TASAF yajipanga kuongeza umakini

KATAVI

Na Walter Mguluchuma

Mfuko wa Maendeleo na Hifadhi ya Jamii (TASAF) umeandaa mkakati makini katika kuwabaini wanufaika halali wa mfuko huo.

Akizungumza wakati wa kikao kazi cha kuwajengea uelewa wawezeshaji na madiwani wa Halmashauri ya Mpimbwe, mkoani Katavi, Ofisa wa TASAF kutoka makao makuu, Elizabeth Onesmo, amesema mbinu za kisasa kwa njia ya mtandao zitatumika katika kuepuka kuwamo wanufaika hewa.

“Hii itaondoa changamoto zilizojitokeza katika mpango uliopita. Tutatumia mtandao kubaini wanufaika stahiki,” anasema Elizabeth.

Anasema mkakati huo utasaidia kuepusha  kuweka wanufaika hewa kama ilivyotokeza katika baadhi ya halmashauri nchini kwenye mpango uliopita.

Elizabeth amewaasa wanufaika wa mpango wa TASAF sehemu ya pili, awamu ya tatu wa Halmashauri ya Mpimbwe kutumia fedha kwa malengo yaliyokusudiwa ili kujikwamua kiuchumi na kuondokana na utegemezi.

“Kuna wanufaika wanaotumia fedha hizo kinyume cha utaratibu wa mpango, hivyo kushindwa kufikia malengo waliyojiwekea,” anasema.

Mpango huu unatarajiwa kutekelezwa katika halmashauri zote 184 nchini kwa kuwafikia walengwa ambao hawakufikiwa na mpango uliopita.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mpimbwe, Silas  Ilumba, ameishukuru serikali kwa kuleta mpango huu kwa mara nyingine kwenye halmashauri hiyo.

“Hii itajibu maswali mengi yaliyokuwa yakiulizwa na wananchi waliokuwa wakidhani kuwa mpango huu umefutwa,” anasema Ilumba.

Anasema mafunzo waliyopata yatawafanya kuwa mabalozi wazuri kwa kuwaelimisha wananchi juu ya manufaa ya mpango huu.