DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Katika hali ya kushangaza, wiki tatu baada ya JAMHURI kuandika taarifa ya Balozi anayejihusisha na usafirishaji mabinti kwa njia isiyo halali, bado Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa haijachukua hatua yoyote.

Katika toleo namba 509 la Juni 29, mwaka huu kuliripotiwa taarifa yenye kichwa cha habari ‘Balozi ageuka kuwadi’, ikizungumzia kitendo cha Balozi wa Libya nchini, Ramadan Krista, kuwapeleka Libya mabinti wa Kitanzania bila kufuata taratibu sahihi.

Mabinti hao inadaiwa hupelekwa kutumikishwa kingono, ingawa Balozi Krista anasema huwapeleka kufanya kazi za ndani.

Awali, ofisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa aliliambia JAMHURI kuwa iwavyo vyovyote, kitendo cha Balozi kutumia madalali kutafuta wasichana na kuwapeleka Libya ni kinyume cha sheria na utendaji kazi wa kidiplomasia.

“Kesi kama hii ikithibitika kuwa ni kweli, lazima hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi yake,” anasema ofisa huyo.

Miongoni mwa adhabu za kidiplomasia kwa makosa kama hayo iwapo yatathibitika ni kuondolewa nchini kwa mhusika ndani ya saa 72.

Hata hivyo, tangu kutolewa kwa taarifa hiyo hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na taarifa kutoka ndani ya ubalozi zinadai kuwa sasa Krista ameamua ‘kusafisha’ ofisi yake.

“Habari ile ilipotoka tu, mambo yamebadilika. Balozi anawaondoa kazini wafanyakazi kila kukicha! Ndani ya wiki tatu, wafanyakazi watatu wamefukuzwa kazi. Anahisi ni wao ndio wanavujisha siri,” anasema mtoa taarifa wetu kutoka ndani ya ubalozi.

Inadaiwa kuwa fukuzafukuza hiyo haijazingatia sheria na taratibu za kazi, hasa kwa wafanyakazi wa ofisi za kidiplomasia.

Hata hivyo, mmoja wa wafanyakazi watatu walioondolewa kazini ameliambia JAMHURI kuwa hana tatizo na hatua hiyo.

Lakini hali ni tofauti kwa aliyekuwa dereva ubalozini hapo, Salim Hamis, kwani yeye anadai kuwa hajatendewa haki.

“Bahati mbaya hata watetezi wetu, Wizara ya Mambo ya Nje, hawatusaidii. Tunapeleka malalamiko, hayashughulikiwi na hali ikiendelea hivi, wafanyakazi wengi anaohisi wanafahamu siri zake wataumia,” anasema Hamis.

Hamis aliajiriwa Septemba 2015, mkataba wake ulitakiwa kwisha Desemba 31, mwaka huu.

Aprili mwaka huu, Balozi Krista akamsainisha mkataba mwingine wa mwaka mmoja, lakini amemuondoa kazini mapema mwezi huu.

Mwingine aliyekumbwa na fagio la Krista ni Judith Woisso, mhudumu wa Ubalozi wa Libya nchini.

“Nimeelezwa kwamba mkataba umekwisha, lakini sijapewa stahiki zangu,” anasema Judith.

Anasema Krista amemshauri kutojiunga na watu wanaompinga kwani ana nafasi ya kurudishwa kazini iwapo ‘atatulia’.

Judith, ambaye amedumu kazini kwa miaka 10, anasema kabla hajaondolewa kazini, Krista alimuonyesha barua akidai kuwa imetoka Libya, ikimuelekeza kuwaondoa kazini wote waliofanya kazi kwa muda mrefu; kwamba sasa mikataba mipya ni ya miaka mitano tu.

Hadi sasa wafanyakazi saba wamekwisha kufukuzwa ubalozini, zaidi ya asilimia 60 ya wafanyakazi wote.

Wengine waliofukuzwa kazi na bado wanadai stahiki zao huku wakizungushwa na maofisa wa Mambo ya Nje ni Salum Said, Ashura Hassan na Mwinyi Ramadhani.

“Ni zaidi ya mwezi sasa tunakwenda Mambo ya Nje kuomba msaada lakini hakuna anayetusikiliza,” anasema Ashura.

Alipotafutwa mkalimani wa Balozi Krista kutaka kujua ukweli kuhusu fukuzafukuza hizo, amejibu akisema: “Mimi sifahamu chochote kinachoendelea kwa sasa. Niko likizo.”

Mambo ya Nje wasuasua

Kwa upande mwingine, siku chache baada ya taarifa za Krista kuandikwa gazetini, JAMHURI limebisha hodi Wizara ya Mambo ya Nje kutaka kufahamu hatua zilizochukuliwa dhidi yake na tuhuma za kusafirisha nje mabinti wa Kitanzania.

“Kwani gazeti limeshatoka? Sisi hatujaliona. Magazeti yanayoandikwa kwa Kiingereza ndiyo ambayo taarifa zake hufanyiwa kazi haraka,” anasema ofisa mmoja wizarani hapo akiomba apelekewe nakala ya gazeti, ombi ambalo lilitekelezwa mara moja.

Kuhusu malalamiko ya wafanyakazi wa Ubalozi wa Libya, ofisa huyo anadai kuwa hayajafika kwenye dawati lake, suala linaloacha shaka kwamba huenda kuna kizuizi kinachokwamisha kwa makusudi barua kumfikia.

Alipofuatwa kwa mara nyingine wiki iliyopita, akamwelekeza mwandishi wa habari hii kuwasiliana na Ofisa wa Idara ya Afrika ndani ya wizara hiyo, Balozi Naimi Aziz.

Alipopigiwa simu na kuelekezwa kuhusu masuala ya Krista, Balozi Naimi alijibu akisema: “Kwa muda huu ninaingia kwenye kikao mara moja. Nipigie baada ya saa moja tuzungumze.”

Baada ya saa moja kupita, simu yake iliita bila kupokewa na hata ujumbe wa simu aliotumiwa hakuujibu.

Ujumbe huo unasomeka hivi: “Wiki tatu zilizopita tuliripoti taarifa kuhusu kashfa ya kusafirisha mabinti wa Kitanzania kwenda Libya kufanya biashara ya ngono.

“Anayetuhumiwa ni Balozi wa Libya nchini, Kamal Ramadan Krista. Je, kuna hatua gani zilizochukuliwa na serikali hadi leo?

“Balozi huyo pia analalamikiwa kunyanyasa wafanyakazi wa ubalozini kingono huku pia akiwanyima mikataba na kuwafukuza kazi hovyo. Malalamiko yao, mbali na kuandikwa gazetini yamefikishwa wizarani.”

Baada ya ujumbe huo kutojibiwa, JAMHURI likalifikisha suala hilo kwa Mkuu wa Kitengo cha Habari Wizara ya Mambo ya Nje, Emmanuel Buhohela, aliyeahidi kuyafikisha masuala yote hayo mezani kwa Waziri, Balozi Liberata Mulamula ambaye wakati huo alikuwa ziarani nchini Burundi.

Wanaharakati wanyamaza

Taasisi kadhaa zisizo za kiserikali zinazojihusisha na masuala ya haki za binadamu hazikuwa tayari kuzungumzia suala la Balozi Krista na kashfa ya kuwapeleka Libya wasichana kama lilivyoripotiwa na JAMHURI.

Ofisa Habari wa Msichana Initiative, Sara Beda, baada ya kuambiwa suala hilo, alijibu: “Nitakupigia baadaye.”

Baada ya hapo hakupokea simu wala hakupiga tena kwa wiki nzima iliyopita.

Mratibu wa Tanzania Human Rights Defenders Coalition (THRDC), Onesmo Olengurumwa, anasema:

“Hilo ni suala la kidiplomasia. Naamini wanalifanyia kazi. Watalichunguza na wakithibitisha, watachukua hatua.”

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Dk. Rose Ruben, hakufurahishwa na taarifa hiyo, akisema:

“Sina maoni yoyote kwa sababu stori hii haikufanyiwa uchunguzi wa kutosha.”

Alipoelezwa kwamba suala ni kukiukwa kwa haki za watoto wa kike na kusafirishwa nje ya nchi kinyume cha sheria huku TAMWA ikijipambanua kama watetezi wa haki za wanawake, Dk. Rose alishauri watafutwe Polisi wa Kimataifa (Interpol) na Idara ya Uhamiaji.

Mkurugenzi huyo ameonyesha kutofurahishwa na JAMHURI kuandika tuhuma dhidi ya mwanadiplomasia huyo.

1442 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!