‘Wametuangusha’

*Wananchi wawatupia lawama wabunge kuhusu tozo kwenye miamala

*Wamgeukia Rais wakimuomba atafute namna ya kufanya

*Profesa wa uchumi adai ingawa ni ngumu, inawezekana

*Wakala M-Pesa: Kuna ‘watu’ wanataka kumkosanisha Mama na wananchi

*Simu ya Azzan Zungu yawa yamoto, haipokeleki

DODOMA

Na Omary Moyo

Siku chache baada ya kuanza utekelezaji wa tozo mpya katika miamala ya simu, wananchi wamemwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati, huku wakiwalaumu wabunge kupitisha tozo hizo.

Julai 15, mwaka huu, kampuni za simu nchini zimeanza kukusanya tozo ya serikali, jambo lililozua mtafaruku miongoni mwa jamii, ikidaiwa kuwa makato ni makubwa kuliko uhalisia wa maisha ya Mtanzania.

Kodi hiyo iliyobatizwa jina la ‘kodi ya kizalendo’, ni ya makato ya fedha kwa anayetuma au kupokea kwa njia ya simu.

Wananchi wa Dodoma na Dar es Salaam wameliambia JAMHURI kuwa kwa siku chache tu tangu tozo ilipoanza kukatwa, maisha yamebadilika na kuingiwa hofu ya kuporomoka kipato na biashara.

Mmoja wa mawakala wanaotoa huduma za kifedha Mtaa wa Samora jijini Dar es Salaam, Frida Kilumbu, anasema makato hayo mapya yanawaumiza hata watoa huduma.

“Kila mtu anayekuja hapa analalamika. Hii maana yake ni kwamba muda si mrefu wateja watapungua, na sisi tutakosa kipato. Inatia hofu sana. 

“Serikali inapaswa kufahamu kwamba watu si kwamba wanakataa au hawataki kulipa kodi, hapana. Wapo tayari kabisa. Lakini uwekwe utaratibu rafiki ili kila mtu aridhike kutoka moyoni.

“Hofu yangu kubwa zaidi ni kwamba huenda kuna ‘watu’ wanataka kumharibia mama (Rais Samia). Wanataka kumkosanisha na wananchi,” anasema Frida.

Hoja yake inaungwa mkono na mmoja wa wateja aliyekuwapo kibandani kwake, Michael James, akishauri kiwango kipunguzwe.

“Serikali inataka fedha, wala hilo si tatizo kwetu! Lakini makato haya ni makubwa sana. Kwanini makato yasifanyike katika muamala mmoja tu kwa siku?” anahoji.

James anasema kuna watu hufanya malipo au huwalipa vibarua kupitia simu za kiganjani.

“Sasa kama una watu 20 halafu kila unayemtumia unakatwa na yeye anapotoa anakatwa si haki. Ingefaa nikatwe kwenye muamala wa kwanza halafu mingine ikatwe kwa kiwango cha zamani,” anashauri.

Anaungana na Frida akisema Watanzania wapo tayari kuchangia maendeleo ya taifa lao: “Lakini si kwa kiwango hiki! Au basi, tozo liwe upande mmoja. Anayetuma tu, anayepokea apokee kwa makato ya awali.”

Naye anamwomba Rais Samia kuingilia kati na kutoa tamko litakalowapa ahueni wananchi wengi.

Mkazi wa Ntyuka jijini Dodoma, Hussein Haji, anasema uamuzi wa tozo hilo umefanywa kwa utashi wa viongozi wa kisiasa bila kuwashirikisha wananchi ambao ndio wadau wakubwa katika kutuma na kupokea fedha kwa njia ya mitandao.

Anawapelekea lawama wabunge akisema: “Wamekuwa wakilinda masilahi yao. Wanafanya uamuzi wa ajabu unaoumiza wananchi waliowaweka madarakani.”

Haji anasema hali iliyofikiwa kwa sasa ni huruma ya Rais Samia pekee itakayoleta ‘suluhu’ mitaani.

Naye anaamini kuwa kodi ni muhimu kwa maendeleo ya taifa lakini inatakiwa kutozwa kwa kiwango rafiki, shirikishi na kilichokubalika kwa wadau wote; serikali na wananchi.

Mkazi wa Kikombo, Chamwino, Josephine Maligana, anasema suala hilo lilihitaji mjadala wa kina kabla ya wabunge kulikubali.

Anamnyoshea kidole cha lawama Mbunge wa Ilala, Musa Azzan ‘Zungu’, akidai kuwa ni yeye aliyependekeza bungeni kodi ya miamala ya simu kama chanzo kipya cha ‘mapato ya kizalendo’.

Anasema Zungu, hata kama alikuwa na nia njema, hakuangalia athari zake kwa Watanzania wengi wanaopata fedha katika mazingira magumu, hasa kipindi hiki cha janga la corona.

“Yeye alitakiwa kwanza kujadiliana na wananchi wake ambao ndio mabosi wake kabla ya kulipeleka bungeni. Muafaka ungepatikana na malalamiko haya yasingekuwapo,” anasema Josephine.

Wakazi kadhaa wa Mvumi, kilometa 40 kutoka Dodoma mjini, wanasema makato hayo yatawafanya kushindwa kumudu gharama za kutuma na kupokea fedha; na kwamba sasa njia ya rahisi iliyobaki ni benki.

“Lakini vijiji vingi nchini havina huduma ya benki. Matokeo yake tutarejea kwenye huduma ya mabasi kuepuka makato ingawa si njia salama.

“Lazima muafaka upatikane kwa pande zote mbili; serikali na wananchi, kujadiliana. Serikali isitumie mabavu kutoza tozo zisizo rafiki,” anasema mmoja wa wakazi wa Mvumi, Alex Mkunda.

Anasema anaamini kuwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, ni mzalendo na anawajali wanyonge, lakini katika hili ameshindwa kupata njia sahihi.

Mmoja wa wabunge wa Mkoa wa Dodoma ambaye hakutaka kutajwa gazetini, anasema amepokea malalamiko kutoka kwa wananchi wengi kuhusu tozo hiyo.

“Kwa hiyo ninaandaa mkutano wa hadhara jimboni kuzungumzia suala hili. Serikali ina nia njema katika kuleta maendeleo, na bila kodi hakuna maendeleo,” anasema.

Baadhi ya mawakala waliozungumzia suala hili wanaungana na hoja ya kumuomba Rais Samia kuingilia kati na kuwasaidia Watanzania wanyonge.

“Mawakala wengi ni wajasiriamali wadogo wenye mikopo benki. Tunaomba mama alishughulikie suala hili kutuokoa sisi na familia zetu. Watanzania wengi hatuna uwezo wa kulipa kiwango cha tozo kilichopangwa,” anasema mmoja wa mawakala waliopo Makoye, mkabala na CBE jijini Dodoma.

Serikali inaweza kuondoa tozo?

Akizungumzia uwezekano wa serikali kupitia upya na kuondoa tozo hiyo iliyozua malalamiko makubwa nchini, Profesa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Kampusi ya Dar es Salaam, Honest Ngowi, anasita kutamka moja kwa moja.

“Bajeti imeshapita na maoni ya wadau ndiyo haya. Wadau wanaona tozo hizi ni mzigo. Lakini kimsingi bajeti ikipita, imepita.

“Kama italazimika ‘ku-review’, basi lazima tuje na chanzo mbadala cha mapato, vinginevyo bajeti itakuwa na nakisi,” anasema Profesa Ngowi.

Profesa huyo anasema namna nyingine ni kusubiri hadi mwaka huu wa fedha utakapokwisha ndipo tozo ziondolewe, au kufanyike ‘mid-year budget review’.

“Lakini katika maisha lolote linawezekana. Serikali inaweza kusikiliza kilio cha wananchi,” anasema.

Mwanasheria na Wakili mkazi wa Morogoro, Everest Mnyele, anasema katika maisha yake hajawahi kuona tozo kubwa kama hili la sasa.

“Kwa malalamiko haya serikali inaweza kujikuta inakosa mapato iliyotarajia. Kodi inapaswa kukusanywa kutoka kwenye ‘broad customer base’. Kodi itoke kwa watu wengi hata kama ni ndogondogo.

“Sasa tozo kubwa kama hii itawafanya watu watafute njia mbadala. Maana yake wataacha kutumiana fedha kwenye simu,” anasema Mnyele.

Anasema ni vema kuwa na tozo rafiki ambazo hazina maumivu kama zinazotozwa kwenye muda wa maongezi.

Wakili Mnyele anahoji ni wapi suala hili lilikoibukia, kwa kuwa awali haikudhaniwa kungekuwa na kodi hii.

“Kilio ni kikubwa, ni muhimu sana kwa serikali kurejea na kurekebisha suala hili. Uwezekano huo upo. Ingawa Mwigulu anasema serikali itaingiza Sh trilioni 5 kwenye mzunguko wa fedha na kwamba hiyo itamaliza malalamiko, sidhani kama itawezekana, kwa kuwa siku zote fedha huwa hazitoshi,” anasema.

Mnyele anahofia kwamba huenda tozo hizi zikasababisha kudorora kwa ujasiriamali nchini.

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Dk. Rose Ruben, anasema tozo za miamala ya simu zimeongezwa mara mbili kuliko uwezo wa mtumiaji.

“Ukiangalia viwango vyake utagundua vimepandishwa zaidi ya mara mbili wakati kipato cha Mtanzania kimebaki palepale,” anasema. 

Tozo iliyoongezwa wakati wa kutuma au kutoa fedha anasema ni sawa na matumizi ya kawaida ya familia ya Mtanzania kwa siku.

“Sh 15,000! Kuna familia hutumia kiwango hiki cha fedha kwa chakula kwa siku mbili hadi tatu,” anasema Rose na kuongeza kuwa kuna hatari wananchi wakaachana na kutumiana fedha kwa simu na kurejea kwenye kutumiana fedha kama vifurushi vya mizigo.

Anasema hali hiyo haitasababisha hasara kwa Mtanzania, bali pia itasababisha kampuni zilizowekeza katika huduma hiyo kuathirika.

Dk. Rose anasema pia kwamba tozo kubwa zitasababisha ushindani wa kampuni zinazotuma miamala kwa njia ya simu kupungua, kwa sababu watakosa nguvu ya kuhamasisha watu wengi kutumia huduma yao.

“Suala hili linahitaji kutolewa ufafanuzi na Waziri wa Fedha, kulielekeza kwa Rais ni kukosea kwani yeye siye aliyelianzisha,” anasema.

Zungu hapokei simu

JAMHURI limemtafuta Mbunge wa Ilala, Zungu kutaka kupata maoni yake juu ya suala hili.

Alipopokea simu, akajibu kwa ufupi: “Andika ujumbe.”

Alipoandikiwa ujumbe, Zungu hakuujibu na hakupokea tena simu kwa siku mbili alizotafutwa na mwandishi wa habari hii.

Mataifa kadhaa yamewahi kukumbwa na kadhia kama hii ya kuingiza kodi kwenye miamala ya simu. Mataifa hayo ni Uganda, DRC, Ivory Coast na Malawi na kote serikali ililazimika kurejesha utaratibu wa awali.