufanikiwa kama hawana watu ambao wanashirikikiana nao,” anasema.

Mkuu huyo wa mkoa amewataka waandishi wa habari Mkoa wa Tanga kufikisha ujumbe kwamba wale wanaotumika kufanikisha biashara hii haramu, wafahamu kuwa huenda dhambi ya kusafirisha ni kubwa sana kuliko kusafirishwa.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake. Kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Judica Omari

By Jamhuri