DAR ES SALAAM

Na Pawa Lufunga

Shirika la Oxfarm Tanzania limewaasa wadau wa maendeleo nchini kuweka kipaumbele katika sekta ya kilimo ili kutokomeza umaskini.

Akizungumza katika warsha ya wiki mbili iliyowakutanisha wadau wa kilimo nchini, Ofisa Ushawishi wa shirika hilo, George Mwita, amesema kilimo ndiyo sekta inayochukua kundi kubwa la wajasiriamali na wazalishaji mali nchini.

“Sekta hii inaajiri zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania na kuchangia takriban asilimia 30 ya pato la taifa; na asilimia 30 ya bidhaa zote zinazosafirishwa nje ya nchi,” anasema Mwita.

Kwa upande wa mifugo, Mwita anasema sekta hiyo ndogo huchangia asilimia 1.4 ya pato la taifa na kuajiri asilimia 35 ya Watanzania huku Tanzania ikishika nafasi ya tatu kwa nchi zenye mifugo mingi Afrika.

“Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2020 -2025 inasema kilimo cha kisasa ndio msingi wa kujenga uchumi wa taifa na kina nafasi ya pekee.

“Ndiyo maana serikali imekuwa ikiweka mikakati mbalimbali kuwezesha sekta hii kuleta tija kwa wananchi na kwa pato la taifa,” anasema.

Baadhi ya washiriki wa warsha hiyo wakiwamo madiwani, wamebainisha kuwa kutokuwapo bajeti shirikishi inayotokana na mahitaji halisi kutoka kwa wakulima wenyewe ni moja ya changamoto zinazokikabili kilimo.

“Kuna tatizo la bajeti kutokuendana na unyeti wa kilimo ambacho ndio uti wa mgongo wa uchumi wetu. Sasa sisi tunapaswa kuishauri serikali kuhakikisha bajeti inakigusa kilimo katika nafasi ya pekee sana,” anasema Alice Mwangomo, Diwani wa Liwiti, mkoani Dar es Salaam.

By Jamhuri